Saturday, 30 August 2014

WAHAMIAJI HARAMU

  HAPA KWETU FULL KIYOYOZI


Kivulini kwetu tunataka daima mambo yawe mazuri kama ilivyo hapo juu na si vinginevyo kama inavyoonekana hapa chini.


Kwa taarifa tu, hii ninaitoa kama tahadhari kuwa nyie mawakala wa wahamiaji; mchezo wenu ndiyo mauti kwetu.

Habari tulizonazo ni kuwa Kivulini kwetu wahamiaji haramu wamekuwa wengi kupita kiasi . Hatuna uhakika kama watu wa Uhamiaji wanalijua hili kwa mapana yake ama la, lakini iwe iwavyo, mambo yakiharibika wote tutaingia katika matatizo.


Sasa hivi wahamiaji kutoka nchi jirani na za mbali wamekuwa wakipishana mitaani mpaka wenyewe kwa wenyewe wanaanza kukimbiana; lakini sisi wenyeji wala hatuna wasiwasi; tupo tu tunawagawia huduma zote watakazo. Wapo wengi tu wanaouza matunda kwa baiskeli; wapo wanaouza maua na mapazia; wapowanaojifanya makandarasi; wapo wanaojifanya madaktari; wauza vikombe; wasuka nywele; wasanii; wajasiliamali; na wa aina kadha wa kadha. Sasa hivi kila mgeni anatusifia hapa kwetu kwamba KIVULINI KWETU NI FULL KIYOYOZI. Kwamba hapa shida ni kuingia, lakini ukifika ni kama umeingia peponi; hakuna bugudha.

Kitendawili ninachokiona ni kuwa wageni hawa huja mikono mitupu tena kupitia njia za panya, lakini baada ya kipindi kifupi hustawi kushinda hata wenyeji; na ustawi wao huupata kwa kutumia fulsa hizihizi ambazo wakati mwingine wageni tumeshindwa kuzipata. Ni vipi wanafanikisha mambo yao, hilo nalo neno. Anakuja mhamiaji haramu baada ya miezi miwili anapanda cheo anakuwa mwekezaji.



Kwa sasa sio tatizo sana, lakini baada ya muda watazaliana, watanunua ardhi kwa maekali, wataoa shangazi zetu, na wakiwa wengi wanaanzisha kashkash za kwao hapa Kivulini kwetu, kipindi hicho tumejisahau hata madaraka mengine tumewakabidhi. Mbona sisi kwao hatufanyi hivyo na wala hawatuachii tukajimwaga kama sisi tunavyowaachia. Huu wema kuzidi uwezo tumeutoa wapi.

Nimelazimika kusema msije mkasema sikuwaambia.


UBINAADAMU KAZI

KWANI SALAMU KILO BEI GANI ?




 Kwenu msiopenda kusalimia na kusalimiwa,

Kuvulini kwetu wamenituma niwaambie ama niwapashe mpashike kuwa tabia hii mliyonayo ni chafu na inatia kichefuchefu. Tabia yenyewe ni ya kuwa wazito katika salamu. Kwanza hamna utaratibu wa kusalimia watu na mbaya zaidi hata mkisalimiwa hampokei salamu na kama mnapokea basi ni kama mnalazimishwa. Kwani hamjui kuwa salamu ndiyo kipimo cha awali cha ustaarabu wa mtu ? Basi habari ndiyo hiyo.

Watu wa kivulini kwetu wamewachokeni kwa tabia hiyo ya ovyo. Ikiwa hata mbwa, kuku, nyani na wengineo wakikutana wanasalimiana sembuse wewe mwanadamu usiyekuwa na mkia. Kumbe ubinaadamu wako umekalia wapi; miguuni kiunoni ama kichwani ? Kwa kweli mnaudhi.

Nalisema hil ili liwatue vizuri vichwani mwenu. Ebu tuelezeni, tabia hiyo ni kwa vile mna pesa sana, ama ni kwa vile mmesoma sana ama ni kwa ajili gani. Na mseme pia kama mkiwasalimia watu ama mkiitikia salamu za watu mtapungukiwa nini. Na kama mnajua bei ya salamu huko mnunuako tuelezeni salamu kwa kilo mnauziwa bei gani ? Mbona sisi tunajua salamu hazina gharama.

Utawakuta watu hawana cha pesa, hawana cha elimu, hawana sura nzuri; kwanza miguu yao yote ni ya kushoto lakini mabahili kwa salamu kushinda hata nyoka. Nini hasa kinawasumbua ? Mmelogwa ?

Wenyewe ukiwabana utasikia wanasema kwani salamu ni lazima; kwa taarifa yetu ili mradi nyinyi ni binadamu na tuko nanyi katika jamii hii, salamu ni lazima. Ni lazima kwa sababu hatima yako wewe ni kifo na siku ukifa hatutakuacha barabarani utuozee utunukie; tutalazimika sisi kubana pua zetu kukuzoazoa na kwenda japo kukutupa jalalani; sasa sisi utatulipa nini na kipindi hicho kujitambui. Maiti hazikwi na pesa, hazikwi na vyeti, wala hazikwi madaraka, anazikwa mtupu kama alivyozaliwa; sasa mnalinga nini nyie.

 Jambo jingine ni kuwa wewe ni binadamu eti siyo tumbili; na binadamu kama walivyo viumbe wengine tuna taratibu zetu ambazo ni lazima zifuatwe ili tukukubali katika jamii; vinginevyo hamia msituni ukaishi na mafisi wenzio utuache sisi tusalimiane; kwanza hutulishi, hutuvishi na wala wewe sio barabara kusema tutapita wapi.

Ninaongea hivi kwa hasira kutokana na kukerwa. Mtu anakuja msibani anawakuta watu wamejaa, hana salamu hana cha nini anakaa kwenye kiti na kuendelea kubonyezabonyesa kasimu kake ka mchina; hata kuwashika mikono wafiwa anaona tabu; kumbe kilichomleta pale kitu gani. Ama mtu anaingia katika ofisi ya watu hasalimii wala haulizi getini; ili mradi alikwishaongea na mwenyeji wake kuwa atakuja basi. Ama jirani yenu kila siku akiingia au akitoka hasalimii majirani. Hawa ndio wanaosababisha majirani wanafungulia muziki mpaka sauti ya mwisho siku wanaumwa ama wamefiwa katika vyumba vyao.

Hii ni mara yangu ya mwisho kuwakumbusha nyinyi takataka msiojua maana na umuhimu wa salamu; kwamba kuwakumbusha huku si kutaka chochote kutoka kwenu bali ni kuwafahamisha kuwa ubinaadamu kazi hivyo lazima muwajibike kama binaadamu hata kama mlilelewa ndivyo sivyo; salimieni na pokeeni salamu; vinginevyo nendeni mkaishi na majongoo vichakani; mtuondolee kiwingu.

Thursday, 28 August 2014

MTAANI KWETU



        VALANGATI KIVULINI

Ndugu zangu leo Kivulini kwetu kumetokea valangati la kufa mtu.



Majira kama ya saa tano asubuhi maeneo ya mtaa wa madukani niliukuta umati wa watu wakishuhudia patashika nguo kuchanika baina ya akinamama wawili. Vurugu iliyokuwapo pale ilikuwa si ya kuzimwa na wapita njia. Mungu ashukuliwe baada ya msukosuko mkubwa kwa bahati wakapita askari wa Tigo na pikipiki lao ndio waliofanikiwa kumaliza kasheshe ile tena baada ya kulipua kabomu kadogo ka kutoa machozi.



Utulivu uliporejea nikapata fulsa ya kuongea na mmoja wa mashuhuda waliokuwepo kutoka mwanzo ili nijue chanzo cha kadhia hiyo; ndipo nilipopewa mkanda mzima.



Chanzo chetu cha habari kinasema kisa cha ugomvi huo ni mwekezaji wa ndani ambaye ana hotelibaa pale mtaani palipotokea ugomvi. Inasemekana mwekezaji huyo alikuwa amemwajiri dada mmoja kutoa huduma katika mradi huo ambaye kutokana na umahiri wake na bidii yake ya kazi akaamua kumuongeza jukumu la kumhudumia pia yeye mwekezaji binafsi.



Chanzo chetu cha habari kinaendelea kumwaga cheche kwa kusema kuwa baada ya kipindi kifupi tokea mwekezaji huyo amtunukie shahada mhudumu wake akatokea mteja mmoja wa kike ambaye naye kutokana na umaarufu wake katika ile hotelibaa ikapelekea mwekezaji kumtunukia medali ya uteja wa kutukuka na hivyo mbali ya kuwa mteja katika mradi akawa pia mteja wake binafsi.



Changanya kanganya hii iliendelea kwa kipindi cha kama mwezi mmoja hivi bila mteja bora na mhudumu mahiri kutambuana kuwa wapo katika kujenga nyumba moja. Wenyewe wakawa wanacheka na kuchangamkiana sana kiasi cha kuwa mashosti. Lakini wapo baadhi ya wateja na wahudumu katika kiwekezwa hicho ambao walikuwa wanajua kuwa urafiki huo ulikuwa ni wa mashaka; kwamba walikuwa wakila sahani  moja bila wenyewe kugusana mikono.



Kikichotokea leo ni kama ajali. Ilikuwa ni kawaida kwa mwekezaji kumpa kinoti kama kibali mteja bora kumpelekea mhudumu mahiri  ili apewe huduma aliyokuwa anaitaka na pesa atalipa atakapojisikia. Kwa bahati mbaya leo aliandika vinoti viwili; kimoja cha huduma kwa mteja na kingine cha huduma kwa mwekezaji; vikiwa katika karatasi zinazofanana. Kwa uzembe wa mteja bora alipofika kwa shosti wake akajichanganya na kutoa kinoti cha huduma binafsi ya mwekezaji ambamo ndani ya kinoti hicho kulikuwa na jina la mteja bora lililoanza na haneeilikifuatiwa na saa ya kukutana, mahali pa kukutana, nini cha kufanya na mambo mengine ambayo hayaandikiki na chini ya kinoti hicho kulitiwa saini kwa mbwembwe na mwekezaji mwenyewe.

Mhudumu mahiri baada ya kupokea kinoti hicho kwa makosa na yeye akakosea kumhoji kwa kumuuliza mteja bora ana maana gani kumpatia ujumbe ambao si wake ama ndiyo kantangaze anaianzia kwake. Mteja bila kengere kogonga kichwani kwake akahoji kuwa kama ujumbe haumuhusu maneno yote hayo yanakujaje; kwani inahuu..



Majibizano yakiwa katika hatua za awali, mara akaingia mwekezaji pale hotelibaa; kuingia kwake ikawa kama unazima moto kwa kupulizia gesi asilia. Yakaanza kurushwa maneno, jembe, matusi, vitisho, kutoka pembe hadi pembe; aliyekuwa na masikio ya chuma alisikiliza na mwenye masikio ya mbao alisalimisha masikio yake maana  matusi na kashfa zilizokuwa zikimwagwa pale zilikuwa ni mpya kutoka  dukani ambazo zilikuwa hazijawahi kutumika. Kana kwamba hiyo haitoshi vitendea kazi na bidhaa zikaanza kutumika kama silaha za mapambano na ukumbi wote wa biashara ukawa mbengelembengele; vurumai hadi barabarani. Ilibidi ili kujenga heshima mwekezaji aingie mitini na kuacha gari liende bila dereva maana mambo sasa yalikuwa si mambo.



Baada ya kupata taarifa hiyo nikabaki ninajiuliza kufanya vurugu kiasi hiki wale akina dada mashosti wakati wote ni madoezi maana yake nini na yule mwenye mali aliyeko nyumbani afanyeje ? Na huyu mwekezaji naye huu ndio kweli utaratibu wa kuwekeza; kwa kuwa na mhudumu mpaka binafsi na mteja mpaka binafsi. Kwa staili hii uchumi kivulini kwetu utaimarika kweli ?

Wednesday, 27 August 2014

BARUA PEPE KWENDA USTAWI WA JAMII

WATOTO WA MITAANI NA WALALA MATANGA

Kwenu Waheshimiwa sana Wana Ustawi wa jamii,

Jamii ya Kivulini kwetu imelazimika kutuma barua hii pepe ipeperuke hadi ije kuwapepea enyi waheshimiwa sana ambao kwa hakika tunawategemea.

Madhumuni ya waraka huu ni kuwazindua mkumbuke shuka kabla usingizi haujawakolea na pia kabla ya usiku wa manane ili msijekumbuka shuka wakati kumekucha.



Mara tu baada ya kupokea waraka huu ebu kwa mchana pitieni kwenye makutano yote ya barabara muone jinsi ustawi unavyomomonyoka na kuzorota. Mtajionea jinsi ambavyo wananchi wa kila rika walivyogeuza makutano ya barabara na bustani za miji kuwa makazi rasmi na ya kudumu. Wameweka majiko ya kupikia, fenicha za kukalia na kulalia. Wanafua, wanapika, wanapiga soga na mengine mengi ya kinyumbani yanaendelea.



Baada ya hapo ebu nyakati za usiku piteni mitaa ya masoko muone jinsi ambavyo watu wamelala kuanzia mwanzo wa mitaa hadi inakoishia utadhani kuna misiba iliyounganika mtaa mmoja hadi mwingine.

Yawezekana waheshimiwa mmebanwa na kazi za kuingiza data maofisini; lakini ebu fanyeni mtoke ofisini muende kwenye kwenye viwanja ili mpate kuona jinsi jamii inavyopoteza mwelekeo. Kitendo cha watu milioni kulala nje lazima kuna namna mahali hapajakaa vizuri. Nina uhakika Waziri wa Makazi na Nyumba hajachacha kiasi hicho na wala hajui kuna watu wengi kiasi hicho wanalala nje.


Vinginevyo tuvunje Wizara ya Ustawi tuunde kitu kingine kitakachosaidia kustawisha jamii maana hali kwa kweli ni mbaya na inatisha. Watu wanakutwa wanakoroma barabarani mpaka saa mbili....kwao wapi ?


Monday, 25 August 2014

NGANO ZA KALE

            HEKAYA ZA SUNGURA


Ipo hadithi moja ambayo wengi wetu hatuijui yote bali tunaijua kipande tu; hadithi hii ni ya Sungura mjanja na ndizi mbichi.

Inasemekana kuwa hapo zamani za kale SUNGURA mjanja alikwenda kondeni ambako kulikuwa na migomba ambayo mingi kati yake ilikuwa imebeba mikungu ya ndizi.

Siku hiyo ambayo Sungura aliingia katika shamba hilo alikuwa na njaa sana lakini kwa bahati mbaya mikungu karibu yote ilisheheni ndizi zilizokuwa mbichi japo zilikuwa zimekomaa.

Kutokana na njaa aliyokuwa nayo akaona ni heri ajaribu kufanya maarifa apate japo ndizi kadhaa chache aweze kutuliza njaa yake na ikiwezekana kiasi apelekee wanae. Kwa kutumia nguvu zilizokuwa zimebaki mwilini mwake akatikisa kila mgomba ili aweze kupata chochote; lakini bahati haikuwa yake; hakuna hata ndizi moja iliyoanguka; alichoambulia ni uchovu zaidi.

Baada ya Sungura kuona mambo yameshindikana akaamua kutoka kwa hasira huku akisema SIZITAKI.....MBICHI HIZI. Wakati akiyasema hayo Sungura hakujua kuwa hakuwa peke yake katika lile shamba; alikuwepo SHORE pia. Shore alimwonea huruma sana sungura kwa namna alivyochoka  na  kunyong'onyea kwa njaa kiasi cha kutembea kwa shida kuelekea kwao. Hakumsemesha hata neno moja akamwacha aende zake.

Baada ya siku mbili karibu shamba zima la migomba  ndizi zote ziliiva. Kwa kuwa Shore alikuwa habanduki shambani hata kama ndizi ni mbichi; kwa kuona zimeiva  akamkumbuka Sungura. Akaamua akamwite aje shamba ale kwa kadri atakavyoweza.

Kwa bahati Shore akamkuta Sungura maskani kwake akamwomba wafuatane kwenda shamba. Sungura mwanzoni alikataa katakata kuwa yeye hana haja ya ndizi kwanza ndizi zenyewe mbichi. Lakini baada ya kubembelezwa sana akaamua aongozane na Shore kwenda shambani.

Walipofika shambani Sungura hakuamini macho yake kwani ndizi zote zilikuwa zimebadilika rangi. Shore akamwambia Sungura aanze kutikisa migomba. Katika kutikisa mgomba wa kwanza tu zilidondoka ndizi ambazo kwa siku ile Sungura na familia yake hawangeweza kuzimaliza.

Akiwa mwenye furaha Sungura akamwuliza Shore kuwa amejuaje kuwa ndizi zile zilikuwa zimeiva. Shore akamwambia kuwa yeye huwa habanduki shambani hata kama ndizi mbivu zimeisha bali hukaa humo humo shambani akila matunda mengine hadi ndizi mbichi zinaiva. Hapo ndipo Sungura alipomwangalia Shore kwa mshangao na kutikisa kichwa huku akisema " ama kweli MVUMILIVU HULA MBIVU".

Saturday, 23 August 2014

KIPEPERUSHI

      UJUMBE KUTOKA KWA MFADHIRI


Leo Kivulini tumetumiwa kipeperushi chenye ujumbe mzito kutoka kwa mwekezaji. Amesema tukisome na kama kitafaa tukipeleke kwa waheshimiwa wakae nacho kama akiba kwani siku zote akiba haiozi. Japo Kivulini si uwanja wa siasa lakini ukweli ni kwamba hakuna maisha yasiyo na siasa. Tunaomba kuwasilisha kipeperushi hicho. Asanteni sana.


Friday, 22 August 2014

BLEKINGI NYUZI

      GARI LAIBIWA KIMAZINGARA



Wandugu wapenzi,

Habari tulizozipata sasa hivi ni kuwa Kivulini kwetu limeibiwa gari Lori aina ya Scania likiwa na shehena yake ya mafuta. Lori hilo liikuwa limeegeshwa katika gereji ya kivulini likisubiri kusafiri kesho kwenda nchi za nje kupeleka mafuta hayo.

Gari hili likiwa mali ya kivulini limekutwa halipo lilipoachwa jana.

Cha kushangaza kuhusiana na kutoweka kwa gari hili ni kuwa magurudumu yake yote yakiwemo na ya spea ambayo yalikuwa yamefungwa katika gari hilo yamekutwa mahali lilipokuwepo gari hilo. Imethibitika kuwa magurudumu hayo yalikuwa ya gari hilo kwa kuwa yalikuwa na alama. Kama kuna aliyechukua gari hilo, basi lazima alikuja na magurudumu yake akabadilisha. Kana kwamba hiyo haitoshi, hata ufunguo wa gari hilo umekutwa juu ya mataili hayo.

Habari zaidi za kuaminika zinasema walinzi watatu waliokuwa wakililinda lori hilo wamekutwa wazima lakini wamelala fofofo; na mpaka tunaingia mitamboni juhudi za kuwaamsha zilikuwa hazijawezekana; hivyo walikuwa bado wamelala. Na hivi tunavyosema wapo hospitali wanaendelea kulala chini ya ulinzi mkali.

Wanakivulini waliokutwa eneo hilo la tukio wanadai kuwa hii ni mara ya kwanza kwa wizi wa aina hiyo kutokea ukitilia maanani kuwa gari hilo lilikuwa ndani ya uzio na katikati ya magari mengine ambayo yalikutwa hayajasogezwa japo hatua moja; lakini nafasi lilipokuwepo gari hilo imeachwa wazi na gari halipo..

Tutaendelea kuwajuza kitakachojiri juu ya tukio hili ambalo kwa hakila si la kawaida.

MGENI NJOO MWENYEJI APONE


         MGENI KUTOKA MAJUU


Jana tumepata bahati ya kutembelewa na mgeni kutoka ng’ambo. Mgeni huyu aliwasiri kivulini kwetu akiwa na maoni kadhaa kwenye mkoba wake  kama zawadi badala ya vitu ambavyo tumevizoea kuletewa na wageni wa aina hii.




Kwanza mgeni huyu alitupongeza kwa kuunda chombo cha mawasiliano cha kisasa(blog) kwa madai kuwa angalau tunaonyesha upeo fulani wa maendeleo kwa kwenda na wakati.



Akiwa kivulini kwetu alituomba tuendeleze mawasiliano na watu wa mataifa mbalimbali kutumia blog hiyo kwani dunia ya leo ni kama kijiji; na tujitahidi kuweka mambo ya msingi badala ya kuijaza matusi na uchafu kama zilivyo blog nyingine nyingi.



Baada ya kutuasa hivyo alitupatia ujumbe toka umoja wa mabloga wa kwao kuwa sisi wa kivulini kwa faida yetu na ya vitukuu wetu tuzingatie yafuatayo:



1.      Tujitahidi kuanzia sasa kupunguza kasi ya kuzaliana; tusisubiri maji yakiwa shingoni ndipo tuweke sheria kalikali. Amedai kuwa ardhi hii tunayoiona kubwa haitakuwa hivi baada ya miaka kumi ijayo kama matumizi yenyewe yatakuwa kwa kufuja kama ilivyo sasa. Kingine kitakachotuumbua ni huduma za jamii; kwamba wao kwao pamoja na maendeleo waliyonayo  katika aina mbalibali ya huduma za majii bado kuzaa zaidi ya watoto wawili katika familia ni kama ajali; labda mama ajaliwe kujifungua mapacha watatu. Tukumbuke watoto wazaliwapo wanahitaji chakula, matibabu, nguo, elimu na mambo mengi sana hivyo kuzaa bila mpango si busara. Kila mwanakivuli atoe busati, badala yake aweke nyota ya kijani mlangoni kwake.


2.      Tupunguze siasa  tufanye kazi. Ameshangazwa sana alipowasili kivulini na kumkuta kila mwanakivuli ni mwanasiasa, mwanaharakati na mwanasheria. Alishangaa kuona kivuli duni kama chetu kina wanaharakati wengi kushinda wataalam wa fani mbalimbali.  Ameshangaa kuona tunapoteza muda mwingi sana kuongea, kushitakiana, kubishana, kulaumiana,  na kujadiliana mambo mengi sana ambayo wala hayana tija wala umuhimu; tena tunayafanya tukiwa katika makundi huku tukimwaga mapesa mengi kupata muafaka  .  Yeye alisema ipo haja ikibidi tupange siku maalum za longolongo ziwe japo siku  mbili kwa wiki na siku tano zilizobaki kusiwe na vikao, mikutano, vijiwe wala mabonanza tujikite katika kazi. Yeye amedai kuwa hakuna kokote walikopata maendeleo kwa maneno bali kwa kazi. Ametishika sana kukuta robo ya wanakivuli ndio wanaofanya kazi na robo tatu yote ni wategemezi. Tumesahau hata msemo mtakatifu usemao "ASIYEFANYA KAZI NA ASILE". 



3.      Tatu, alitusihi kuwa wazalendo. Ameshangaa kutuona watu wa kivulini pamoja na matatizo yetu hatujipendi wenyewe na baya zaidi hatupendani.  Alishangaa sana kumsikia kijana wetu mmoja tena msomi aliyesomeshwa na serikali akitamka hadharani bila kujali  kazungukwa na nani  anasema kwamba anajuta kuzaliwa kivulini;  eti ni heri angelizaliwa mbwa majuu angeliishi kwa raha sana. Anadai tamko la aina hii kule kwao mtu huyu angelipigwa risasi kwani hana faida na tena ni sumu katika jamii. Kama ni kwenye kompyuta hiki kingelikuwa kirusi hatari sana. Amedai kuwa bila ya uzalendo sera nzuri, katiba bora na mipango mizuri havitaweza kutusadia chochote. Ni lazima turingie kivuli chetu.



4.      Jambo jingine;  alitusihi watu wa kivulini tuwe waadirifu na hasa viongozi. Ameshangaa jinsi ambavyo hatushangai wala kuhoji maajabu ya kiuchumi yaliyopo kivulini. Kwamba tumeamua kutohoji chochote wala kuwianisha kazi ya mtu na kipato chake. Kwamba si ajabu tarishi wa mahakama kumiliki gari ya vogi. Haitushangazi mtoto wa kazi kuwa na jumba la kifahari kijijini kwao. Ni kitu cha kawaida waziri kumiliki ardhi ya wilaya nzima kwa ajili ya kilimo cha familia yake. Mwanafunzi kumiliki simu ya milioni na zaidi ni kawaida. Amedai kwa mwendo huu tuna kama miaka mitano tu iliyobaki maisha kivulini yasiwezekane. Kundi la walionacho limezidi kuwa dogo mno likiishi katika msongo wa maisha magumu yasiyo na matumaini hata chembe; wakati huohuo kuna kundi dogo linaloishi kama liko mbunguni; linaishi kadri linavyowaza. Amedai kuwa hii inaongeza chuki na hasira za kundi kubwa; na inavyoonekana muda si mrefu uvumlivu wa wengi utatoweka watajichukulia vyao walivyoporwa na wachache. 



5.      Mgeni huyu amewasilisha mshangao kutoka majuu kuwa kivulini mungu katujalia kwa kutupa kila kitu ambacho wenzetu wamepewa kimoja kimoja au viwili ama hawakupata kabisa. Kasema tumepewa bahari, mito, maziwa, wanyama, ardhi, madini, maajabu, na vingine vingi. Anadai bado anatafiti kuona wapi lilipo tatizo kiasi cha sisi kushindwa kuongoza kwa utajiri duniani. Amediriki hata kusema kuwa pengine mataifa kakubwa yanatufanyia chumaulete kutuibia uchumi wetu kwa mazingira ama tumepigwa kipapai au tumekanyaga mdudu. Amedai lazima rasilimali zetu zitunufaishe wenyewe kwanza sio tunagawa kama njugu ili mradi tu ziishe.



6.      Mwisho ametuonya tusichezee amani tuliyonayo. Ameshauri kila mwenye kuleta chokochoko tumpe skolashipu aende kusoma digrii ya amani Somalia, Misri, Parestina au Zaire ili  akirejea afundishe wengine. Amesema maeneo hayo kuna vyuo vizuri sana vya amani; hivyo ni vema vijana wetu tuwaendeleze katika fani hiyo pia.



Baada ya kutupa salamu hizo akatukabidhi zawadi ya msalaba mwekundu akaondoka.

Thursday, 21 August 2014

METHALI MPYA ZA LEOLEO

CHAGUA MOJA TU......NIKUUZIE

1. Ujanja wa nyani porini, mjini hata  kuvuka 
    barabara hawezi.

2. Panga lake kupangua, kupanga si la upanga

3. Maji yakijaa chupa ndiyo mwisho wa kujaza.

4. Udi haulumbani na ubani.

5. Kioo hakina ila, ila ajitezamaye

6. Mchawi usiku, mchana mganga

Friday, 15 August 2014

KWANI KUVAA KUNA KAZI ?



           BONANZA KIVULINI

Jana Kivulini kulikuwa na Bonanza. Wenyewe wanasema hilo Bonanza ni tamasha la aina yake ambalo hujumuisha burudani na michezo ya aina mbalimbali. Kama mjuavyo hayo ni moja ya marupurupu ya  kuwa na amani nchini. Watafiti wanadai kuwa huwezi kukuta mabonanza  kwa Waparestina na wengine ambao kila uchao huna uhakika kama kesho utakuwepo.



Tamasha hilo kwa kweli lilifana sana. Vijana waliitikia vilivyo wakacheza, wakala mpaka wakanywa.

Kilichoninikwaza mimi,na pengine na wenzangu wengi ni matumizi mabaya ya bonanza hilo, hasa kwa upande wa vijana. Nilishangazwa sana kuona namna walivyokuja kivulini bila ya kujistiri maungo yao; hususani akina dada. Wengi walikuja wamevaa vipande vya nguo na kuacha sehemu muhimu za maungo yao bila ya kufunikwa.Mungu bariki kumbe vijana wa siku hizi si wakware wala wabakaji.  Labda unaweza kusema nguo za michezo ndivyo zilivyo. Lakini si hivyo. Mimi jezi nazijua. Zile hazikuwa jezi bali ni nguo zao za nyumbani. Sikuweza kuelewa vizuri kama hivyo walivyokuja kivulini ndivyo walivyotoka majumbani kwao ama la. Lakini kubwa ni swali ambalo nilijiuliza mpaka leo sijapata jibu kuwa akina dada hawa kutujia vile walikuwa wanataka tuelewe vipi ama walikusudia kutuonyesha nini ? Ninachelea kusema hata vipande hivyo walivyovaa walikuwa wakiogopa Dola; vinginevyo wanavyoonekana wangelikuja kama walivyozaliwa kwani walikuwa wamebakiza padogo sana.



Na akina kaka nao sikuwaelewa. Wengi walivalia sarawali zao nusu ya vikalio na kuacha ngua zao za ndani zikionekana. Kana kwamba hilo halitoshi wengi walikuwa wametengeneza nywele na kuvaa vidani kiasi kwamba ilikuwa wakati mwingine vigumu kumtofautisha mtu na dada yake. Hawa nao walikuwa na ajenda gani kutufanyia vile ?



Yawezekana mwanakivuli mimi nimepitwa na wakati. Na iwe hivyo; ila kusema kweli vijana hawa ni wazi nao wamepitiwa na wakati; wakati unawaburuta mzobemzobe kuwapeleka ambako wala hawakujui. Hivi kwa utaratibu huo wa kuparaganya maumbile, si tunazikonyeza Sodoma na Gomora nyingine ?

Wazazi wapendwa, waalimu, wanazuoni, na viongozi wa dini ebu saidieni kizazi hiki; sijui kama wanaharakati na hili mnahusika au nyinyi ni katika siasa, katiba na sera za serikali. Tusaidiane katika kazi hii nzito.

Kwa ushahidi zaidi nawaalikeni wote mje katika Bonanza kivulini tarehe kama ya jana kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa moja usiku katika viwanja vyetu vilevile mje mjionee vimbwanga vya dijitali.