Friday, 15 August 2014

KWANI KUVAA KUNA KAZI ?



           BONANZA KIVULINI

Jana Kivulini kulikuwa na Bonanza. Wenyewe wanasema hilo Bonanza ni tamasha la aina yake ambalo hujumuisha burudani na michezo ya aina mbalimbali. Kama mjuavyo hayo ni moja ya marupurupu ya  kuwa na amani nchini. Watafiti wanadai kuwa huwezi kukuta mabonanza  kwa Waparestina na wengine ambao kila uchao huna uhakika kama kesho utakuwepo.



Tamasha hilo kwa kweli lilifana sana. Vijana waliitikia vilivyo wakacheza, wakala mpaka wakanywa.

Kilichoninikwaza mimi,na pengine na wenzangu wengi ni matumizi mabaya ya bonanza hilo, hasa kwa upande wa vijana. Nilishangazwa sana kuona namna walivyokuja kivulini bila ya kujistiri maungo yao; hususani akina dada. Wengi walikuja wamevaa vipande vya nguo na kuacha sehemu muhimu za maungo yao bila ya kufunikwa.Mungu bariki kumbe vijana wa siku hizi si wakware wala wabakaji.  Labda unaweza kusema nguo za michezo ndivyo zilivyo. Lakini si hivyo. Mimi jezi nazijua. Zile hazikuwa jezi bali ni nguo zao za nyumbani. Sikuweza kuelewa vizuri kama hivyo walivyokuja kivulini ndivyo walivyotoka majumbani kwao ama la. Lakini kubwa ni swali ambalo nilijiuliza mpaka leo sijapata jibu kuwa akina dada hawa kutujia vile walikuwa wanataka tuelewe vipi ama walikusudia kutuonyesha nini ? Ninachelea kusema hata vipande hivyo walivyovaa walikuwa wakiogopa Dola; vinginevyo wanavyoonekana wangelikuja kama walivyozaliwa kwani walikuwa wamebakiza padogo sana.



Na akina kaka nao sikuwaelewa. Wengi walivalia sarawali zao nusu ya vikalio na kuacha ngua zao za ndani zikionekana. Kana kwamba hilo halitoshi wengi walikuwa wametengeneza nywele na kuvaa vidani kiasi kwamba ilikuwa wakati mwingine vigumu kumtofautisha mtu na dada yake. Hawa nao walikuwa na ajenda gani kutufanyia vile ?



Yawezekana mwanakivuli mimi nimepitwa na wakati. Na iwe hivyo; ila kusema kweli vijana hawa ni wazi nao wamepitiwa na wakati; wakati unawaburuta mzobemzobe kuwapeleka ambako wala hawakujui. Hivi kwa utaratibu huo wa kuparaganya maumbile, si tunazikonyeza Sodoma na Gomora nyingine ?

Wazazi wapendwa, waalimu, wanazuoni, na viongozi wa dini ebu saidieni kizazi hiki; sijui kama wanaharakati na hili mnahusika au nyinyi ni katika siasa, katiba na sera za serikali. Tusaidiane katika kazi hii nzito.

Kwa ushahidi zaidi nawaalikeni wote mje katika Bonanza kivulini tarehe kama ya jana kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa moja usiku katika viwanja vyetu vilevile mje mjionee vimbwanga vya dijitali.

No comments:

Post a Comment