Wednesday, 3 September 2014



           FACEBOOK

Leo Kivulini kwetu tulikuwa na mjadala kuhusu mitandao hususani mtandao wa Facebook. Tulikuwa tukijaribu kufanya tathmini  ili kuona ni kwa kiasi gani mitandao hii inatusaidia hasa sisi wa nchi zinazoendelea.



Kwanza tulipitia akaunti nyingi na kukuta idadi kubwa ya akaunti hizo zina walakini. Kulikuwa na akaunti nyingi sana ambazo hazikuwa na majina ya kweli. Kulikuwa na akaunti nyingi ambazo hazikuwa na picha za kweli za wahusika. Kulikuwa na akaunti nyingi ambazo badala ya picha za watu kulikuwa na picha za maboksi, miti, bendera, wanyama, maua n.k. Kulikuwa na baadhi ya akaunti zilikuwa na jina moja lakini picha ni ya kikundi na hivyo kuwa vigumu kumjua mwenye jina  husika ni nani. Lakini zipo akaunti ambazo zilikuwa ni za halali kwa kila hali.



Utafiti huo kwanza ulituthihirishia kuwa pindi akaunti hizo zilikuwa ni za mizengwe, hata mawazo na uchangiaji wake katika facebook wa hao waongo pia ulikuwa ni wa bandia.  Mengi yaliyokuwa yakielezwa hayakuwa mawazo halisi au mitizamo thabiti. Uchangiaji mwingi ni wa kufuata mkumbo, kijipendekeza, ushabiki njaa, na kejeli.



Kivulini kwetu hatukuwa na nia ya kuingilia uhuru wa mtu wala kukinzana na maboresho ya utandawazi bali tulikuwa tukitaka kujithibitishia kuwa fulsa hii ya mitandao ya jamii imetusaidiaje kwa mtu mmoja mmoja. Ili kupata picha ya nini kipo katika facebook na faida zake nitatoa mifano midogo mitatu.

1. Kuna siku mtu aliweka picha ya jeneza kwenye ukurasa wake. Watu zaidi ya mia tano wali like. Sijaelewa wali like kwa sababu ya urafiki na aliyeliweka ama wali like kwa kulipenda sana jeneza ama vipi. Lakini iwe iwavyo bila ya hata mmoja wapo kutoa maoni yoyote inatia shaka.

2. Inatokea dada anaweka picha yake. Baada ya sekunde kunamiminika like, sifa, na kashfa kibao mpaka wakati mwingine anaamua kuiondoa.

3. Anatokea mtu anaandika neno moja tu NAOMBA; zaidi ya watu elfu watachangia kwa sentesi mojamoja au neno mojamoja. Baada ya mjadala kwisha ndiyo hadithi imekwisha.

Sasa unaweza kukuta mtu kashinda ana facebook lakini hajapata rafiki, hajapata mchumba, hajafanya biashara, hajaongeza japo elimu kidogo ya chochote, hajatoa mawazo wala kuelimisha chochote lakini bando limekwenda, muda umekwenda, macho yameingia giza na vidole vimewasha. Sasa huu mtandao unakuwa umekuweka wapi katika ulimwengu wa sasa.



Hii ni mada inayotugusa wengi sana, na lazima tukasirike kidogo; lakini ukweli unabaki palepale kuwa hatuitumii vizuri hii mitandao. Wenzetu wanauza, wananunua, wanaelimika, wanaelimisha, wanatafuta na wanapata watakavyo kupitia mitandao. Ndugu zangu tusikubali siku ipite hujajifunza au kupata chochote cha nyongeza kutoka katika mtandao.




No comments:

Post a Comment