Wednesday, 18 March 2015

TUPIMIANE VIWANJA KILA MTU AFE NA CHAKE

Kama ilivyo ada Kivulini kwetu huwa hatukosi kero. Kero hizi huwa hatuzitafuti bali huwa zinatukumba kutokana na mazingira yenyewe yalivyo; mambo ya utandawazi, mambo ya tabia nchi, hali ya miundombinu na wakati mwingine ukosefu tu wa mirejeshonyuma  juu ya masuala kadhaa ambayo tunadhani ni ya muhimu katika jamii yetu.

Safari hii tunaomba tuliweke wazi suala la viwanja ama ardhi katika ujumla wake. Tunaliweka wazi kwa sababu limeshakuwa tatizo na siku hadi siku linaendelea kukua kiasi kwamba limekuwa likisababisha majerudi na vifo kama ajali za barabarani.


Suala la ardhi halikutakiwa lifikie hapo kama kwa kweli nia ingelikuwepo ya kuondokana na adha hii. Inaelekea watu hawajali na pengine na serikali nayo imechukulia rahisi suala hili. Tunasema hivi kutokana na ukweli kwamba kuna migogoro mingine ingeliweza kutatuliwa bila hata ya gharama zozote zaidi ya maamuzi tu ya kuelekeza hawa waishi kule na wale waishi huku. Kwamba kutokana na maelekezo tu yasiyoeleweka kumetokea ugomvi katika baadhi ya maeneo kiasi cha kusababisha hasara za mali na upotevu wa viungo na maisha. Wakati mwingine tunafika mbali kwa kuwaza kuwa huenda ulegevu huu katika masuala ya ardhi wapo watu wananufaika ya migogoro hiyo.

Katika tatizo hili la ardhi kumekuwepo na maeneo ambayo wakati wa sehemu hizo kwa miaka nenda rudi wamepokonywa na maeneo hayo kugawiwa wengine  kama wawekezaji na wakati mwingine si wawekezaji kitu. Unakuta ardhi ya kijiji kizima kinagawiwa mtu mmoja na kwa bahati mbaya sana mtu huyu kwa miaka kadhaa anakuwa hafanyi chochote katika eneo hili zaidi ya kuweka walinzi kuhakikisha mtu haingii eneo hilo. Usumbufu kwa wengi kwa ajili ya fahari ya mtu mmoja; taifa halifaidiki na jamii haifaidiki.


Yapo maeneo ambayo wananchi wamenyang'anywa bila ya majadiliano wala makubaliano. Wakihoji najibu yanakuwa ardhi ni mali ya serikali hivyo chochote kinaweza kufanyika. Lakini ni kweli haki kumpokonya ardhi mkazi wa siku nyingi na kuigawa ardhi hiyo bila ya kumweleza utaratibu utakuwaje baada  hapo ? Huyu au hawa walishajenga nyumba zao, walishapanda mimea yao ya kudumu, walishajipangia maisha yao hapo. Wakitoka hapo waende wakavamie wapi ili maisha yaendelee; huko ambako tafrani kama hii iliyowakumba haitawakumba ? Wakati mwingine jinsi wanavyoondolewa katika maeneo yao nyumba huchomwa moto au kubomolewa.


Kuna maeneo wananchi wanavamiana. Wafugaji wanawavamia wakulima. Wakulima wanafyeka mashamba maeneo ya wafugaji. Hakuna mipaka, hakuna utaratibu, hakuna sheria ila ni kila mtu na ubavu wake; mwisho wa siku eneo linakuwa halilimiki wala halifugiki; kila siku vilio.



Wote tunajua kuwa Watanzania wa leo wanalenga kila mtu kuwa na makazi yake. Miji inapanuka; Dar es salaam inakutana na Kibaha n.k. Watu wanauziana mashamba, mashamba yanakuwa makazi. Lakini viwanja havipimwi, ujenzi unaendelea holela; hakuna maeneo ya wazi, hakuna barabara, hakuna huduma; kila mtu kwa uwezo wake. Mjini humo kuna wanaofuga nguruwe, ng'ombe na mbuzi. Mjini humo kuna wenye viwanda vya kuranda mbao, kusindika mafuta, kusaga viungo vya pilau na viwanda vya gongo. Mjini humo humo kuna kumbi za kukesha za disko, kuna bar jirani na shule, misikiti mkabala na makanisa n.k Haya mambo yamejengwa holela; hayafungamani, hayatangamani na mpangilio wake tu ni kero.


Ukija uswazi huku ndiko maisha magumu. Choo mlangoni kwa jirani. Gari unaliacha mtaa wa pili, barabara haipo zaidi ya uchochoro. Ukitokea msiba hakuna mahali pa kupitisha jeneza, inabidi mwili ubebwe hadi mtaa wa pili ndipo upambwe. Watoto hawana pa kucheza, na ukitokea moto mtaa huo kunakuwa hakuna jinsi zaidi ya kuupigia makofi moto uteketeze nyumba salama.

Maisha kuhusiana na viwanja ama ardhi kwa ujumla ni kero. Tusichokielewa Kivulini kwetu ni kwanini iwe hivyo. Inakuwa hivyo kwa faida ya nani. Na itakuwa hivyo hadi lini.

Kinachojitokeza ni kutokuwepo na mipango mahususi ya upimaji wa viwanja, ugawaji wa viwanja na urasimu mwingi katika kutoa hati za viwanja; kwa ujumla suala la viwanja na ardhi limejaa urasimu kiasi kwamba kwa mtu wa kawaida linatia kizunguzungu.


Kivulini kwetu tunauliza, ni kwanini kama wizara inaona suala hili limewazidi kimo shughuli hii ya upimaji wasiibinafsishe. Tunaziuliza mamlaka zenye wakazi wenye shughuli zinazokinzana kama vile wafugaji na wakulima kwanini wasitengewe maeneo kwa uwazi na uhakika ili kila mtu ajue mipaka yake ili kuondokana na  hali hii ya sasa na kutumishiana misuri.

Na hawa wawekezaji mwitu wanaopewa ardhi maekali kwa maekali tena yenye rutuba lakini hawayafanyii chochote kwa miaka nenda rudi na kuwaacha wakazi katika maeneo makame wanaachiwa kuendelea kumiliki maeneo hayo ?


Kivulini kwetu tunashauri serikali itupimie kila mtu na eneo lake, apewe hati yake aishi kwa amani. Ipime na igawe maeneo kwa kila kijiji ili kijue mipaka yake. Wakulima waelekezwe maeneo yao, wafugaji weaonyeshwe maeneo yao. TUPIMIANE VIWANJA NA ARDHI YETU KILA MMOJA AFE NA CHAKE.

No comments:

Post a Comment