Monday, 25 August 2014

NGANO ZA KALE

            HEKAYA ZA SUNGURA


Ipo hadithi moja ambayo wengi wetu hatuijui yote bali tunaijua kipande tu; hadithi hii ni ya Sungura mjanja na ndizi mbichi.

Inasemekana kuwa hapo zamani za kale SUNGURA mjanja alikwenda kondeni ambako kulikuwa na migomba ambayo mingi kati yake ilikuwa imebeba mikungu ya ndizi.

Siku hiyo ambayo Sungura aliingia katika shamba hilo alikuwa na njaa sana lakini kwa bahati mbaya mikungu karibu yote ilisheheni ndizi zilizokuwa mbichi japo zilikuwa zimekomaa.

Kutokana na njaa aliyokuwa nayo akaona ni heri ajaribu kufanya maarifa apate japo ndizi kadhaa chache aweze kutuliza njaa yake na ikiwezekana kiasi apelekee wanae. Kwa kutumia nguvu zilizokuwa zimebaki mwilini mwake akatikisa kila mgomba ili aweze kupata chochote; lakini bahati haikuwa yake; hakuna hata ndizi moja iliyoanguka; alichoambulia ni uchovu zaidi.

Baada ya Sungura kuona mambo yameshindikana akaamua kutoka kwa hasira huku akisema SIZITAKI.....MBICHI HIZI. Wakati akiyasema hayo Sungura hakujua kuwa hakuwa peke yake katika lile shamba; alikuwepo SHORE pia. Shore alimwonea huruma sana sungura kwa namna alivyochoka  na  kunyong'onyea kwa njaa kiasi cha kutembea kwa shida kuelekea kwao. Hakumsemesha hata neno moja akamwacha aende zake.

Baada ya siku mbili karibu shamba zima la migomba  ndizi zote ziliiva. Kwa kuwa Shore alikuwa habanduki shambani hata kama ndizi ni mbichi; kwa kuona zimeiva  akamkumbuka Sungura. Akaamua akamwite aje shamba ale kwa kadri atakavyoweza.

Kwa bahati Shore akamkuta Sungura maskani kwake akamwomba wafuatane kwenda shamba. Sungura mwanzoni alikataa katakata kuwa yeye hana haja ya ndizi kwanza ndizi zenyewe mbichi. Lakini baada ya kubembelezwa sana akaamua aongozane na Shore kwenda shambani.

Walipofika shambani Sungura hakuamini macho yake kwani ndizi zote zilikuwa zimebadilika rangi. Shore akamwambia Sungura aanze kutikisa migomba. Katika kutikisa mgomba wa kwanza tu zilidondoka ndizi ambazo kwa siku ile Sungura na familia yake hawangeweza kuzimaliza.

Akiwa mwenye furaha Sungura akamwuliza Shore kuwa amejuaje kuwa ndizi zile zilikuwa zimeiva. Shore akamwambia kuwa yeye huwa habanduki shambani hata kama ndizi mbivu zimeisha bali hukaa humo humo shambani akila matunda mengine hadi ndizi mbichi zinaiva. Hapo ndipo Sungura alipomwangalia Shore kwa mshangao na kutikisa kichwa huku akisema " ama kweli MVUMILIVU HULA MBIVU".

No comments:

Post a Comment