Friday, 1 August 2014


NGANO ZA KIVULINI


     MAKUBWA KIVULINI

Siku moja majirani tulikuwa kivulini tunapunga upepo huku tukiwa na maongezi ya hapa na pale. Tulikuwa watano; wanawake wawili na wanaume watatu. Tukiwa hatuna hili wala lile akaja mzee mmoja naye jirani yetu vilevile. Akatusalimu na kasha anaanzisha mada mpya kabisa. Akasema, hebu tuwe wakweli na kila mmoja atoe mchango wake kwa moyo wote; mmoja mmoja kila mtu aseme anawaza nini hapo alipo; nini tatizo lake kubwa ambalo linamla akili. Kwanza tulitazamana, tukacheka na baadae mmoja wetu kwa jina bwana Juma Kilobaki akaanza kijieleza:

JUMA KILOBAKI:  “Ndugu zangu, kusema kweli mimi ninalowaza ni kuwa nitajikomboaje katika hii hali. Kwanza, mwanangu jana karudishwa kutoka shuleni anadaiwa ada sh.300,000/=. Pili, nimeletewa taarifa kutoka nyumbani kuwa mama mzazi kalazwa hospitali; hana damu, figo moja haifanyi kazi, na mapafu yamejaa maji; kwenda tu kumuona lazima niwe na 250,000. Tatu,nilikuwa nimekopa Benki ya Posta kwa kila mwezi kurejesha sh. 180,000/= na tarehe ya marejesho ilikuwa juzi. Nne, nimepata simu muda sio mrefu kuwa mama mkwe yuko njiani anakuja kutusalimia; yeye na wajukuu zake wawili; lakini hapa nilipo senti tano kipande sina…..!”

Tulikuwa kama tumekubaliana; wote tukasema “…du !”. Wa pili nikawa mimi……nikaanza “ Jana nililetewa taarifa kuwa kuwa watoto wa mjomba(mtu na dada yake) wamepeana mimba. Mjomba mwenyewe amekwisha pata habari juu ya suala hilo lakini yupo safari; kesho anarudi. Keshatoa maagizo kuwa asiwakute watoto hao nyumbani kwake. Mkewe kaja nyumbani analia nimsaidie. Sasa ninawaza nianzeje.”

Ikaja zamu ya Mama Sakina; yeye akaanza lake “…jamani mwenzeni nina tatizo. Mkilisikia mnaweza kudhani dogo lakini……leo ni karibu mwezi lakini amini usiamini kila siku ya mungu nikilala usiku ninamuota mume wa jirani yangu nimelala nae. Yaani ndoto hiyo imenichosha maana nikiamka nikilala tena ndoto ni hiyohiyo…sijajua nimelogwa, ama nina jinni ama vipi…..sielewi kwa kweli”

Aliyefuata alikuwa Eliza. Yeye nae alikuwa na lake. “Mwenzenu mimi tatizo langu  ni ndoa. Kila saa nawaza huu ni mwaka wa 35 lakini haijatokea hata katika utani mwanamume yoyote kunitamkia ndoa. Na si ndoa tu hata kuniambia chochote kwamba ananipenda au nini. Nikijiangalia mwenyewe sijoni kama nina kasoro sasa hii hali mpaka lini. Msinione ninacheka mkadhani vipi mwenzenu inaniuma kwelikweli sina hata raha na maisha” Kila mmoja wetu akabaki ameduwaa.

Wa mwisho alikiwa Dick Mbalanga. “ Mwenzenu mimi nasumbuliwa na mke wangu, siyo siri kwa kweli atanishinda. Huu sasa nikihama utakuwa mtaa wa tisa ndani ya mwaka mmoja. Mtaa wa kwanza alimpiga baba mwenye nyumba. Mtaa wa pili alifumaniwa na mume wa jirani yetu. Mtaa wa tatu alikutwa anafukia hirizi mlangoni kwa mwenye nyumba. Mtaa wanne nikiwa safari alikamata bata wa watu akamkaanga wakati mimi niliposafiri nilimwachia hela kibao za matumizi. Mtaa wa tano amekula hela za watu za upatu. Mtaa wa sita kamchoma kisu binti mmoja jirani, kisa, anamshuku kuwa mimi ninatembea nae. Mtaa wa saba aligombana na mama mwenye nyumba akachukua mafuta na kiberiti kutaka kuchoma nyumba. Mtaa wa nane ilibidi nihame maana alikuwa anatembea na mpemba mmoja ayelikuwa na duka lake nyumba hiyohiyo. Sasa juzi mke wangu kagombana na wapangaji wenzie akawatishia maisha na wenzake wamemwambia watamfanyizia…….mkumbuke huko kote hatukukaa tukamaliza mwaka, tulikuwa tunahama tunasamehe kodi miezi iliyobaki.”

Yule jamaa aliyetuhoji akatuangalia kingano za kivulnsha akasema “….mnaona ndugu zangu, kipindi mnaongea mliyajua haya ?; kazi kwenu mimi siyawezi labda kivuli kitawasaidia. Akaondoka na kutuacha midomo wazi kivulini.

No comments:

Post a Comment