Wednesday, 4 March 2015

 NINA MASHAKA SANA NA KUNDI HILI LA VIJANA



Jana jioni Kivulini kwetu tulikuwa na mjadala juu ya kundi la vijana. Kundi tulilokuwa tukiliongelea ni kundi la vijana wasomi na wasiosoma, wadogo kwa wakubwa lakini ambao wapowapo hawana mbele wala nyuma. Kundi hili ni la vijana waliomaliza shule au vyuo lakini hawana la kufanya na ni kundi linalojumuisha vijana  wenye afya na uwezo wa kufanya kazi. Hili ni kundi linalokula kwa kengere makwao ama kundi linalozagaa kujidonyolea mitaani na usiku kulala kwenye magofu, upenuni mwa nyumba, kando ya barabara ama kukesha wakinywa viroba, kubwia unga au kuvuta bangi waweze kupoteza mawazo.

Kivulini kwetu tulilifananisha kundi hili na nyasi kavu msimu wa kiangazi; nyasi ambazo akitokea mlevi akatupa kichungi kisichozimwa juu yake; moto utakaolipuka hapo kuuzima ni majaliwa yake mola. Kundi hili tulilifananisha ya sinia la dagaa wabichi wazima linaloelea ziwani ambapo yakitokea mawimbi wakati wowote hutakuwa na kitu katika sinia bali matone ya maji kwani wote wakakuwa wameishia ndani ya maji.

Kundi hili la vijana ni kubwa na siku hadi siku linaendelea kukua katika miji yetu. Tumekuwa na vijana wengi ambao mchana kutwa wanashinda wamejiinamia, wanawaza, kufikiri na kupanga mipango ambayo hatuijui ni ipi na kwa hakika hatujui hatma yao itakuwaje.Kundi la vijana wenye hasira na chuki kwa nchi yao. Vijana ambao wako tayari hata kumtafuna na kummeza mbaya wao endapo wataonyeshwa kwa kidole kuwa huyo ndiye anayewasababishia matatizo waliyo nayo.

Hawa ni watoto wetu, jirani zetu, shemeji zetu na kwa kila hali wanatuhusu. Kwa kuwa wanatuhusu ni wajibu wetu kujua wanaishije; kwa maana ya kuwa tujue wanakula nini na wapi, wanalala wapi na wanamudu vipi kuzipata japo hizo huduma japo ni duni. Tunapaswa tujiridhishe na uhalali wa maisha yao kabla makubwa hayajatukuta.

Kivulini kwetu tulifanya tathmini ya haraka na kubaini kuwa zipo familia nyingi ambazo baba au mama ama baba na mama wana jukumu la kulisha ndugu wasiopungua sita ambao wapo tu hapo nyumbani kwao wakiwa hawana kazi yoyote kutwa nzima zaidi ya kuangalia TV na kuwapokea wenye nyumba vifurushi warudipo nyumbani.

Tulikwenda mbali zaidi na kubaini kuwa katika hali halisi ya kipato cha Mtanzania wa kawaida, mshara wake unamtosha kula yeye na mkewe tu na pengine usiwafikishe mwisho wa mwezi. Kufika hapo tukajiuliza kama ndivyo wanafamilia hawa wanamudu vipi kuwahudumia hawa ndugu wa ziada katika familia zao; tena kwa kipato cha halali.?

Tumekuta ni wachache sana wenye vijimradi ambavyo vinawapunguzia makali kwa kipato zaidi kujazia mshahara lakini kundi kubwa tukaanza kulishuku kuwa linaendesha maisha kiaina. Linaendesha maisha kwa kukopa, kuiba, kutapeli, na kula rushwa makazini kwao na mitaani. Ikiwa mahitaji ni 700,000/= kwa mwezi na kipato ni 300,000/=; unaweza kujitahidi kuziba pengo kwa mwezi mmoja lakini kwa mwaka ni lazima uingie msituni ukasake nyoka; ukatapeli, ukakope, ama ukapokee rushwa. Na kadri majukumu yanavyoongezeka katika familia na utapeli, rushwa, wizi na ukopaji pia unaongezeka. Hii kitaifa ni hatari kuwa sana.

Mada yetu kuu haikuwa athari za kifamilia zinazoletwa na vijana hawa bali tulikuwa tukijitahidi kukuna vichwa juu ya nini tufanye ili kupunguza joto linaloletwa na vijana hawa kwa sababu mateja wamo katika kundi hili, panya rodi wamo katika kundi hili, waandamanaji wa kukodi wapo katika kundi hili, vibaka, machangudoa, wapiga debe, watoto wa mitaani, ombaomba, na wengine wengi ambao mbali na kuwa mzigo kwa jamii wamekuwa tishio la usalama na amani katika taifa letu.Hawa wako tayari kuunga mkono chochote kiwe cha halali ama hatari ili mradi wahakikishiwe kuwa watapata kitu. Kwa bahati mbaya kundi hili limekuwa likitumiwa kwa maasi zaidi ya mambo mema; kulipwa kidogo na kicha kuachwa wakiwa na majeraha ya mwilini na mioyoni.

Kivulini kwetu tunasikitishwa na kuongezeka kwa kundi hili katika nchi yenye ardhi kubwa na nzuri, nchi yenye madini mengi, nchi yenye wanyama wa kila aina, na nchi yenye amani na utulivu. Miji yetu ina kazi nyingi za kufanya na wafanyaji wengi wanazagaa lakini tumeshindwa kabisa kuunganisha kazi na wafanya kazi ili tuweze kuondoa aibu hii ili  kundi hili litusaidie  kusonga mbele kimaendeleo.

Mfano mdogo usio na gharama; tukienda mjini Dar es salaam kumejaa takataka kila mtaa, wakazi wa mitaa wanazichukia taka hizo na wanazo fedha za kuwalipa wazoaji taka; hapo hapo mjini ndiko kwenye vijana wengi wanaoshinda wakiranda bila ya kazi ya kufanya mpaka wanaishia kutapeli ama kuwachomoa watu mifukoni ili wapate pesa ya kununua chakula.

Kivulini kwetu tunajiuliza hivi wana Ustawi wa jamii wako wapi watusaidie mawazo juu ya kuwasaidia vijana wetu hawa ? Wizara husika wana mipango gani juu ya vijana hawa ? Umoja wa vijana wa kila Chama cha Siasa ni nini mchango wao kwa vijana hawa ambao ndio wapiga kura na wadau wao ? Mashirika ya Dini na madhehebu mbalimbali, zaidi ya nasaha mnawasaidia vipi vijana hawa. KUMBUKENI KUWA HAWA NDIYO NGUZO YA TAIFA; WAKIOZA HAWA NA TAIFA LITAKUWA LIMEOZA.

Mjadala huu bado haujafika mwisho. Kivulini kwetu kwa leo tutaishia hapa lakini tutaendelea nao ili tuhakikishe tumeridhishwa kuwa umeeleweka ipasavyo katika jamii yetu na hatua zinachukuliwa.

No comments:

Post a Comment