ACHENI KUTUSINGIZIA
Kivulini kwetu jana tulikutana kujadiliana juu ya upuuzi huu ambao umekuwa kila siku ukifanywa na wanasiasa uchwara na wanaharakati njaa kuwa kila waliwazalo wao hushindwa kuliwasilisha kama mawazo yao na kusingizia kuwa ni matakwa ama mawazo ya wananchi.
Nasema tulijadili kwa pamoja tukaamua kutoa tamko kuwa tuwapashe na kuwaeleza wazi kuwa waache kabisa kama sio kukoma kudumisha harakati zao juu ya vichwa vyetu.
Kwa hali ilivyo sasa jamaa hawa ni vema wakajua kuwa kuna kila fulsa na kila nyenzo za kumwezesha kila mwananchi kuwasilisha mawazo yake popote na wakati wowote juu ya nini anawaza, nini anahitaji na kipi hakitaki. wananchi wa sasa wamesoma na wana upeo wa kufikiri na uwezo mkubwa wa kuzungumza. Wananchi wa sasa si watu wa kusemewa na si mbumbumbu kiasi cha kila siku kusingiziwa kuwa wanataka hili ama wanataka lile. Kama wazo lako ni jema au zuri kwanini usiliseme kama wewe na badala yake unatafuta uzito kwa kusingizia kuwa ni wazo la wananchi, walikutuma lini ?
Inaudhi sana kumkuta mtu mzima na masharubu yake kasimama jukwaani anatoka mapovu akijidai anawasilisha maoni ya wananchi; yeye kama nani awasemee watu na anaowasemea wako wapi. Na katika udhaifu, na uvumilivu walionao wananchi hawamkemei wala kumzomea; wanamsikiliza kwa matumaini kuwa pengine atakuwa na jipya la kuwaeleza; mpaka muda unakwisha wanabaini kuwa alichongea ni pumba tupu toka mwanzo hadi mwisho.
Mwanzoni baadhi ya majimbo tulikuwa tukiwasilishiwa mawazo yetu na wabunge bungeni; imefikia sasa mbunge wengi hakanyagi kabisa majimboni na wala hawana mawasiliano na wapiga kura wao, lakini mbunge huyohuyo akifika bungeni anaongea kama kasuku mambo na mawazo aliyoongea na mkewe kwa kuyafanya ndiyo mawazo ya wananchi; toka lini mke wako akawa ndiyo wananchi. Acheni mambo yenu.
Ukitaka jaribu kuyafuatilia anayoyasema; utakuta ni mambo tofauti ya jinsi ilivyo katika jimbo lake. Kwa wale ambao wanawasiliana na wapiga kura wao ni sahihi kuwasemea kwani walitumwa; lakini hao wengine ambao nawasema leo ambao siku hadi siku wanaongezeka idadi kwa kweli ni kero tupu na wanayatia aibu majimbo yao.
Na hao ambao kila uchao huitisha mikutano na waandishi wa habari wakidai wanatoa hoja za wananchi ama wanadai haki za wananchi, hivi ni wapi wanakaa na wananchi tunawaeleza kuwa hivyo ndivyo tunavyotaka. Utasikia wananchi hawataki hiki ama wanataka kile; cha ajabu haohao tena wanadai kuwa tutawahamasisha wananchi wasikubali ama wakubali; kama ni kweli wanachosema ni mawazo yetu iweje waje tena kutuhamasisha tukubali ama tukatae; si watuache tu tutakubali au kukataa wenyewe kwa wakati wetu; waokoe muda wautumie kulea watoto wao. Kinachoonekana sasa ni watu kutumia vyama na taasisi kuomba chochote kwa wajomba zao kwa kusingizia kuwa wanakuja kutusaidia wananchi kumbe wezi wakubwa. Tumewachoka wezi hawa na ipo siku tutawapiga mawe wakija kivulini kwetu. Harakati hizo na siasa hizo tumezichoka. Mambo ya kujenga magorofa juu ya vichwa vyetu tumeyastukia; kila siku nyinyi tu ndio mnaojua mawazo yetu nyie mawazo yenu anayajua nani; ebu oneni haya msidhani hatujui ujanja wenu na vitaasisi vyenu feki.
No comments:
Post a Comment