Friday, 19 September 2014



    E- MAIL KUTOKA KWA KOMREDI PEE CHOU

Wakati tukiwa katika ziara yetu kuzunguka Kivulini kwetu tumepokea e mail kutoka kwa rafiki yetu komredi Pee Chou ambayo kutokana na uzito wa ujumbe uliokuwemo tumeonelea tuuweke wazi ili angalau na wapenzi wa Kivulini kwetu muweze na nyinyi kupata vionjo vyake.

Ujumbe huu ulikuwa ni wa  kutusalimu na juu ya salamu hizo ulikuwa ukieleza mambo yafuatayo:

1.           Ndugu Pee Chou alikuwa akitupa pole kwa misukosuko ambayo tunakabiliana nayo kwa sasa ya  kiuchumi, kijamii na hasahasa kisiasa.


2.          Ndugu yetu alikuwa akitutahadharisha kwa kutueleza kuwa tukiendelea kucheka na manyani basi  tujiandae kuvuna mabua. Alidai huko kwao hawaoni aibu kumzamisha baharia mmoja au nahodha mkorofi ili mradi kuhakikisha kuwa meli imefika nchi kavu salama iliwa na abiria   wengi.


3.          Ndugu yetu alituonya sana kuhusu suala la kuwa wema kupita uwezo. Alitushangaa 
             sana tunapokuwa waungwana hata kwa watu wasiokuwa na fadhira wala staha.
            Alisema huko kwao wakitaka kumwua nyani hawamwangalii
             usoni.


4.          Pee Chou alituonya juu ya imani yetu kuwa sisi tumebarikiwa na ni nchi teule ambayo haitakuja kuharibika siku zijazo. Alituasa sana sana tusijidanganye. Amani siku zote hulindwa kwa gharama zozote kwa sababu siku ikipotea ni kama kudondosha sindano ndogo usiku kwenye msitu wa nyasi.


5.         Ndugu yetu alituonya tusiwaendekeze watu ambao kwanza hawana hata faida kwa nchi. Aliomba tumjali sana mzalendo na mpenda nchi na yeyote mpenda fujo na vurugu azomewe na kudhibitiwa mapema kabla hajaleta madhara katika nchi kwa sababu ujinga wa mtu mmoja unaweza kuliangamiza taifa zima.


6.         Pee Chou alisema kuwa tusisahau kuwa kitulacho ki nguoni mwetu.

 Hayo ndiyo yaliyokuwemo katika e mail hiyo. Sisi wa Kivulini kwetu hatuna maoni yoyote juu ya e  -  mail hiyo zaidi ya kumshukuru ndugu yetu Pee Chou kwa kututumia maoni haya kwa 
 wakati muafaka.

No comments:

Post a Comment