VALANGATI KIVULINI
Ndugu zangu leo Kivulini kwetu kumetokea valangati la kufa
mtu.
Majira kama ya saa tano asubuhi maeneo ya mtaa wa madukani niliukuta umati wa watu wakishuhudia patashika nguo kuchanika baina ya
akinamama wawili. Vurugu iliyokuwapo pale ilikuwa si ya kuzimwa na wapita njia.
Mungu ashukuliwe baada ya msukosuko mkubwa kwa bahati wakapita askari wa Tigo
na pikipiki lao ndio waliofanikiwa kumaliza kasheshe ile tena baada ya kulipua
kabomu kadogo ka kutoa machozi.
Utulivu uliporejea nikapata fulsa ya kuongea na mmoja wa
mashuhuda waliokuwepo kutoka mwanzo ili nijue chanzo cha kadhia hiyo; ndipo
nilipopewa mkanda mzima.
Chanzo chetu cha habari kinasema kisa cha ugomvi huo ni
mwekezaji wa ndani ambaye ana hotelibaa pale mtaani palipotokea ugomvi.
Inasemekana mwekezaji huyo alikuwa amemwajiri dada mmoja kutoa huduma katika
mradi huo ambaye kutokana na umahiri wake na bidii yake ya kazi akaamua
kumuongeza jukumu la kumhudumia pia yeye mwekezaji binafsi.
Chanzo chetu cha habari kinaendelea kumwaga cheche kwa
kusema kuwa baada ya kipindi kifupi tokea mwekezaji huyo amtunukie shahada
mhudumu wake akatokea mteja mmoja wa kike ambaye naye kutokana na umaarufu
wake katika ile hotelibaa ikapelekea mwekezaji kumtunukia medali ya uteja wa
kutukuka na hivyo mbali ya kuwa mteja katika mradi akawa pia mteja wake
binafsi.
Changanya kanganya hii iliendelea kwa kipindi cha kama mwezi
mmoja hivi bila mteja bora na mhudumu mahiri kutambuana kuwa wapo katika
kujenga nyumba moja. Wenyewe wakawa wanacheka na kuchangamkiana sana kiasi cha
kuwa mashosti. Lakini wapo baadhi ya wateja na wahudumu katika kiwekezwa hicho ambao walikuwa wanajua
kuwa urafiki huo ulikuwa ni wa mashaka; kwamba walikuwa wakila sahani moja bila wenyewe kugusana mikono.
Kikichotokea leo ni kama ajali. Ilikuwa ni kawaida kwa
mwekezaji kumpa kinoti kama kibali mteja bora kumpelekea mhudumu mahiri ili apewe huduma aliyokuwa anaitaka na pesa
atalipa atakapojisikia. Kwa bahati mbaya leo aliandika vinoti viwili; kimoja
cha huduma kwa mteja na kingine cha huduma kwa mwekezaji; vikiwa katika karatasi
zinazofanana. Kwa uzembe wa mteja bora alipofika kwa shosti wake akajichanganya
na kutoa kinoti cha huduma binafsi ya mwekezaji ambamo ndani ya kinoti hicho
kulikuwa na jina la mteja bora lililoanza na haneei, likifuatiwa na saa ya kukutana, mahali pa kukutana, nini cha
kufanya na mambo mengine ambayo hayaandikiki na chini ya kinoti hicho kulitiwa
saini kwa mbwembwe na mwekezaji mwenyewe.
Mhudumu mahiri baada ya kupokea kinoti hicho kwa makosa na yeye
akakosea kumhoji kwa kumuuliza mteja bora ana maana gani kumpatia ujumbe ambao si wake ama
ndiyo kantangaze anaianzia kwake. Mteja bila kengere kogonga kichwani kwake
akahoji kuwa kama ujumbe haumuhusu maneno yote hayo yanakujaje; kwani inahuu..
Majibizano yakiwa katika hatua za awali, mara akaingia
mwekezaji pale hotelibaa; kuingia kwake ikawa kama unazima moto kwa kupulizia
gesi asilia. Yakaanza kurushwa maneno, jembe, matusi, vitisho, kutoka pembe
hadi pembe; aliyekuwa na masikio ya chuma alisikiliza na mwenye masikio ya mbao
alisalimisha masikio yake maana matusi
na kashfa zilizokuwa zikimwagwa pale zilikuwa ni mpya kutoka dukani ambazo zilikuwa hazijawahi kutumika.
Kana kwamba hiyo haitoshi vitendea kazi na bidhaa zikaanza kutumika kama
silaha za mapambano na ukumbi wote wa biashara ukawa mbengelembengele; vurumai hadi barabarani. Ilibidi ili
kujenga heshima mwekezaji aingie mitini na kuacha gari liende bila dereva maana mambo sasa yalikuwa si mambo.
Baada ya kupata taarifa hiyo nikabaki ninajiuliza kufanya
vurugu kiasi hiki wale akina dada mashosti wakati wote ni madoezi maana yake nini
na yule mwenye mali aliyeko nyumbani afanyeje ? Na huyu mwekezaji naye huu ndio kweli
utaratibu wa kuwekeza; kwa kuwa na mhudumu mpaka binafsi na mteja mpaka binafsi.
Kwa staili hii uchumi kivulini kwetu utaimarika kweli ?
No comments:
Post a Comment