Tuesday, 7 July 2015

SIMU KUTOKA KWA MGOMBEA MTARAJIWA

Leo alfajiri Kivulini kwetu tumepokea ujumbe wa sauti ufuatao toka kwa Ndugu yetu Mheshimiwa sana mgombea mtarajiwa :

"Halo ndugu zangu Kivulini,

Muda wowote kuanzia sasa Chama chetu kitaanza mchakato wa kutuchuja. Wakati tukisubiri muda huo ufike nilitaka niwatoe hofu wapenzi wangu wote kuwa uwezekano wa mimi kuwemo katika kumi bora hauna shaka kabisa.........tano bora pia sina wasiwasi..............kidooogo nina mashaka na tatu bora; japo hapo napo endapo sifa zitazingatiwa ipasavyo naweza kuvuka.

Moyo wangu unanidunda sana katika kuteuliwa kuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo muhimu. 

Kitu kingine ambacho ningependa kuwapa kama akiba ni kuwa mmoja kati ya jamaa zangu endapo nitaingia nae katika tatu bora nina uhakika kabisa na nafasi ya ugombea mwenza.

Baada ya kuwapa matumaini hayo ningelipenda kuwafahamisha kwamba nitakuwa radhi na matokeo yoyote ili mradi rafiki zangu wawili hawatakuwemo katika tano bora. Nasema hivyo kutokana na harakati zao ambazo kwa kiasi kikubwa kiliathiri sana mchakato huu kwa wagombea wengi tangu utangazaji nia, uchukuaji fomu mpaka urejeshaji fomu kiasi kwamba sina imani na hata mienendo yao hapa mjini katika kipindi hiki kigumu cha subra.

Kitu ambacho ninawapasha wana Kivulini kwetu na wapiga kura wote ni kuwa jiandaeni safari hii kushuhudia maajabu katika uteuzi kwani hautakuwa ndani ya matarajio yenu mlio wengi. Matokeo ya uteuzi yatawaacheni midomo wazi. Cha msingi wote mtafurahia uteuzi huo ambao hautarajiwi.

Mimi japo sijitaji ni miongoni mwa hao ambao wapo nje kabisa ya mawazo yenu na nina matumaini makubwa kabisa ya kuwa mgombea mtarajiwa. Hata hao watakaoingia tatu bora mtashangaa na roho zenu.

Ili nisije nikasema na kupitiliza naomba niishie hapa nikiwaomba ndugu na rafiki zangu mniombee niteuliwe kwani mimi ndiye nitakayekuwa mkombozi wenu pekee  miongoni mwa wagombea wote.

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza."

Tulidhani ni vizuri tukawaonyesha wote ujumbe huu ambao ni kama utabiri wa aina yake ambao pengine utaweka vizuri kisaikolojia wale ambao kwa muda sasa tumekuwa tukijiapiza kuwa matokeo yatakuwa yale tunayoyawaza sisi.

Friday, 22 May 2015


TUSIENDEKEZE UTAMADUNI WA MIGOMO

Kivulini kwetu kwa kipindi kirefu tulikuwa tumesimama kukutana chini ya mti wetu kutokana na hali ya hewa ya mvua na kwamba chini ya mti wetu kulikuwa na tope na unyevu hivyo tulikuwa tunasubiri hali iwe shwari.

Wakati tukiwa katika subira kuna mambo kadhaa yalitokea ambayo kwa hakika mara hali iliporejea kuwa nzuri tulianza nayo katika mijadala yetu.

Moja ya mambo ambayo tulidhani ni muhimu tukaeleweshana ni suala la migomo.

Ni kweli kuwa nchi yetu ni nchi ya demokrasia tena ya vyama vingi. Ni nchi inayoamini katika utawala bora. Ni nchi inayojali haki za binadamu. Ni nchi ambayo inajitahidi sana katika kukwepa udikteta na kuamini kila mtu kujieleza na kudai haki yake kwa kadri ya uwezo wake; wakati mwingine hata kama haki hiyo haipo; mtu ashindwe mwenyewe.

Haki ya mtu kugoma siyo mjadala mkubwa kwetu; mjadala kwetu ni matokeo ya migomo hiyo na namna migomo hiyo inavyochukuliwa.

Tuchukue mfano walipogoma wafanya biashara kufungua maduka wakilalamikia mashine za kukatia risiti. Kwa kuwa ni watu wazima wenye akili timamu tunaamini kabisa walikuwa wanajua wanachokidai. Lakini walipofunga maduka yao nchi ilikosa makusanyo ya mapato kwa siku zote walizogoma. Mapato hayo kwa hesabu zake lazima yalikuwa makubwa na yangeweza kutupa huduma nyingi sisi wananchi wa nchi hii ambamo  na wao wamo. Hatukuelezwa ni hasara ya kiasi gani ilipatikana, pengine akina sisi tungelikasirika zaidi. Madai ya mgomo huo yalikuwa ni ya muda mrefu na kama yangelijadiliwa na kupatiwa ufumbuzi; ufumbuzi ambao umekuja kupatikana baada ya mgomo; hasara hiyo isingelipatikana.



Hasara nyingine ni ya usumbufu kwa wananchi ambao walikuwa wanahitaji kununua aidha vyakula au vifaa mbalimbali kwa ajili ya kazi zao. Wengine walikuwa wametoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya kufanya manunuzi. Wote hawa mbali na usumbufu wapo walioingia gharama kutokana na maduka hayo kufungwa. Gharama hizo hawana wa kumdai.

Mfano mwingine ni mgomo wa madereva. Hawa waligomea kusomeshwa tena kusomeshwa kwa gharama kubwa waliyodai iko nje ya uwezo wao. Waligomea pia kufanyishwa kazi bila ya mikataba na malipo madogo na mapungufu mengi katika ajira zao. Hili nalo lilikuwa linaweza kuzungumzwa na wahusika na kufikia makubaliano ambayo yalikuja kufikiwa baada ya mgomo. Kilichotokea wakati wa mgomo huo ni usumbufu kwa watu chungu nzima.



Sijagusia mgomo wa wenye magari ya usafirishaji, migomo bubu ya kufunga barabara ambayo sasa hivi imeshamiri; usilogwe sasa hivi kumgonga japo mbwa wa mtu; kesho utakuta mawe yamepangwa barabarani wahusika wakidai hiki ama kile.



Kivulini kwetu tunasema kuwa kila kunapotokea migomo huwa wanaoathirika zaidi ni watu ambao hawahusiki kabisa na chanzo cha migomo hiyo wala hawana maamuzi yoyoye juu ya utoaji wa hayo yanayogomewa. Na pindi wanapopata hasara iwe ya gharama yoyote huwa hawana wa kuwafidia na wakati mwingine huwa hata radhi hawaombwi. Hii kwa kweli si haki. Kama waliogonma walikuwa wakidai stahiki zao; iweje hawa nao walioathirika na migomo bila kuhusika na lolote wawe hawana haki yoyote.



Kivulini kwetu tulikuwa tunaiomba jamii yetu itafakari upya juu ya utaratibu huu wa kudai haki kwa kukiuka haki za wengine. Mwingine kumwaga damu kwa ajili ya kutetea damu ya mwingine bila makubaliano yoyote.

Kivulini kwetu pia tulikuwa tunaiomba jamii ielewe kuwa wasije wakadhani makundi mengine yameridhika na hali zao; kilichopo ni kuwa makundi mengine yanafanya ustaarabu kwa kutiojiingiza katika kero ya kuwakera wengine ili kupata haki zao.

Kivulini kwetu tulikuwa tunawaomba wote waliogoma na wenye nia ya kugoma wakumbuke kuwa endapo kila mtu atagoma kwa wakati wake ili kudai chake, ipo migomo ambayo itagharimu maisha ya wengi. Kumbukeni walipogoma madaktari hali ilikuwaje; kumbukeni walipogoma walimu hali ilikuwaje; kumbukeni walipogoma wanafunzi wavyuo vikuu hali ilikuwaje.


Chukulia Wakulima wakigoma na mazao yao itakuwaje; chukulia Polisi wakigoma kupokea mashtaka yetu tukiparurana uswahilini itakuwaje; Wanajeshi wakigoma kulinda mipaka yetu itakuwaje; Wenye Bar na wauza Bar wakigoma wanywaji itakuwaje, wakigoma wahudumu wa usafi wa majiji wiki nzima itakuwaje mijini; wakigoma wahudumu wa Mochwari mambo yatakuwaje; wakigoma wauza bidhaa masokoni mapochopocho tutayanunua kwa nani; akina mama wakiwagomea waume zao au waume kuwagomea wake zao; hali itakuwaje katika familia zetu; Mahakimu wakigoma wahalifu mtawashitaki kwa nani; Kivulini kwetu tunasema na Rais wetu nae akigoma kama alivyofanya wa Burundi hali itakuwaje...........ebu tubadili huu utaratibu wa kugoma na kusababisha maafa kwa ambao hawakuyasababisha matatizo yetu. Tuwe na utaratibu wa kuzungumza na kukubaliana mapema; hii ni kwa wanaodai na wanaodaiwa; kama uwezekano upo basi wenye haki yao wapewe mapema kuliko kusubiri mpaka wengine wasumbuliwe ndipo mje na kukubali mnachoombwa.



Kivulini kwetu tunaamini kwamba ni wajibu wetu kuelimishana na kuwekana sawa kwa sababu kila mtu anayo haki yake kama aliyonayo mwenzake. Kuwepo na utulivu haina maana ya wasiogoma kuridhika na kila kitu bali ni ustaarabu wa kuamia kutumia busara katika watu kupata mahitaji yao na kudsai haki zao bila ya kuwasababishia wengine usumbufu vinginevyo kila mtu akiingia mtaani kudai chake hatutakuwa na nchi kama ilivyo sasa bali uwanja wa mauti.

Sunday, 5 April 2015

TABIA MBAYA ZA WAHUDUMU WA BAR NA HOTELI

Kama mjuavyo leo ni sikukuu ya Pasaka. Pamoja na kuwa si maadili lakini hiyo ndiyo hali halisi ilivyokuwa; Kivulini kwetu na sisi tuliamua kutoka kwenda maeneo kusafisha macho. Hatukwenda wote sehemu moja bali tulitawanyika maeneo mbalimbali kwa maelekezo kwamba ifikapo muda tuwe tumerejea kujumuika pamoja kama familia kupata kilichoandaliwa kwa ajili ya siku ya leo.

Kivulini kwetu kutokana na utaratibu wa kuongozwa na nidhamu, ulipotimu muda kila mmoja wetu alifika nyumbani mapema. Kwa kuwa tulikuwa tumewahi ilibidi kusubiri kidogo maandalizi yakae sawa tupate kuendelea na kipindi hicho. Wakati tukisubiri ilianzishwa mada ambayo kutokana na umuhimu wake tusingelipenda kuwanyima ndugu zetu uhondo; na pengine kupata maoni juu ya namna ya kukomesha tabia hizi za hawa ndugu zetu wahudumu.

 Image result for wahudumu wa bar



Mmoja wetu kutokana na alichokiona alisema wahudumu hawa na hasa wa kike wana tabia mbaya sana ya kuwaombaomba wateja wawanunulie soda, bia ama chakula. Inasemekana huwa nawaoni haya wala vibaya kumwomba mteja hata kama hiyo ni mara ya kwanza wameonana nae. Kwa namna wanavyoomba humfanya mteja akereke kiasi kwamba hata akimpa huwa anampa kwa shingo upande ili kuondoa hiyo kero ili aendelee na starehe zake bila ya bugudha yoyote.

 Image result for wahudumu wa bar

Kituko kingine cha hawa wahudumu ni uzito wa kurejesha chenji na hata wakirejesha huwa siyo kamili kwa kisingizio cha chenji kuwa tatizo. Penye 800/= ukitoa noti ya sh. 1000/= usitarajie kuipata 200/=; penye 4000/= au 4500/= ukitoa noti ya sh. 5000/= usutarajie kuipata sh. 1000/= au 500/= na ukiipata ni sharti ugombane. Hii ni kwa upande wa chenji; lakini pia kuna mchezo wa kuongezeana bei; chakula cha 2500/= utatajiwa sh. 3500/=, ama chakula cha 4000/= utaambiwa sh. 4500/= au 5000/= ili mradi kipatikane kiasi chochote mbali na kiasi stahiki wakichukue kama chao. Kazi kubwa huwapata wale ambao huwa wamelewa kidogo ama wanaoonekana wana pesa nyingi na hawapendi kulumbana au kuonyesha wana gubu kwa kudaidai chenji.

Tatizo jingine lililobainishwa kwa ndugu hawa ni udoezi. Wapo wahudumu hasa akina dada ambao hudiriki kwenda kunawa maji kabisa na kuja kuketi mezani kwa wateja na kuanza kula nao vipande vya kuku na mishikaki bila ya hata kukaribishwa kwa kisingizio cha kuonja kama vimeiva au chumvi imekolea; pengine husingizia kuwasindikiza wateja kimaongezi. Wapo ambao huchukua glasi na kumimina soda ya mteja au bia na kunywa. Ukiwaona unaweza kudhani ni wacheshi kwa wateja kumbe ni wadoezi wakubwa.

Tuliambiwa kwamba wapo wahudumu visirani ambao hupenda kuwahudumia wateja wanaokuja peke yao tu na pindi wajapo na wenza wao huwa ni wazito kutoa huduma na watoapo huwa wanenuna ama hutoa huduma mbaya kwa makusudi. Ukiagiza bia baridi utaletewa ya moto, ukiagiza supu ya kuku utaletewa ya mbuzi na wakati mwingine unaweza kuambia kitu fulani hakipo kumbe kipo; wao huwa ni vituko kwa kwenda mbele ili mradi siku nyingine usirudie tena kuja sehemu hiyo na huyo uliyeongozana naye.

Wapo wahudumu ambao wakikuzoea sana huwa hawana adabu wala heshima; anaweza kusema chochote na popote bila kujali uko katika mazingira gani ama uko na nani. Aweza kukwambia amekumiss sana wakati hana uhusiano na wewe; aweza kuanza kukuuliza hali ya mkeo au mmeo wakati hamjui; aweza kukucheka kuwa umefulia kwa sababu leo unakunywa soda badala ya bia; anaweza kukwita shemeji kwa sababu tu jana alikuona umekaa na rafiki yake. Wabaya zaidi ni wale ambao hupita wakitangaza kuwa mteja fulani ni mtu wake na kutoa onyo kwa wenzie wasimhudumie isipokuwa yeye; na wakati mwingine hutwangana makonde kumgombania mtu ambaye hana habari nao kabisa; kisa ni kuwa mteja anaonekana anazo. Utashangaa kama una mazoea na sehemu siku unakwenda unaona kila mhudumu anaogopa kukusogelea kutokana na vitisho wakati mteja mhusika hujui kinachoendelea.

Kero jingine ni wahudumu  ambao huja kazini na kutumia muda wao mwingi kuchezea simu na kusoma magazeti ama kuongea na washikaji wao na kuacha kuwahudumia wateja. Mteja anaweza kukaa zaidi ya dakika kumi bila ya kuulizwa ahudumuwe nini na wakati huohuo kuna wahudumu kibao wamezagaa na kila mmoja anafanya lake ambalo ni nje ya majukumu yake ya kazi. Na akitokea mteja kujaribu kulalamika; majibu atakayopata hatodiriki kurejea tena mahali pale.

Kivulini kwetu baada ya kupata aina hizi za wahudumu tulijaribu kujiuliza kuwa ni nini chanzo cha matatizo hayo. Tulichogundua ni sababu kadhaa ambazo tunadhani zikifanyiwa kazi matatizo haya ya huduma za hoteli na bar yatapungua kama siyo kwisha kabisa.

Tulibaini kuwa sababu ya kwanza ni kuwa wahudumu wengi hawakusomea kazi hizo na wala kupigwa japo msasa wakati wanapatiwa ajira hizo hivyo hawana kabisa elimu yoyote juu ya wanachotakiwa kukifanya; na kuna wengine ambao huwa hata darasa la saba hawakumaliza. Tunadhani wakati umefika wa wenye mahoteli na bar kuajiri wahudumu waliopitia mafunzo ili huduma zikidorora tujue ni sababu nyingine na si ya elimu au mafunzo.

Tulibaini pia kuwa hawa wahudumu wengi hulipwa mshahara mdogo sana usiotosheleza hata nauli ya kuja kazini kwa wiki mbili na pamoja na kuwa mshahara ni mdogo huwa hawapewi wote kwa pamoja na bado kiasi kikubwa hukatwa kwa kisingizio cha kuvunja chupa, glasi n.k. ama kupata shoti katika malipo ya huduma; hivyo ili waweze kumudu maisha inabidi wawe ombaomba kwa wateja wao kufidia upotevu ama kupata cha kurudi nacho nyumbani kwa matumizi yao. Wengine inasemekana hupatiwa nafasi ya kuhudumia lakini bure kwa makubaliano kuwa atumie uwepo wake mahali hapo kupata pesa ya kujikimu; vipi atapata hiyo huwa ni akili kichwani mwake. Tunadhani waajiri wa wahudumu hawa wawe waungwana kwa kuwalipa kwa mujibu wa sheria na kanuni kwani maisha ni magumu na hali ni ngumu sana ya maisha; kumtumikisha mtu bila ya kumlipa sio uungwana hata kidogo.

Tuligundua pia kuwa wahudumu hawa huajiriwa kwa kufuata sura zao na maumbile yao kuwavutia wateja na wala si uwezo wao wa kazi ama wito wa kazi. Na mbaya zaidi hulazimika kutoa rushwa ya ngono kwa wamiliki wa mahoteli ama mameneja wahoteli na bar hizo. Hivyo huwa na kiburi toka siku ya kwanza kwa kuamini hata akifanya madudu tayari alikwisha hakikishiwa usalama wa ajira yake na mwenye mali au meneja. Wenye hoteli na bar wakumbuke hawa ni wahudumu wa watu na wanastahili kuheshimu na kuheshimiwa; kuajiri mtu kama kitu ni kuleta kero mahali pa kazi na mwisho wa siku hata biashara hudumaa kutokana na wateja kuacha kuja mahali hapo.

Kitu kingine tulichokibaini ni kuwa wahudumu hawa wengi wao wamepambana na misukosuko ya maisha mapema kabla ya umri wao. Wapo waliopewa mimba na kukimbiwa; kati yao wapo waliozaa na wengine kutoa mimba. Wapo waliofukuzwa au kutengwa na familia zao kwa sababu mbalimbali . Wapo waliokimbia ndoa zao. Wapo waliokimbia masomo n.k. Kutokana na sababu hizo wengi wao wana hasira na maisha na wanatembea na nadhiri kuwa siku wakipata mwanya wakufanya lolote kulipiza kisasi wanaweza kufanya. Wanaweza kumwibia tajiri, wanaweza kumuibia mteja, wanaweza kumchoma mtu kisu n.k. Hali hii hufanya maeneo ya hoteli na bar kuwa kichaka cha kuficha kundi la watu wenye hasira na walipa visasi ambao kila mtu mbele yao humwona adui. Matajiri wawe makini katika kuajiri kwa kujaribu japo kupata historia za wafanyakazi wao ili kuwa na uhakika wa usalama mahala pao pa kazi.

Kuvilini kwetu inaamini sana katika huduma bora kwa mteja na haki kwa wafanyakazi; na ili kwenda sawa ni vema kufuata taratibu na sheria katika ajira za wahudumu.




Wednesday, 1 April 2015

CHONDE CHONDE SIMU ZITATUPELEKA PABAYA

Kwa kipindi kirefu Kivulini kwetu tulikuwa tunasikia tu kuwa kuna ugonjwa umeingia nchini unaitwa UBISI. Mara ya kwanza kuusikia tulidhani jina limekosewa; kwamba badala ya "ubishi" wameuita "ubisi"; lakini baada ya kuhoji mara mbili mbili tukahakikishiwa kuwa hilo jina la UBISI ni sahihi; kwamba ni kifupisho cha maneno Ulevi Binafsi wa Simu.


Awali tuliuposikia ukitajwa tukajua kuwa hayo ni mambo ya mjini; uzushi, soga, hadithi, mipasho n.k.
Lakini jana kwa mara ya kwanza tulijionea mwenyewe kile ambacho awali tulikipuuza, kuwa nchi imeingiliwa na ugonjwa wa Ubisi.

 Tulikuwa tumepanda gari kutoka Makumbusho kwenda Posta. Kama bahati tulikaa kiti cha nyuma. Tulipofika mataa ya Morocco tukastaajabu kidogo kutokana na ukimya uliokuwepo kwenye gari; tukataka kujua kulikoni;tusije tukawa tumepanda gari la kwenda kwenye msiba. Tulichokiona ndicho kilichotusukuma kuyasema haya; kwamba kumbe karibu robo tatu ya abilia walikuwa wamezama kwenye simu zao. Hata kondakta wa basi ilibidi afanye kazi ya ziada kupata nauli yake; watu na simu, simu na watu.

Tulipofika Posta kama kawaida yetu tukaanzisha mjadala wa wazi juu ya ugunjwa huu wa Ubisi; hapo ndipo tulipohakikishiwa kuwa hivi sasa Simu ni janga la Taifa.


Katika mjadala huo usio rasmi tukabaini mambo mengi sana. Wapo waliosema kuwa Ubisi umevunja ndoa nyingi sana nchini. Wengine wakasema Ubisi umefelisha wanafunzi wengi sana vyuoni. Hapohapo tukaambiwa mbali na ubisi kufukuzisha watu kazi; kwa waliobaki kazini umechangia kushusha viwango vyao vya utendaji kazi. Walinzi wamevamiwa malindoni kutokana na ubisi. Hospitali wagonjwa wamesababishiwa vifo kutokana na ubisi wa madokta na manesi. Familia zimelishwa vyakula  vibichi au vilivyoungulia sababu ya ubisi. Waumini hawasikilizi mahubiri makanisani na misikitini kutokana na ubisi. Makaburini kwenye mazishi ubisi unatuandama. Watoto hawalelewi vizuri sababu ya ubisi wa mama zao na walezi wao. Magari yamepata ajali na watu kuumia au kufa shauri ya ubisi wa madereva. Biashara zimedorora kutokana na ubisi. Nidhamu imeshuka sana kila sehemu kutokana na ubisi. Pesa inaskwisha kutokana na ubisi.


Kutokana na hili sisi Kivulini kwetu tukadhani japo tumechelewa kidogo tuwashike bega ndugu zetu, jamaa zetu na rafiki zetu kuwa tujiangalie na huu ulevi binafsi wa simu. Sasa hivi simu  zimetutawala kiasi kwamba tumejisahau na kusahau wajibu wetu. Toka asubuhi watu tumo katarazaji kutoka Facebook kwenda Twitter; kutoka twitter kwenda instagram; kutoka instagram kwenda WhatApp; kutoka WhatsApp kwenda Viber; kutoka Viber kwenda Tango; kutoka Tango kwenda immo; kutoka immo kuingia google; kutoka google kuibukia kwenye mablog, website na takataka kibao. Na mtu akizama hapo hata umwite vipi hakusikii labda umpige kibao. Hakika huu ugonjwa ni hatari sana japo ni wa kujitakia.


 Na ili uende sambamba nao ni lazima uwe na simu zaidi ya moja na uhakika wa muda wa maongezi. Hutaijua hasara ya simu mpaka uwe mkweli katika kufuatilia kiasi cha pesa kinachotumika kwa ajili ya muda wa maongezi; hufikia kwa wengine simu zao kutumia mara mbili zaidi yao wao binafsi. Ubisi unatupeleka puta.


Pamoja na kuwa simu si anasa; bado nina hofu na matumizi yetu ya simu kama kweli yana tija yoyote katika maisha yetu. Wengi wetu simu zinatuharibia maisha.



Ombi langu kwenu jamaa zangu kila mtu kwa wakati wake ajitolee kuchangia vita vya ubisi kwa kupunguza japo saa moja ya matumizi yake ya kila siku ya simu. Kumbukeni hapo nimeelezea hasara zake kiuchumi tu sijagusia masuala ya mionzi n.k. Naomba kutoa hoja. 


Thursday, 19 March 2015

KURA NA MAFURIKO WAPI NA WAPI ?

Leo asubuhi kwenye daladala tukitokea Kivulini kwetu kuja mjini tulimsikia abiria mmoja akilalamikia lile agizo la watu wa mabondeni kuhama kutokana na kuwepo uwezekano mkubwa wa kukubwa na mafuriko kufuatia mvua kubwa zinazotarajia kunyesha muda wowote kuanzia sasa.



Jamaa huyu alikuwa akililalamikia lile tamko la kwamba safari hii atakayekaidi kuhama yakimkuta mafuriko hakutakuwa na msaada kama inavyokuwa miaka yote. Yeye alikuwa anasema kuhama hatahama na kwamba hayo mafuriko na yaje; ila anaisubiri kama ni hiyo serikali imnyime misaada kama ambavyo huwa wanapata miaka yote. Atakachofanya yeye ni kuhakikisha kuwa hapigii kura rasimu ya katiba iliyopendekezwa na hata uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani hatoshiriki. Huyu ndugu alikuwa anazungumza kwa hisia na hakuwa anatania.

  Alipoulizwa ni kwanini hataki kuhama, yeye akasema katiba ya nchi inamruhusu yeye kama raia wengine kuishi popote anapotaka ili mradi havunji sheria. Na akaendelea kudai kuwa badala ya serikali kumboreshea makazi yake mahali alipo hapo bondeni inamhamisha kumpeleka ugenini huko Mabwepande wakati babu yake, baba yake na yeye mwenyewe wamezaliwa mjini Jangwani.



Alipoulizwa endapo mafuriko yatakuja na kumchukua akafa hiyo kura ya maoni na ya wabunge ataipigia wapi; akajibu kuwa kama kufa angeshakufa siku nyingi lakini amesalimika mafuriko yote tangu enzi leo afe kwa misingi ipi; kwa sababu serikali imesema ?



Huyu ni mmoja kati ya wakazi wengi wabishi ambao wamedhamiria kukaidi kuhama mabondeni. Kukaidi si tatizo. Tatizo ni hapo watakapoathirika na mafuriko na kuilazimisha serikali iwahudumie kwa ujeuri wao Maudhi zaidi ni ule msimamo wao wa kuwa lazima serikali iwahudumia kwa kuwa wao ni wapiga kura wa nchi hii.



Kivulini kwetu kwa hakika tumesikitishwa sana na ukaidi wa aina hii; wa mtu kufanya makusudi kuyatafuta matatizo na kulazimisha kutatuliwa matatizo kwa kisingizio cha katiba. Mtu wa aina hii hatofautiani sana na mtu anayekunywa sumu au kujinyonga kwa madai kuwa hawezi kufa na akifa basi siku zake zimefika. Watu hujiua faragha, lakini mbele za watu lazima binadamu waungwana watachukua hatua za kukuokoa, na wanapokuakoa huonyeshi kujali walichofanya kwa madai kuwa huo ulikuwa ni wajibu wao.



Hivi mpiga kura wa aina hii ni mgombea gani anayemtaka ? Lakini ajabu ni kuwa wapo wagombea wanaopenya mabondeni usiku na kuwaambia hao jamaa wapiga kura wao wasihame; kwamba wapo pamoja nao kwa lolote liwalo, na wasiwe na wasiwasi hata wakikubwa na mafuriko watahakikisha misaada kutoka serikalini inapatikana. Hizo ndiyo siasa za uchaguzi, kuomba kura juu ya maisha ya watu. Na je wapiga kura hao wakizama kabisa na kufa watawapelekea viroba vya maisha au uhai huko mochwari ili wafufuke waje kuwachagua.



Kivulini kwetu tulidhani ni wajibu wetu kuwafahamisha ndugu zetu mfahamu nini kinachoendelea. Mwaka huu ni wa uchaguzi na katika mafuriko yajayo lolote linaweza kutokea. Kama kweli tunawapenda wenzetu tuwasaidie sasa kwa angalau kuwashawishi na kuwasaidia wahame mabondeni ili tuwe nao salama hadi Oktoba mwaka huu tupate mchango wao. Isifike mahari tukawa na mashaka kuwa jeuri hii ni ya kufanya mafuriko kuwa mtaji wa kujikimu kimaisha wa kila mwaka  kwa waathirika na mtaji wa kura kwa wagombea kwa kila kipindi cha uchaguzi. Lakini tujiulize wenyewe KURA NA MAFURIKO WAPI NA WAPI ?

Wednesday, 18 March 2015

TUPIMIANE VIWANJA KILA MTU AFE NA CHAKE

Kama ilivyo ada Kivulini kwetu huwa hatukosi kero. Kero hizi huwa hatuzitafuti bali huwa zinatukumba kutokana na mazingira yenyewe yalivyo; mambo ya utandawazi, mambo ya tabia nchi, hali ya miundombinu na wakati mwingine ukosefu tu wa mirejeshonyuma  juu ya masuala kadhaa ambayo tunadhani ni ya muhimu katika jamii yetu.

Safari hii tunaomba tuliweke wazi suala la viwanja ama ardhi katika ujumla wake. Tunaliweka wazi kwa sababu limeshakuwa tatizo na siku hadi siku linaendelea kukua kiasi kwamba limekuwa likisababisha majerudi na vifo kama ajali za barabarani.


Suala la ardhi halikutakiwa lifikie hapo kama kwa kweli nia ingelikuwepo ya kuondokana na adha hii. Inaelekea watu hawajali na pengine na serikali nayo imechukulia rahisi suala hili. Tunasema hivi kutokana na ukweli kwamba kuna migogoro mingine ingeliweza kutatuliwa bila hata ya gharama zozote zaidi ya maamuzi tu ya kuelekeza hawa waishi kule na wale waishi huku. Kwamba kutokana na maelekezo tu yasiyoeleweka kumetokea ugomvi katika baadhi ya maeneo kiasi cha kusababisha hasara za mali na upotevu wa viungo na maisha. Wakati mwingine tunafika mbali kwa kuwaza kuwa huenda ulegevu huu katika masuala ya ardhi wapo watu wananufaika ya migogoro hiyo.

Katika tatizo hili la ardhi kumekuwepo na maeneo ambayo wakati wa sehemu hizo kwa miaka nenda rudi wamepokonywa na maeneo hayo kugawiwa wengine  kama wawekezaji na wakati mwingine si wawekezaji kitu. Unakuta ardhi ya kijiji kizima kinagawiwa mtu mmoja na kwa bahati mbaya sana mtu huyu kwa miaka kadhaa anakuwa hafanyi chochote katika eneo hili zaidi ya kuweka walinzi kuhakikisha mtu haingii eneo hilo. Usumbufu kwa wengi kwa ajili ya fahari ya mtu mmoja; taifa halifaidiki na jamii haifaidiki.


Yapo maeneo ambayo wananchi wamenyang'anywa bila ya majadiliano wala makubaliano. Wakihoji najibu yanakuwa ardhi ni mali ya serikali hivyo chochote kinaweza kufanyika. Lakini ni kweli haki kumpokonya ardhi mkazi wa siku nyingi na kuigawa ardhi hiyo bila ya kumweleza utaratibu utakuwaje baada  hapo ? Huyu au hawa walishajenga nyumba zao, walishapanda mimea yao ya kudumu, walishajipangia maisha yao hapo. Wakitoka hapo waende wakavamie wapi ili maisha yaendelee; huko ambako tafrani kama hii iliyowakumba haitawakumba ? Wakati mwingine jinsi wanavyoondolewa katika maeneo yao nyumba huchomwa moto au kubomolewa.


Kuna maeneo wananchi wanavamiana. Wafugaji wanawavamia wakulima. Wakulima wanafyeka mashamba maeneo ya wafugaji. Hakuna mipaka, hakuna utaratibu, hakuna sheria ila ni kila mtu na ubavu wake; mwisho wa siku eneo linakuwa halilimiki wala halifugiki; kila siku vilio.



Wote tunajua kuwa Watanzania wa leo wanalenga kila mtu kuwa na makazi yake. Miji inapanuka; Dar es salaam inakutana na Kibaha n.k. Watu wanauziana mashamba, mashamba yanakuwa makazi. Lakini viwanja havipimwi, ujenzi unaendelea holela; hakuna maeneo ya wazi, hakuna barabara, hakuna huduma; kila mtu kwa uwezo wake. Mjini humo kuna wanaofuga nguruwe, ng'ombe na mbuzi. Mjini humo kuna wenye viwanda vya kuranda mbao, kusindika mafuta, kusaga viungo vya pilau na viwanda vya gongo. Mjini humo humo kuna kumbi za kukesha za disko, kuna bar jirani na shule, misikiti mkabala na makanisa n.k Haya mambo yamejengwa holela; hayafungamani, hayatangamani na mpangilio wake tu ni kero.


Ukija uswazi huku ndiko maisha magumu. Choo mlangoni kwa jirani. Gari unaliacha mtaa wa pili, barabara haipo zaidi ya uchochoro. Ukitokea msiba hakuna mahali pa kupitisha jeneza, inabidi mwili ubebwe hadi mtaa wa pili ndipo upambwe. Watoto hawana pa kucheza, na ukitokea moto mtaa huo kunakuwa hakuna jinsi zaidi ya kuupigia makofi moto uteketeze nyumba salama.

Maisha kuhusiana na viwanja ama ardhi kwa ujumla ni kero. Tusichokielewa Kivulini kwetu ni kwanini iwe hivyo. Inakuwa hivyo kwa faida ya nani. Na itakuwa hivyo hadi lini.

Kinachojitokeza ni kutokuwepo na mipango mahususi ya upimaji wa viwanja, ugawaji wa viwanja na urasimu mwingi katika kutoa hati za viwanja; kwa ujumla suala la viwanja na ardhi limejaa urasimu kiasi kwamba kwa mtu wa kawaida linatia kizunguzungu.


Kivulini kwetu tunauliza, ni kwanini kama wizara inaona suala hili limewazidi kimo shughuli hii ya upimaji wasiibinafsishe. Tunaziuliza mamlaka zenye wakazi wenye shughuli zinazokinzana kama vile wafugaji na wakulima kwanini wasitengewe maeneo kwa uwazi na uhakika ili kila mtu ajue mipaka yake ili kuondokana na  hali hii ya sasa na kutumishiana misuri.

Na hawa wawekezaji mwitu wanaopewa ardhi maekali kwa maekali tena yenye rutuba lakini hawayafanyii chochote kwa miaka nenda rudi na kuwaacha wakazi katika maeneo makame wanaachiwa kuendelea kumiliki maeneo hayo ?


Kivulini kwetu tunashauri serikali itupimie kila mtu na eneo lake, apewe hati yake aishi kwa amani. Ipime na igawe maeneo kwa kila kijiji ili kijue mipaka yake. Wakulima waelekezwe maeneo yao, wafugaji weaonyeshwe maeneo yao. TUPIMIANE VIWANJA NA ARDHI YETU KILA MMOJA AFE NA CHAKE.

Tuesday, 17 March 2015

BAYA MOJA HUFUTA MEMA MENGI

Leo Kivulini kwetu tulikuwa na mjadala wa kijamii juu ya tabia inayoambatana na msemo wa BAYA MOJA HUFUTA MEMA MENGI. Sambamba na kujadili tabia hiyo tukawa pia tunajiuliza ni kwa nini kwa manufaa ya jamii tusingelibadili tabia na kufuata usemi wa JEMA MOJA HUFUTA MABAYA MENGI.

Katika kuiangalia jamii yetu tumekuta tabia hii imekuwa ikimuathiri kila mmoja wetu katika maeneo na nyakati tofauti.

Utakuta mtu ni mfanyakazi katika ofisi fulani. Pengine huyu ndugu kwa miaka zaidi ya kumi ya utumishi amekuwa akifanya kazi zake vizuri kwa uaminifu na unyenyekevu.Na si hivyo tu, pengine ni mbunifu na ameliingizia shirika au kampuni mamilioni ya fedha kwa kiaka nenda rudi. Siku moja baada ya miaka 10 akatokea kufanya kosa, pengine la upotevu wa kiasi kidogo sana cha fedha ama uzembe wa kusababisha hasara ya kiasi kidogo sana cha fedha; kinachotokea ni kuwa uongozi au utawala bila kuzingatia mchango wake wa kiaka kumi watamtimua kazini na wakati mwingine kumdhalilisha mpaka kwenye vyombo vya habari; hivi ni kweli kampuni haiwezi kuheshimu mema na mazuri aliyofanya mtumishi huyu kwa kipindi chote cha utumishi wake  ? Hivi mfanyakazi bora kwa miaka mitatu mfurulizo katika kampuni anaweza kuchukuliwa sawa na mfanyakazi mwingine ambaye hajawahi kuchukua tuzo yoyote mahali pa kazi ?



Utakuta kijana kasomeshwa na familia na hatimae kapata kazi. Baada ya kuwa kazini akawa si mchoyo kwa kujitahidi kumsaidia kila ndugu atakayekuja kuomba msaada kwake. Ndugu watasaidiwa na watamsifu kutokana na wema wake. Baada ya muda kijana wao atakuwa na familia na hivyo majukumu yake kuongezeka na kubadilika. Kidogo kidogo ataanza kushindwa kutoa misaada kama awali na pengine kushindwa kabisa kuacha familia yake ili asaidie ndugu. Hapo sasa ndipo ndugu wataanza kuja juu kuwa kijana wao toka ameoa amebadilika sana. Na hawataishia hapo bali watamwita mpumbavu kwa kuwasaidia wakwe zake badala ya wazazi wake; watasema mkewe au mmewe kamroga ili asisaidie familia yake n.k Kisa wamekwenda kuomba wakakosa kupewa.



Utakuta katika chama cha siasa kuna wanachama ambao wamefanya kazi kubwa sana katika kukijenga chama; wakati mwingine walilazimika kutoa mali zao ili chama kisitetereke. Wapo waliouza utu wao na kuhatarisha maisha yao ili kuhakikisha chama kinasonga mbele. Lakini siku wanahoji chochote katika chama, viongozi bila kujali mchango wao na haki yao ya msingi katika chama watawatengenezea zengwe na kuwafukuza katika chama.



Utakuta katika Klabu ya soka mchezaji amekuwa ndiyo tegemeo. Mchezaji huyo pengine ndiye aliyechangia  kuipandisha daraja timu; ama ndiye aliyekuwa msaada mkubwa kuhakikisha timu haishuki daraja; ama ndiye mfungaji hodari kiasi cha timu kunyakua ubingwa mara kadhaa. Yeye kama binadamu anaweza kukosea ama wakati mwingine kwa kumdhania tu kuwa ameuza timu; klabu huuvunja mkataba wake ama kumfikisha mahakamani kwa sababu hii au ile na kusahau kabisa mangapi alifanya kwa  manufaa kwa klabu.



Utakuta mume au mke amekuwa mwaminifu katika ndoa kwa kipindi cha miaka chungu nzima lakini ikatokea siku akachepuka, basi hiyo kesi haitaisha na hakutakuwa na msamaha mpaka na ndoa inavunjika; kisa ni kosa la siku moja ndani ya uaminifu wa miaka hata zaidi ya ishirini.




Kivulini kwetu tuliibua mifano mingi sana ya athari za tabia hii ya kufuta wema wote kwa ubaya wa siku moja na kujiuliza hivi sisi wanajamii tabia hii itatusaidia nini; ni kwanini tumekuwa wepesi wa kusahau mema na kutoa maamuzi makali hata pale tunapohakikisha kuwa hili ni kosa la kwanza. Ni kwanini hatui wavumilivu; kwanini hatupeani ushauri nasaha; kwanini hatusameheani zaidi badala yake tunakuwa wepesi wa kuhukumiana. Kwa taarifa ya mjadala huu tuna imani wengi watakaosoma watatafakari ya kuchukua hatua.

Thursday, 5 March 2015

SAFARI YA KUTOKA UZALENDO WA KAWAIDA KWENDA UASI KUPITIA UZALENDO CHOTARA

 Leo Kivulini kwetu tunakuja na kilio kingine ili tuungane na Watanzania wenzetu wenye mawazo kama yetu kukataa na kuchukua hatua kabla hatuhafika mbali.

Kilio chetu ni juu ya zile harakati za kutusafirisha bila ya ridhaa yetu kutoka kwenye Uzalendo halisi wa nchi yetu kutupeleka kwenye Uzalendo Mwitu au Uasi kwa jina jingine dhidi ya nchi yetu.

Japo tumechelewa kutafakari lakini ni heri tumejitahidi kuliwaza hilo wakati tayari tumekwisha fikishwa katika Uzalendo Chotara.

Wataalamu wanasema siku zote ukiweka viumbe wawili wenye asili moja iwe ni mmea au mnyama na wakakaa kwa kipindi fulani, cha kwanza kutokea huwa ni kiumbe chotara na baadae kiumbe cha asili mojawapo.




Tunaamini kuwa yeyote anayejichanganya kimaongezi mitaani na katika mitandao atakubaliana na sisi kuwa kauli, mawazo na mtizamo wa wananchi wengi kwa sasa unaashiria ukomavu wa Uzalendo Chotara; yaani mawazo na mtizamo wa wananchi kutoridhishwa na mwenendo mzima wa nchi yao, wananchi kutowapenda viongozi wao, wananchi kulalamikia karibu kila jambo, Uzalendo wa kubeza, kukejeri, na kulaani kila jambo. Kauli za utengano, kauli za dharau,  na kauli za vitisho. Kuna kauli nyingi sana ambazo hatukuzoea kuzisikia katika nchi yetu sasa hivi zimekuwa ni za hawaida; watu hawaoni haya wala hawaoni vibaya.

Kivulini kwetu tumebaini kuwa kustawi kwa uzalendo huu chotara hakukuja kama ajali; tunaamini kabisa uzalendo huu ulitokana na mchanganyiko wa Uzalendo halisi na Uzalendo mwitu. Watu waliudaka Uzalendo mwitu katika upya wake wakidhani kuwa huo ndio ustaarabu. Kwamba ili uonekane msomi mzuri basi uwe na kifua cha kuisema serikali na kukashifu nchi; kwamba ili uonekane tajiri basi shurti uwakashifu wananchi na uwakejeri viongozi; kwamba ili uonekane umetembea sana duniani, basi uweze kuponda mambo ya kwetu na kuimba mambo ya ughaibuni; kwamba ili uonekane mtu makini ni lazima uchote fedha za umma na uhujumu nchi;  Tuliingia mkenge kupitia utandawazi tukajiona tumepata na kumbe tumepatikana.

Hapo mwanzo ilikuwa ni aibu mtu kusimama na kujidai kuwa ana shamba ekari 2000 Mpanda;  au ana maroli 90 ya kusafirisha mafuta ama ana vijisenti kama dola 20 milioni Uswisi  kwani ni kiasi ambacho kilikuwa kikivuta hisia ya utovu wa Uzalendo. Sasa hivi hata wanafunzi wanaweza kuwa na mali; nani atawauliza ? Nakumbuka enzi ya Sokoine mtu kuonekana na bidhaa kiasi fulani; haikuwa na haja ya mamlaka kumfuatilia bali yeye mwenyewe kwa jinsi alivyolelewa alikuwa anaona aibu. Waswahili wana sema kawaida ni kama sheria. Watu kama Sokoine hawakumbukwi kwa ukorofi wala sura zao bali wanakumbvukwa kwa Uzalendo wao.

Tumefika mahali ambapo Uzalendo Chotara huo unaanza kututafuna. Tulianza kwa kulia kizaire kwa kutumia magitaa sasa hivi tunalazimika kulia kwa midomo na machozi machoni. Tumechoka na mvurugano wa mawazo, tumechoshwa na msongamano wa itikadi na tumechanganyikiwa na hekaheka za falsafa  kila uchao. Tunaamini yapo mazuri na tunaamini pia yapo mabaya lakini kuyapambanua inatupa shida kutokana na kupigiwa makelele kila uchao na magwiji wa Uzalendo Mwitu. Sasa hivi wao ndio wanaojua kila kitu na wanatulazimisha na sisi tufanye watakavyo. Haiwezekani.

Tunadhani ni wakati muafaka kuelezana haya ili kukusanya nguvu tuweze kuachana na safari hii mbaya. Ikiwa hapa tu katikati tulipofika hali imekuwa mbaya kiasi hiki je tukizidi kuendelea huko itakuwaje ? Tunadhani ule Uzalendo tuliouacha nyuma ndio mali kuliko huo Uzalendo Mwitu tunaoufuata. Kama maendeleo ndiyo haya ni heri turudi nyuma kwani hata tukiyapata maendeleo hayo hayatusaidii; sana sana yatatuacha tukiwa mahututi na taabani.

Wednesday, 4 March 2015

 NINA MASHAKA SANA NA KUNDI HILI LA VIJANA



Jana jioni Kivulini kwetu tulikuwa na mjadala juu ya kundi la vijana. Kundi tulilokuwa tukiliongelea ni kundi la vijana wasomi na wasiosoma, wadogo kwa wakubwa lakini ambao wapowapo hawana mbele wala nyuma. Kundi hili ni la vijana waliomaliza shule au vyuo lakini hawana la kufanya na ni kundi linalojumuisha vijana  wenye afya na uwezo wa kufanya kazi. Hili ni kundi linalokula kwa kengere makwao ama kundi linalozagaa kujidonyolea mitaani na usiku kulala kwenye magofu, upenuni mwa nyumba, kando ya barabara ama kukesha wakinywa viroba, kubwia unga au kuvuta bangi waweze kupoteza mawazo.

Kivulini kwetu tulilifananisha kundi hili na nyasi kavu msimu wa kiangazi; nyasi ambazo akitokea mlevi akatupa kichungi kisichozimwa juu yake; moto utakaolipuka hapo kuuzima ni majaliwa yake mola. Kundi hili tulilifananisha ya sinia la dagaa wabichi wazima linaloelea ziwani ambapo yakitokea mawimbi wakati wowote hutakuwa na kitu katika sinia bali matone ya maji kwani wote wakakuwa wameishia ndani ya maji.

Kundi hili la vijana ni kubwa na siku hadi siku linaendelea kukua katika miji yetu. Tumekuwa na vijana wengi ambao mchana kutwa wanashinda wamejiinamia, wanawaza, kufikiri na kupanga mipango ambayo hatuijui ni ipi na kwa hakika hatujui hatma yao itakuwaje.Kundi la vijana wenye hasira na chuki kwa nchi yao. Vijana ambao wako tayari hata kumtafuna na kummeza mbaya wao endapo wataonyeshwa kwa kidole kuwa huyo ndiye anayewasababishia matatizo waliyo nayo.

Hawa ni watoto wetu, jirani zetu, shemeji zetu na kwa kila hali wanatuhusu. Kwa kuwa wanatuhusu ni wajibu wetu kujua wanaishije; kwa maana ya kuwa tujue wanakula nini na wapi, wanalala wapi na wanamudu vipi kuzipata japo hizo huduma japo ni duni. Tunapaswa tujiridhishe na uhalali wa maisha yao kabla makubwa hayajatukuta.

Kivulini kwetu tulifanya tathmini ya haraka na kubaini kuwa zipo familia nyingi ambazo baba au mama ama baba na mama wana jukumu la kulisha ndugu wasiopungua sita ambao wapo tu hapo nyumbani kwao wakiwa hawana kazi yoyote kutwa nzima zaidi ya kuangalia TV na kuwapokea wenye nyumba vifurushi warudipo nyumbani.

Tulikwenda mbali zaidi na kubaini kuwa katika hali halisi ya kipato cha Mtanzania wa kawaida, mshara wake unamtosha kula yeye na mkewe tu na pengine usiwafikishe mwisho wa mwezi. Kufika hapo tukajiuliza kama ndivyo wanafamilia hawa wanamudu vipi kuwahudumia hawa ndugu wa ziada katika familia zao; tena kwa kipato cha halali.?

Tumekuta ni wachache sana wenye vijimradi ambavyo vinawapunguzia makali kwa kipato zaidi kujazia mshahara lakini kundi kubwa tukaanza kulishuku kuwa linaendesha maisha kiaina. Linaendesha maisha kwa kukopa, kuiba, kutapeli, na kula rushwa makazini kwao na mitaani. Ikiwa mahitaji ni 700,000/= kwa mwezi na kipato ni 300,000/=; unaweza kujitahidi kuziba pengo kwa mwezi mmoja lakini kwa mwaka ni lazima uingie msituni ukasake nyoka; ukatapeli, ukakope, ama ukapokee rushwa. Na kadri majukumu yanavyoongezeka katika familia na utapeli, rushwa, wizi na ukopaji pia unaongezeka. Hii kitaifa ni hatari kuwa sana.

Mada yetu kuu haikuwa athari za kifamilia zinazoletwa na vijana hawa bali tulikuwa tukijitahidi kukuna vichwa juu ya nini tufanye ili kupunguza joto linaloletwa na vijana hawa kwa sababu mateja wamo katika kundi hili, panya rodi wamo katika kundi hili, waandamanaji wa kukodi wapo katika kundi hili, vibaka, machangudoa, wapiga debe, watoto wa mitaani, ombaomba, na wengine wengi ambao mbali na kuwa mzigo kwa jamii wamekuwa tishio la usalama na amani katika taifa letu.Hawa wako tayari kuunga mkono chochote kiwe cha halali ama hatari ili mradi wahakikishiwe kuwa watapata kitu. Kwa bahati mbaya kundi hili limekuwa likitumiwa kwa maasi zaidi ya mambo mema; kulipwa kidogo na kicha kuachwa wakiwa na majeraha ya mwilini na mioyoni.

Kivulini kwetu tunasikitishwa na kuongezeka kwa kundi hili katika nchi yenye ardhi kubwa na nzuri, nchi yenye madini mengi, nchi yenye wanyama wa kila aina, na nchi yenye amani na utulivu. Miji yetu ina kazi nyingi za kufanya na wafanyaji wengi wanazagaa lakini tumeshindwa kabisa kuunganisha kazi na wafanya kazi ili tuweze kuondoa aibu hii ili  kundi hili litusaidie  kusonga mbele kimaendeleo.

Mfano mdogo usio na gharama; tukienda mjini Dar es salaam kumejaa takataka kila mtaa, wakazi wa mitaa wanazichukia taka hizo na wanazo fedha za kuwalipa wazoaji taka; hapo hapo mjini ndiko kwenye vijana wengi wanaoshinda wakiranda bila ya kazi ya kufanya mpaka wanaishia kutapeli ama kuwachomoa watu mifukoni ili wapate pesa ya kununua chakula.

Kivulini kwetu tunajiuliza hivi wana Ustawi wa jamii wako wapi watusaidie mawazo juu ya kuwasaidia vijana wetu hawa ? Wizara husika wana mipango gani juu ya vijana hawa ? Umoja wa vijana wa kila Chama cha Siasa ni nini mchango wao kwa vijana hawa ambao ndio wapiga kura na wadau wao ? Mashirika ya Dini na madhehebu mbalimbali, zaidi ya nasaha mnawasaidia vipi vijana hawa. KUMBUKENI KUWA HAWA NDIYO NGUZO YA TAIFA; WAKIOZA HAWA NA TAIFA LITAKUWA LIMEOZA.

Mjadala huu bado haujafika mwisho. Kivulini kwetu kwa leo tutaishia hapa lakini tutaendelea nao ili tuhakikishe tumeridhishwa kuwa umeeleweka ipasavyo katika jamii yetu na hatua zinachukuliwa.

Monday, 2 March 2015


 EBU FIKIRIA WEWE UNGELIKUWA ALBINO UNGEJISIKIAJE

Jana kwa bahati nzuri tuliwahi kurejea Kivulini kwetu na kubahatika kuisikiliza hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Kikwete. Ilikuwa fupi nzuri na katika muda muafaka.

Ndani ya hotuba hiyo kulikuwa na mambo kadhaa ambayo singelipenda nirarejee ila miongoni mwayo lilikuwepo suala ya Mauaji ya Albino(Ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi). Sipendi nirejee alichosema ila ningelipenda niliongee kwa namna nyingine; nia ikiwa ni kujaribu kuwasaidia wale ambao pengine hawakuweza kuelewa nini kilichokuwa kikisisitizwa katika hotuba ya Rais.

Nadhani wote tunakubali kuwa hayupo aliyebahatika kutoa maoni ama mapendekezo azaliwe vipi; hivi tulivyozaliwa tulijikuta tumezaliwa hivyo. Wapo watu ambao wangelipenda wazaliwe wanawake lakini kwa mapenzi yake mola wamejikuta wamezaliwa wanaume. Na wako wanaume ambao wangelipenda wazaliwe wanawake lakini bahati haikuwa yao badala yake wamezaliwa wanaume. Ni kwa mifano hiyo walioutaka ufupi wakapewa urefu, walioutaka weupe wakapewa weusi na kadharika na waliotaka wazaliwe kawaida wakazaliwa Albino. Na ndiyo sababu kila uchao binadamu hujifanyia marekebisho katika kazi ambayo mwenyezi mungu aliifanya bila ridhaa yake ili angalau kuifurahisha nafsi yake. Tumeshuhudia wanaume wakisuka nywele na kuvaa bangili na mikufu ili angalau wafanane na wanawake; tumeshuhudia akina mama wakijichubua kutoa rangi nyeusi wawe weupe na kuvaa nywele za singa wawe kama wazungu au waarabu; tumeshuhudia wafupi wakivaa viatu vya mchuchumio waonekane angalau warefu kidogo; tumeshuhudia wembamba wakinywa dawa za "kichina" wawe wanene; na mengine mengi. Lakini katika madawa yote sijaisikia dawa ya kumfanya Albino awe na ngozi ya kawaida; pengine wangeliweza kubadili ngozi zao ili kujisalimisha na wauaji hawa.

Kwa kuwa hayupo hata Albino mmoja aliyeomba azaliwe hivyo bali wamezaliwa kwa mapenzi yake mola. Mimi au wewe tungweliweza kuzaliwa Albino kwa sababu tunajua hatukushiriki kujichagulia rangi ya kuzaliwa nayo. Sasa kwa ukweli huo hii jeuri ya kwanza kuwanyanyapaa Albino inatoka wapi na hii imani ya kuwa Albino wanavuta mafanikio inatoka wapi. Rais kauliza jana kuwa kama imani hiyo ina ukweli wowote kwanini basi hao Albino wakiwa mwili kamili hawakuwa mamilionea ila wakiwa vipandevipande wanaleta utajiri ?

Na iwe iwavyo, ni binadamu gani ambaye leo akiambiwa kuwa apoteze maisha yake ili japo watoto wake wapate utajiri atakuwa tayari; na hilo linakuwaje jepesi kwa wenzetu ?

Utaratibu wa kuwavamia na kuwacharanga kinyama Albino ni unyama ambao hauna lugha nzuri ya kuuelezea ukaeleweka katika uzito wake. Kwanza hawa wenzetu wanao upungufu katika kuzaliwa; kana kwamba hilo halitoshi tunawaongezea janga jingine la kuwaua; hii ni laana ambayo kama hatukuifanyia kazi italiangamiza taifa letu. Tunajisikiaje kusoma habari zao magazetini, kuziona katika TV; kwamba leo mmoja kacharangwa kule, kesho mwingine kauawa huku na tunatikisa miguu kana kwamba tunaangalia mechi ya Simba na Yanga ama Filamu ya King Majuto; hatuoni haya wala hatusikii vibaya. Ipo sinema moja ilikuwa ikionyesha ukatili huo wanaofanyiwa Albino; binasfi sikuweza kuiangalia hadi kufika robo; inatisha.

Ebu kila mtu ajifikilie na yeye angelikuwa Albino; anasikia habari za Albino wenzake wanavyouawa; na yeye anakuwa akitembea akijua wakati wowote atavamiwa na kunyofolewa kiungo chochote; hajui aende wapi akajifiche na kwa nini afanye hivyo; ana makosa gani katika dunia hii. Jamani tumwogope mungu. Kama hiyo ndiyo namna ya kutajirika ebu tufikirie namna nyingine; vinginevyo tukubali kubaki maskini kuliko kuwa matajiri juu ya damu za watu tena watu wenyewe walemavu wa ngozi. Ukiendesha gari la kifahari, ukienda kutalii Dubai, ukila kuku, ukinywa bia; mwenyewe unajisifu kuwa imetokana na mkono au mguu wa Albino. Kama ndivyo wewe ni shetani aliye hai ambaye huna haki na kuchanganyika na binadamu wa kawaida. Na ulaaniwe ufe mapema tena ufe kinywa kikiwa wazi kama ishara ya ubaya ulioutenda duniani kwa hao watakaoihudumia maiti yako.

Kitaifa hii ni vita; na iwe vita ya kila mmoja wetu kuhakikisha kila fununu juu ya vitendo hivi inafanyiwa kazi. Walio karibu na waganguzi wawe makini nao na wazifuatilie nyenendo zao ili kuweza kubaini kama wanahusika na chochote juu ya mauaji haya. Ma Albino tuwalinde popote walipo; tusiwatenge bali tuambatane nao ili angalau wapate imani kuwa jamii ipo nao. EBU KILA MMOJA WETU AFIKIRIE KAMA ANGELIKUWA ALBINO KWA MAISHA HAYA ANGELIJISIKIAJE.