Wednesday, 17 December 2014

GUBU

     GUBU LILIVYO



Kuna tabia ambayo watu wengi wanayo; tabia ambayo bila ya wao kujua huwa inawakera wengine na kuwakwaza vilevile. Tabia hii ni ya Gubu.


Mtu mwenye gubu anakera sana kwani daima huwa hana jambo dogo kwake; kila jambo liwe la maana ama la kipuuzi ataliongea kwa muda mrefu na mara kwa mara kiasi kwamba msikilizaji unaweza kuamua kumtoroka  kwa kuchoshwa na kuongelea jambo hilo hilo kwa muda mrefu.


Mtu mwenye gubu daima huwa ni mlalamishi, hashauriki, hajui kusamehe na baya zaidi huwa hakubali makosa. Yeye daima hujiona ndiye anayestahili na kwamba yeye ndiye huwa benki ya matatizo.


Mtu mwenye gubu neno lake halisahauliki; aliliongea jana, leo analiongea na kesho lazima ataliongelea.


Mtu mwenye gubu mada zake hazibadiliki; kama ni sera za chama, mambo ya mpira, au matukio ya jamii; basi kila anayekutana naye. bila kutafakari kuwa anapendelea jambo hilo au hapendelei; yeye ataanza kufunguka. Na haishii hapo atasogea pengine, napo ataendelea na jambo lilelile.


Mtu mwenye gubu huwa hampendi kabisa mtu asiyemsikiliza aongeapo mambo yake, humpenda sana anayemuunga mkono na kumshangilia hata kama anaongea utumbo.


Mtu mwenye gubu daima ni mtu wa visasi, vitisho na mbwembwe nyingi sana; usipomjua unaweza kuingia mkenge ukadhani hakuna mwingine zaidi yake.

No comments:

Post a Comment