Tuesday, 17 March 2015

BAYA MOJA HUFUTA MEMA MENGI

Leo Kivulini kwetu tulikuwa na mjadala wa kijamii juu ya tabia inayoambatana na msemo wa BAYA MOJA HUFUTA MEMA MENGI. Sambamba na kujadili tabia hiyo tukawa pia tunajiuliza ni kwa nini kwa manufaa ya jamii tusingelibadili tabia na kufuata usemi wa JEMA MOJA HUFUTA MABAYA MENGI.

Katika kuiangalia jamii yetu tumekuta tabia hii imekuwa ikimuathiri kila mmoja wetu katika maeneo na nyakati tofauti.

Utakuta mtu ni mfanyakazi katika ofisi fulani. Pengine huyu ndugu kwa miaka zaidi ya kumi ya utumishi amekuwa akifanya kazi zake vizuri kwa uaminifu na unyenyekevu.Na si hivyo tu, pengine ni mbunifu na ameliingizia shirika au kampuni mamilioni ya fedha kwa kiaka nenda rudi. Siku moja baada ya miaka 10 akatokea kufanya kosa, pengine la upotevu wa kiasi kidogo sana cha fedha ama uzembe wa kusababisha hasara ya kiasi kidogo sana cha fedha; kinachotokea ni kuwa uongozi au utawala bila kuzingatia mchango wake wa kiaka kumi watamtimua kazini na wakati mwingine kumdhalilisha mpaka kwenye vyombo vya habari; hivi ni kweli kampuni haiwezi kuheshimu mema na mazuri aliyofanya mtumishi huyu kwa kipindi chote cha utumishi wake  ? Hivi mfanyakazi bora kwa miaka mitatu mfurulizo katika kampuni anaweza kuchukuliwa sawa na mfanyakazi mwingine ambaye hajawahi kuchukua tuzo yoyote mahali pa kazi ?



Utakuta kijana kasomeshwa na familia na hatimae kapata kazi. Baada ya kuwa kazini akawa si mchoyo kwa kujitahidi kumsaidia kila ndugu atakayekuja kuomba msaada kwake. Ndugu watasaidiwa na watamsifu kutokana na wema wake. Baada ya muda kijana wao atakuwa na familia na hivyo majukumu yake kuongezeka na kubadilika. Kidogo kidogo ataanza kushindwa kutoa misaada kama awali na pengine kushindwa kabisa kuacha familia yake ili asaidie ndugu. Hapo sasa ndipo ndugu wataanza kuja juu kuwa kijana wao toka ameoa amebadilika sana. Na hawataishia hapo bali watamwita mpumbavu kwa kuwasaidia wakwe zake badala ya wazazi wake; watasema mkewe au mmewe kamroga ili asisaidie familia yake n.k Kisa wamekwenda kuomba wakakosa kupewa.



Utakuta katika chama cha siasa kuna wanachama ambao wamefanya kazi kubwa sana katika kukijenga chama; wakati mwingine walilazimika kutoa mali zao ili chama kisitetereke. Wapo waliouza utu wao na kuhatarisha maisha yao ili kuhakikisha chama kinasonga mbele. Lakini siku wanahoji chochote katika chama, viongozi bila kujali mchango wao na haki yao ya msingi katika chama watawatengenezea zengwe na kuwafukuza katika chama.



Utakuta katika Klabu ya soka mchezaji amekuwa ndiyo tegemeo. Mchezaji huyo pengine ndiye aliyechangia  kuipandisha daraja timu; ama ndiye aliyekuwa msaada mkubwa kuhakikisha timu haishuki daraja; ama ndiye mfungaji hodari kiasi cha timu kunyakua ubingwa mara kadhaa. Yeye kama binadamu anaweza kukosea ama wakati mwingine kwa kumdhania tu kuwa ameuza timu; klabu huuvunja mkataba wake ama kumfikisha mahakamani kwa sababu hii au ile na kusahau kabisa mangapi alifanya kwa  manufaa kwa klabu.



Utakuta mume au mke amekuwa mwaminifu katika ndoa kwa kipindi cha miaka chungu nzima lakini ikatokea siku akachepuka, basi hiyo kesi haitaisha na hakutakuwa na msamaha mpaka na ndoa inavunjika; kisa ni kosa la siku moja ndani ya uaminifu wa miaka hata zaidi ya ishirini.




Kivulini kwetu tuliibua mifano mingi sana ya athari za tabia hii ya kufuta wema wote kwa ubaya wa siku moja na kujiuliza hivi sisi wanajamii tabia hii itatusaidia nini; ni kwanini tumekuwa wepesi wa kusahau mema na kutoa maamuzi makali hata pale tunapohakikisha kuwa hili ni kosa la kwanza. Ni kwanini hatui wavumilivu; kwanini hatupeani ushauri nasaha; kwanini hatusameheani zaidi badala yake tunakuwa wepesi wa kuhukumiana. Kwa taarifa ya mjadala huu tuna imani wengi watakaosoma watatafakari ya kuchukua hatua.

No comments:

Post a Comment