WATOTO WA MITAANI NA WALALA MATANGA
Kwenu Waheshimiwa sana Wana Ustawi wa jamii,
Jamii ya Kivulini kwetu imelazimika kutuma barua hii pepe ipeperuke hadi ije kuwapepea enyi waheshimiwa sana ambao kwa hakika tunawategemea.
Madhumuni ya waraka huu ni kuwazindua mkumbuke shuka kabla usingizi haujawakolea na pia kabla ya usiku wa manane ili msijekumbuka shuka wakati kumekucha.
Mara tu baada ya kupokea waraka huu ebu kwa mchana pitieni kwenye makutano yote ya barabara muone jinsi ustawi unavyomomonyoka na kuzorota. Mtajionea jinsi ambavyo wananchi wa kila rika walivyogeuza makutano ya barabara na bustani za miji kuwa makazi rasmi na ya kudumu. Wameweka majiko ya kupikia, fenicha za kukalia na kulalia. Wanafua, wanapika, wanapiga soga na mengine mengi ya kinyumbani yanaendelea.
Baada ya hapo ebu nyakati za usiku piteni mitaa ya masoko muone jinsi ambavyo watu wamelala kuanzia mwanzo wa mitaa hadi inakoishia utadhani kuna misiba iliyounganika mtaa mmoja hadi mwingine.
Yawezekana waheshimiwa mmebanwa na kazi za kuingiza data maofisini; lakini ebu fanyeni mtoke ofisini muende kwenye kwenye viwanja ili mpate kuona jinsi jamii inavyopoteza mwelekeo. Kitendo cha watu milioni kulala nje lazima kuna namna mahali hapajakaa vizuri. Nina uhakika Waziri wa Makazi na Nyumba hajachacha kiasi hicho na wala hajui kuna watu wengi kiasi hicho wanalala nje.
Vinginevyo tuvunje Wizara ya Ustawi tuunde kitu kingine kitakachosaidia kustawisha jamii maana hali kwa kweli ni mbaya na inatisha. Watu wanakutwa wanakoroma barabarani mpaka saa mbili....kwao wapi ?
No comments:
Post a Comment