E- MAIL KUTOKA KWA KOMREDI PEE CHOU
Wakati tukiwa katika ziara yetu kuzunguka Kivulini kwetu
tumepokea e mail kutoka kwa rafiki yetu komredi Pee Chou ambayo kutokana na
uzito wa ujumbe uliokuwemo tumeonelea tuuweke wazi ili angalau na wapenzi wa
Kivulini kwetu muweze na nyinyi kupata vionjo vyake.
Ujumbe huu ulikuwa ni wa
kutusalimu na juu ya salamu hizo ulikuwa ukieleza mambo yafuatayo:
1. Ndugu Pee Chou alikuwa akitupa pole
kwa misukosuko ambayo tunakabiliana nayo kwa sasa ya kiuchumi, kijamii na hasahasa kisiasa.
2. Ndugu yetu alikuwa akitutahadharisha
kwa kutueleza kuwa tukiendelea kucheka na manyani basi tujiandae kuvuna mabua.
Alidai huko kwao hawaoni aibu kumzamisha baharia mmoja au nahodha mkorofi ili
mradi kuhakikisha kuwa meli imefika nchi kavu salama iliwa na abiria wengi.
3. Ndugu yetu alituonya sana kuhusu
suala la kuwa wema kupita uwezo. Alitushangaa
sana tunapokuwa waungwana hata
kwa watu wasiokuwa na fadhira wala staha.
Alisema huko kwao wakitaka kumwua
nyani hawamwangalii
usoni.
4. Pee Chou alituonya juu ya imani yetu
kuwa sisi tumebarikiwa na ni nchi teule ambayo haitakuja kuharibika siku
zijazo. Alituasa sana sana tusijidanganye. Amani siku zote hulindwa kwa gharama
zozote kwa sababu siku ikipotea ni kama kudondosha sindano ndogo usiku kwenye
msitu wa nyasi.
5. Ndugu yetu alituonya tusiwaendekeze
watu ambao kwanza hawana hata faida kwa nchi. Aliomba tumjali sana mzalendo na
mpenda nchi na yeyote mpenda fujo na vurugu azomewe na kudhibitiwa mapema kabla
hajaleta madhara katika nchi kwa sababu ujinga wa mtu mmoja unaweza
kuliangamiza taifa zima.
6. Pee Chou alisema kuwa tusisahau kuwa
kitulacho ki nguoni mwetu.
Hayo ndiyo yaliyokuwemo katika e mail hiyo. Sisi wa Kivulini
kwetu hatuna maoni yoyote juu ya e - mail hiyo zaidi ya kumshukuru ndugu yetu Pee
Chou kwa kututumia maoni haya kwa
wakati muafaka.