KWANI SALAMU KILO BEI GANI ?
Kwenu msiopenda kusalimia na kusalimiwa,
Kuvulini kwetu wamenituma niwaambie ama niwapashe mpashike kuwa tabia hii mliyonayo ni chafu na inatia kichefuchefu. Tabia yenyewe ni ya kuwa wazito katika salamu. Kwanza hamna utaratibu wa kusalimia watu na mbaya zaidi hata mkisalimiwa hampokei salamu na kama mnapokea basi ni kama mnalazimishwa. Kwani hamjui kuwa salamu ndiyo kipimo cha awali cha ustaarabu wa mtu ? Basi habari ndiyo hiyo.
Watu wa kivulini kwetu wamewachokeni kwa tabia hiyo ya ovyo. Ikiwa hata mbwa, kuku, nyani na wengineo wakikutana wanasalimiana sembuse wewe mwanadamu usiyekuwa na mkia. Kumbe ubinaadamu wako umekalia wapi; miguuni kiunoni ama kichwani ? Kwa kweli mnaudhi.
Nalisema hil ili liwatue vizuri vichwani mwenu. Ebu tuelezeni, tabia hiyo ni kwa vile mna pesa sana, ama ni kwa vile mmesoma sana ama ni kwa ajili gani. Na mseme pia kama mkiwasalimia watu ama mkiitikia salamu za watu mtapungukiwa nini. Na kama mnajua bei ya salamu huko mnunuako tuelezeni salamu kwa kilo mnauziwa bei gani ? Mbona sisi tunajua salamu hazina gharama.
Utawakuta watu hawana cha pesa, hawana cha elimu, hawana sura nzuri; kwanza miguu yao yote ni ya kushoto lakini mabahili kwa salamu kushinda hata nyoka. Nini hasa kinawasumbua ? Mmelogwa ?
Wenyewe ukiwabana utasikia wanasema kwani salamu ni lazima; kwa taarifa yetu ili mradi nyinyi ni binadamu na tuko nanyi katika jamii hii, salamu ni lazima. Ni lazima kwa sababu hatima yako wewe ni kifo na siku ukifa hatutakuacha barabarani utuozee utunukie; tutalazimika sisi kubana pua zetu kukuzoazoa na kwenda japo kukutupa jalalani; sasa sisi utatulipa nini na kipindi hicho kujitambui. Maiti hazikwi na pesa, hazikwi na vyeti, wala hazikwi madaraka, anazikwa mtupu kama alivyozaliwa; sasa mnalinga nini nyie.
Jambo jingine ni kuwa wewe ni binadamu eti siyo tumbili; na binadamu kama walivyo viumbe wengine tuna taratibu zetu ambazo ni lazima zifuatwe ili tukukubali katika jamii; vinginevyo hamia msituni ukaishi na mafisi wenzio utuache sisi tusalimiane; kwanza hutulishi, hutuvishi na wala wewe sio barabara kusema tutapita wapi.
Ninaongea hivi kwa hasira kutokana na kukerwa. Mtu anakuja msibani anawakuta watu wamejaa, hana salamu hana cha nini anakaa kwenye kiti na kuendelea kubonyezabonyesa kasimu kake ka mchina; hata kuwashika mikono wafiwa anaona tabu; kumbe kilichomleta pale kitu gani. Ama mtu anaingia katika ofisi ya watu hasalimii wala haulizi getini; ili mradi alikwishaongea na mwenyeji wake kuwa atakuja basi. Ama jirani yenu kila siku akiingia au akitoka hasalimii majirani. Hawa ndio wanaosababisha majirani wanafungulia muziki mpaka sauti ya mwisho siku wanaumwa ama wamefiwa katika vyumba vyao.
Hii ni mara yangu ya mwisho kuwakumbusha nyinyi takataka msiojua maana na umuhimu wa salamu; kwamba kuwakumbusha huku si kutaka chochote kutoka kwenu bali ni kuwafahamisha kuwa ubinaadamu kazi hivyo lazima muwajibike kama binaadamu hata kama mlilelewa ndivyo sivyo; salimieni na pokeeni salamu; vinginevyo nendeni mkaishi na majongoo vichakani; mtuondolee kiwingu.
No comments:
Post a Comment