RASIMU IWE MBAYA AU NZURI KUIPIGIA KURA NI MUHIMU.
Moja ya majukumu ambayo yako mbele yatu katika Taifa letu ni kura ya maoni ya kuikubali au kuikataa rasimu ya Katiba mpya inayopendekezwa. Hili ni jukumu muhimu, nyeti na haki ya kila mwananchi mwenye sifa za kupiga kura.
Mchakato wa kuiandaa Rasimu hii umechukua muda mrefu na umegharimu kiasi kikubwa cha fedha za wananchi. Ili kuweza kupima matunda ya kazi iliyofanyika ni jambo la busara kwa wananchi kukamilisha hatua muhimu ya kuipigia kura rasimu hii ili kuweza kujua ni kipi kitaendelea baada ya hapo.
Kivulini kwetu tunatoa maoni haya dhidi ya mawazo mengine ya watu wengine ambao wanashawishi zoezi la kupiga kura ya maoni juu ya Katiba mpya lisifanyike. Wao nao wanazo sababu zao ambazo kwa mtazamo wao wanadhani ni za muhimu.
Sisi tofauti na wao nadhani kufanya hivyo ni kutukwaza, kutuchelewesha, na kutuyumbisha; kwa sababu kama suala ni uhalali wa mchakato, ushirikishwaji duni au kuburuzana yote hayo yanajibiwa na kura ya hapana. Na kama zoezi ni halali, haki ilitendeka, na katiba ni nzuri basi yote hayo yanajibiwa na kura ya ndiyo. Kwa kutoa haki pande zote suala la kuipigia kura rasimu ya katiba ni muhimu.
Kivulini kwetu hatukutaka tuseme; labda kwa kulazimishwa, kuwa mshindani huwa haleti vikwazo na hagomi kuingia ulingoni isipokuwa pale tu ambapo huwa ana mashaka na ushindi wake.
Kama hukuingia ulingoni kujipima uwezo wako ni lini basi utakuwa na uhakika na kiwango chako ?Kama hatupiga kura kuikubali au kuikata Rasimu hii ni njia gani sahihi itatuhakikishia kuwa Rasimu hii ni mbaya au nzuri; tukisie tu !; na kwanini tuandikie mate ilhali wino tunao ?
?
Nilidhani kila mmoja wetu atajitahidi kuwaelimisha anaowadhani hawaelewi ubaya, uzuri, mapungufu, na makunjufu ya katiba ili kumweka kila mwananchi katika ufahamu wa kumwezesha kuamua apige kura ipi siku itakapowadia kuipigia kura Rasimu ya Katiba.
Tunasema hivi kwa sababu hatuelewi nini kitafuata endapo rasimu hiyo haitapigiwa kura........mchakato utaanza upya ?, ama zoezi hilo litasitishwa na iwe basi, au itakuwaje ? Na je muda na gharama zilizotumika itakuwa ndiyo basi tena ama vipi ? Na kauli ya nani itakuwa kipimo cha kufikia maamuzi ya kutopiga kura ? Kwa sababu taratibu na kanuni zilizopo zinaelekeza kura ipigwe.
Bado hatujakubali kuwa hata kama kila kitu tunachosema hakikuzingatiwa kingelizingatiwa; Katiba hiyo isingelikuwa na mawazo yote tuliyonayo, bado tungelihitaji kupata fulsa nyingine wakati mwingine kuipitia tena na kurekebisha hapa na pale kulingana na mahitaji na muda utakaokuwepo. Sasa basi kwanini tusiipigie kura Rasimu hii kwanza tukajihakikishia kuwa ni kwa kiasi gani tunaikataa ama kuikubali ili hata kama tunaingia hasara basi tuwe wote tumeikubali kwa sababu ambazo wengi wamezikubali.
Ushauri wetu ni kwa kila mmoja wetu kujikita katika kutoa elimu juu ya Rasimu hii na kumwandaa mwenzake au kujiandaa yeye kuipigia kura Rasimu ya Katiba ili tuweze kuingia katika hatua inayofuata kwa amani bila ya makelele wala fujo.
No comments:
Post a Comment