Tuesday, 7 October 2014



            SUALA LA UCHAFU

Kivulini kwetu safari hii tunataka kuongelea suala la uchafu katika mji wetu. Suala hili limekuwa kama tabia na inaelekea tabia hii inaimarika sana na kuwa utamaduni wa jamii yetu.
Kama tujuavyo uchafu ni takataka; lakini pia uchafu ni hali ya kutokuwa msafi. Uchafu pia inaweza kuwa tabia ya mtu au watu kutokuwa wasafi.
Wakati tukitathmini uchafu kuna namna nyingi ya mtu au watu kutokuwa wasafi.
Namna ya kwanza ambayo ni rahisi kuelezeka ni tabia ya watu kutoona kinyaa kukaa katika mazingira yenye takataka kama vile masalia ya matunda, matambara, makaratasi na kadharika. Lakini pia kukaa mahali penye uvundo ama panapotiririka maji machafu, kwenye mifereji michafu na kadharika.


Uchafu mwingine ni tabia ya kutotunza mazingira kwa kutupa taka ovyo, kula ovyo, kuvaa ovyo na kadharika.


Uchafu mwingine ni kutokuwa na mpangilio mzuri wa vitu hata kama vitu hivyo ni visafi. Mfano katika mji ni kuegesha magari ovyo, kupanga bidhaa ovyo hadi barabarani, ujenzi holela, migongamano isiyo ya lazima, kufanya shughuli zozote mahali pasipostahili kama kupika sehemu za wazi, kulala kwenye mavaranda, kuosha magari barabarani, gereji kwenye makazi ya watu, vituo vya mafuta kwenye makazi ya watu, viwanda vya jua kali mahali pasipostahili na mengine mengi ya aina hiyo

.
Baada ya kufuatilia kwa karibu tumegundua kuwa chanzo cha hali hii ni mamlaka husika za mji kutowajibika katika kusimamia sheria na taratibu za mji. Aidha si kutosimamia tu bali kutokuwa na mipango au utaratibu endelevu katika kuuweka mji namna unavyopasa kuwa.


Mamlaka zimeshindwa kutoka maelekezo fasaha na kwa wakati juu ya kipi kifanyike, wapi kifanyike, nani afanye na afanye wakati gani. Na juu ya hayo kueleza wazi kuwa atakayekiuka maelekezo hayoatafanywa nini na kweli inapotokea mtu kakiuka basi hatua zichukuliwe.


Kinachojitokeza ni kusimamia machache baadhi na kusimamia kwake ni kinyume na inavyotakiwa; kwamba upo upendeleo kwa baadhi ya watu, kwa baadhi ya maeneo na baadhi tu na masuala yote yanayotakiwa kusimamiwa. Matokeo ya kufanya hivi ni jamii nzima kuachwa njiapanda watu wasijue ni kipi sahihi kufanyika na nani anapaswa kufanya kwani katika eneo moja, watu wa aina moja, katika muda unaofanana; wapo wanaoruhusiwa kufanya na wapo wanaozuiwa kufanya kitu kilekile, mahali palepale na katika muda uleule.


Chanzo kingine cha uchafu ni tabia ya mtu mmoja mmoja ya uchafu. Hii inatokana aidha na malezi, ukosefu wa elimu, umaskini na mlengo wa kushoto wa mawazo.


Kitendo cha mtu kula matunda na kutupa maganda barabarani, kitendo cha mtu kunywa maji au soda na kutupa chupa katika mfereji, tabia ya mtu kuuza bidhaa zake dukani na makasha, maboksi, na vifungio vingine ovyo mbele ya duka lake, vitendo vya watu kujisaidia haja kuwa na ndogo katika mifereji ya majitaka wakati mwingine mchana kweupe, vitendo vya kupanga bidhaa za chakula juu ya maji yanayotiririka na kuwauzia watu na hata wao pia kununua; lakini mbaya zaidi kitendo cha kuona haya yote yanafanyika na kuacha kuyakemea; yate haya yanajumuika katika tabia ya uchafu. Watu wamekuwa hawaoni vibaya juu ya masuala haya na imekuwa ni kawaida.


 Hujitokeza kuacha kwa muda pindi wanapotangaziwa na mamlaka waache kutokana pengine na milipuko ya magonjwa ama kuwe na ugeni unakuja Kivulini kwetu. Katika harakati hizo za kuzuia uchafu watu hulalamika sana kuwa wanaonewa na kunyanyaswa katika nchi yao kwa kuambiwa waachane na uchafu. Baada ya milipuko na ugeni kuondoka hali ya uchafu hurejea mahali pake. Kwa hakika inasikitisha sana.


Binafsi nilidhani ipo haja kwanza ya jamii ambamo na wenye mamlaka wanatoka humo ibadilike na kuchukia mazingira machafu. Tuwe jamii yenye kuona kinyaa  kukaa kwenye majalala, kutupa taka ovyo, kujisaidia ovyoovyo, kununua vitu vichafu, kuvaa mavazi machafu, sisi wenyewe kutokuwa wachafu; kwa sababu nakumbuka kuna siku alipanda mtu mmoja kwenye daladala(simtaji jina, siitaji jinsia yake, dini yake wala kabila japo niliulizia na vyote nikaambiwa) kila abiria ilibidi afunge pua; lakini hiyo haikutosha wakaomba mtu huyo ashushwe vinginevyo wao washuke; ikabidi ashushwe kituo kinachofuata; kwani kwa jinsi alivyokuwa ananuka ni afadhari ya kinyesi; unaweza kupata hiyo picha kuwa mtu huyu anatoka wapi na amewakera watu kiasi gani katika maeneo yote aliyopita. Mtu kama huyu kuna uchafu gani utakaomtisha akaogopa ?


Lakini juu ya jamii kujirekebisha, mamlaka nazo ziweke utaratibu mzuri wa kufuatwa. Kuwe na sheria za kufuatwa ili kuweka mji katika usafi. Taratibu zizuie baadhi ya mambo yanayosababisha uchafu kufanyika na taratibu hizo zisimamiwe bila ya ubaguzi wala upendeleo na usimamizi huo uwe endelevu na sio zima moto.
Ninasali ije itokee kipindi na sisi tukawa wasafi, katika mji safi wenye  kupendeza.

No comments:

Post a Comment