KURA NA MAFURIKO WAPI NA WAPI ?
Leo asubuhi kwenye daladala tukitokea Kivulini kwetu kuja mjini tulimsikia abiria mmoja akilalamikia lile agizo la watu wa mabondeni kuhama kutokana na kuwepo uwezekano mkubwa wa kukubwa na mafuriko kufuatia mvua kubwa zinazotarajia kunyesha muda wowote kuanzia sasa.
Jamaa huyu alikuwa akililalamikia lile tamko la kwamba safari hii atakayekaidi kuhama yakimkuta mafuriko hakutakuwa na msaada kama inavyokuwa miaka yote. Yeye alikuwa anasema kuhama hatahama na kwamba hayo mafuriko na yaje; ila anaisubiri kama ni hiyo serikali imnyime misaada kama ambavyo huwa wanapata miaka yote. Atakachofanya yeye ni kuhakikisha kuwa hapigii kura rasimu ya katiba iliyopendekezwa na hata uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani hatoshiriki. Huyu ndugu alikuwa anazungumza kwa hisia na hakuwa anatania.
Alipoulizwa ni kwanini hataki kuhama, yeye akasema katiba ya nchi inamruhusu yeye kama raia wengine kuishi popote anapotaka ili mradi havunji sheria. Na akaendelea kudai kuwa badala ya serikali kumboreshea makazi yake mahali alipo hapo bondeni inamhamisha kumpeleka ugenini huko Mabwepande wakati babu yake, baba yake na yeye mwenyewe wamezaliwa mjini Jangwani.
Alipoulizwa endapo mafuriko yatakuja na kumchukua akafa hiyo kura ya maoni na ya wabunge ataipigia wapi; akajibu kuwa kama kufa angeshakufa siku nyingi lakini amesalimika mafuriko yote tangu enzi leo afe kwa misingi ipi; kwa sababu serikali imesema ?
Huyu ni mmoja kati ya wakazi wengi wabishi ambao wamedhamiria kukaidi kuhama mabondeni. Kukaidi si tatizo. Tatizo ni hapo watakapoathirika na mafuriko na kuilazimisha serikali iwahudumie kwa ujeuri wao Maudhi zaidi ni ule msimamo wao wa kuwa lazima serikali iwahudumia kwa kuwa wao ni wapiga kura wa nchi hii.
Kivulini kwetu kwa hakika tumesikitishwa sana na ukaidi wa aina hii; wa mtu kufanya makusudi kuyatafuta matatizo na kulazimisha kutatuliwa matatizo kwa kisingizio cha katiba. Mtu wa aina hii hatofautiani sana na mtu anayekunywa sumu au kujinyonga kwa madai kuwa hawezi kufa na akifa basi siku zake zimefika. Watu hujiua faragha, lakini mbele za watu lazima binadamu waungwana watachukua hatua za kukuokoa, na wanapokuakoa huonyeshi kujali walichofanya kwa madai kuwa huo ulikuwa ni wajibu wao.
Hivi mpiga kura wa aina hii ni mgombea gani anayemtaka ? Lakini ajabu ni kuwa wapo wagombea wanaopenya mabondeni usiku na kuwaambia hao jamaa wapiga kura wao wasihame; kwamba wapo pamoja nao kwa lolote liwalo, na wasiwe na wasiwasi hata wakikubwa na mafuriko watahakikisha misaada kutoka serikalini inapatikana. Hizo ndiyo siasa za uchaguzi, kuomba kura juu ya maisha ya watu. Na je wapiga kura hao wakizama kabisa na kufa watawapelekea viroba vya maisha au uhai huko mochwari ili wafufuke waje kuwachagua.
Kivulini kwetu tulidhani ni wajibu wetu kuwafahamisha ndugu zetu mfahamu nini kinachoendelea. Mwaka huu ni wa uchaguzi na katika mafuriko yajayo lolote linaweza kutokea. Kama kweli tunawapenda wenzetu tuwasaidie sasa kwa angalau kuwashawishi na kuwasaidia wahame mabondeni ili tuwe nao salama hadi Oktoba mwaka huu tupate mchango wao. Isifike mahari tukawa na mashaka kuwa jeuri hii ni ya kufanya mafuriko kuwa mtaji wa kujikimu kimaisha wa kila mwaka kwa waathirika na mtaji wa kura kwa wagombea kwa kila kipindi cha uchaguzi. Lakini tujiulize wenyewe KURA NA MAFURIKO WAPI NA WAPI ?
No comments:
Post a Comment