URASIMU WA BENKI
Katika Ziara ya jopo la Kivulini kwetu, kitu cha kwanza
kupambana nacho kilikuwa ni kero ya urasimu wa Banki. Ilikuwa ni kero ya kwanza
kwa sababu kabla ya yote kikundi hiki kililazimika kupata fedha kwa
ajili ya safari ambayo walikuwa wamekusudia kuifanya.
Jamaa hawa walipokwenda Benki walishangaa sana walipopambana
na mambo ambayo hawakutarajia kuyakuta yakitendeka katika karne hii ya
utandawazi iliyojaa wasomi na watu waliokaramka.
Kipindi walichokwenda benki kilikuwa ni kipindi cha mwisho
wa mwezi na benki waliyokwenda ni miongoni mwa benki maarufu ambazo wafanyakazi
hupitishia mishahara yao huko.
Katika tawi walilokwenda kulikuwa na takribani madirisha
nane ya kutolea huduma za kuweka na kutoa fedha. Lakini kitu cha kushangaza ni
kuwa madirisha yaliyokuwa yakitoa huduma yalikuwa ni mawili tu na mengine sita
yalikuwa hayana wahudumu. Matokeo ya hali ile ni kuwa kulikuwa na msururu
mrefu ambao ulikuwa umezunguka kujaa ndani ya benki na hadi kutoka nje. Huko
nje ulipandana na msururu uliokuwa ukisubiri kutoa pesa kwa kutumia mashine za
ATM.
Utaratibu huu mbovu wa kuweka wahudumu wachache kipindi
ambacho kuna wateja wengi kilikuwa ni
usumbufu na udharirishaji wa hali ya juu
kwa wateja. Ili kupata fedha mtu ilimlazimu kusota kwa takribani masaa matatu
kwani hata hao watoa huduma wawili
walikuwa wakifanya kazi hiyo kwa taratibu kana kwamba hawaoni umati uliokuwepo.
Katika hali hii wapo walioamua kwenda zao na fedha zao na
wengine kuondoka na shida zao kwani kwa hakika utaratibu huu ulikuwa unachosha
na kukera.
Kitu cha kujiuliza ni kuwa hivi ni kweli benki hizi
zinakotupeleka ndiko tunakotaka ? Katika kipindi hiki cha ushindani wa huduma
bado wao hawaoni umuhimu wa kubadilika ? Ama wanatulazimisha tulipane hata
mishahara kwa kupitia M-Pesa, Tigo Pesa n.k.; kwa sababu haina maana wala
haiingii akilini kwa karne hii kutumia hata nusu saa tu kupata huduma ya benki
katika msongamano huu wa teknolojia na weledi. Na kwanini mtu fedha yake imtese
kiasi hicho. Wakati mwingine wengine wana dharura, wagonjwa ama wanazo ratiba
zao.
Tunaomba sana na tunawasihi ndugu zetu wa Benki kama
wanatusikia waachane na urasimu huu ambao umepitwa na wakati kabisa. Kama
wanadhani hawawahitaji wateja basi watoe matangazo wasitumie usemi wa
AKUFUKUZAYE HAKWAMBII TOKA.
No comments:
Post a Comment