Tuesday, 12 August 2014

DIJITALI KIVULINI

         KERO ZA SIMU

Leo Kivulini kuliletwa mada. Mada hii ilikuwa nzito na nyeti. Mada hii ilihusu masuala ya utandawazi hususani mambo ya mitandao. Mada hii zaidi ilikuwa ni malalamiko juu ya athari ya kizazi hiki cha "Digital" kwamba kama ni kuugua basi gonjwa hili la mtandao linazidi gonjwa la ukimwi; wengine wakadiriki kupendekeza kuwa litangazwe kuwa ni janga la kitaifa.

Wadau walilalamka kuwa suala la simu limekuwa ni kero badala la kuwa heri. Kutokana na wazungu kutuelewa vizuri vipaji vyetu vya kuwasiliana wametumwagia masimu kama vile mchanga wa bahari. Sasa hivi wasio na simu wamekuwa wachache kushinda wasio na macho. Bei ya simu imekuwa karibu na bure hivyo kumkuta mtu ana simu zaidi ya tatu zake mwenyewe wala sio ajabu.

Kana kwamba hiyo haitoshi; makampuni ya simu yameweka fulsa kibao. Kuna maeksitrimu, ma minikabangi, kabangi,  Burudika, Cheka zogo, shangwe, nipige tafu, mpaka kuna yatosha na mengine kemkem. Sasa kazi iko katika matumizi. Utakuta watu wamejiunga wanaongea kwa zaidi ya masaa manne. Fikiria mtu wa aina hiyo kwa kipindi chote anachoongea ni mambo mangapi yanalala. Sasa hivi mwanafunzi yuko darasani ana simu anadai anachati. Basi mwalimu atafundisha mpaka atakoma kumbe wenzake hawana habari na yeye wanawasiliana na mashoga zao wa dunuani.

Ngoma nyingine iko kwa akina mama. Mboga zinaungua, watoto wanashinda njaa; kisa mama anafanya fesibuku.

Ukienda maofisini ndiyo balaa zaidi maana tangu meneja mpaka mhuhumu wote wanagugo. Huhudumiwi wala husikilizwi mpaka wenyewe waishiwe na vifurushi kwenye simu ndipo wasituke kuwa upo na una shida.

Sasa kwa hali hiyo piga hesabu ni wangapi kwa saa na katika nchi wanafanya hivyo na uchumi ama maendeleo ya nchi yaaathirika vipi; hayo ndiyo yaliyokuwa yakijadiliwa Kivulini.

Mada hii ilikuwa ndefu na maongezi yake yalikuwa moto sana kiasi kivulini palikuwa hapakaliki. Ili wasikilizaji wangu muweze kupata picha kamili nitawatumia mjadala mzima kutumia intagramu na twita ili nanyi mtoe maoni yenu ama hata kulaiki tu itatosha.

No comments:

Post a Comment