ZIARA YA MHESHIMIWA
Wiki jana tulitebelewa na Mh. Mbunge wetu. Pamoja na kuwa kivulini kwetu sio uwanja wa siasa lakini kwa mujibu wa Katiba ya nchi hatuna mamlaka ya kuwapiga marufuku wanasiasa kuja kivulini na kufanya walitakalo ili mradi hawavunji sheria.
Baada ya Mh. Mbunge kujitambulisha kwetu tulilazimika kumsikiliza ujumbe wake. Naye kwa kujiamini kabisa akasema:
" Ndugu wapigakura wangu, waheshimiwa wananchi; nimepata malalamiko yenu ya kwamba tangu mnichague sijawahi kuja japo kuwapa shukrani kiasi kwamba mpaka uchaguzi mwingine unakuja baadhi yenu hata sura yangu mmeisahau. Kwa hilo sikatai. Kama mjuavyo; jimbo langu lina vivuli vingi sana kiasi nimeomba katika Bunge la mwaka huu jimbo ligawanywe mara mbili ili niweze angalau kwa kutembelea kivuli kimoja kila siku nimudu kumaliza vivuli vyote katika msimu mmoja wa uongozi wangu. Vinginevyo katika Bunge hili la Katiba mpya nipendekeze kipindi kimoja cha ubunge kiwe ni kwa miaka kumi."
"Jambo jingine ambalo ningeliomba mnielewe ni kuwa na mimi ni MwanaUkawa. Kimahesabu kwa kuwa mimi ni mbunge wenu 'automatically' na nyinyi wapiga kura wangu wote ni WanaUkawa. Nadhani tunakubaliana na msemo wa "ukipenda boga basi penda na maua yake". Kusema hivyo ina maana sisi wa jimbo hili serikali zetu ni tatu; kwa hilo sina wasiwasi na nyinyi wananchi wangu na msikubali kuyumbishwa na wanasiasa uchwara na vijisera vyao vya majitaka."
"Kitu kingine ni kuwa nilitaka niwadokeze kidogo tu kuwa ninatarajia kuwania Urais wa nchi lakini kutokana na taratibu za chama chetu hiyo tuiache kwanza iwe ni siri yenu msimwambie mtu; lakini kama alivyosema Kikwete akili za kuambiwa basi changanyeni na zenu mtajua pumba ni zipi na mchele ni upi"
La mwisho, nilikuwa nimewaandalia kajilunch kadogo kwenye ukumbi wetu wa Kivulini. Nendeni mkale mshibe bila ya wasiwasi kwani usafiri upo; kuna kijinauli kwa kila mtu, Mtendaji atawapa bahasha zenu."
"Kwa kuwa muda umebana sana kwa leo taarifa ya utekelezaji wa sera ya kivulini na ya maendeleo sitaitoa; tuombe mungu kura zitoshe katika uchaguzi mkuu ujao kwenye kikao kama hiki tutaelezana nini kimefanyika katika vipindi vyote sita vya ubunge wangu. Tanzanyika oyee "
Kabla hatujamhoji chochote akapeana mikono na aliokuja nao aatuacha tumeduwaa kivulini, akidai amasubiriwa na vivuli vingine.
No comments:
Post a Comment