Monday, 8 February 2016

WANAMUZIKI NA MA-DJ EBU NENDENI NA MATUKIO

Kwa hakika Kivulini kwetu tuna mengi sana ya kuzungumza. Kama mjuavyo sisi ni wanajamii na kila wakati hujaribu kushauri kila panapojitokea mahitaji ya ushauri; yote ikiwa ni kwa lengo la kuboresha mambo.

Ni ukweli usiopingika kuwa kila panapo shughuli muziki huwa ni moja ya vitu muhimu. Waweza kuwa ni muziki toka kwa wanamuziki moja kwa moja au muziki kupitia vyombo mahsusi.

Tuliloliona katika hayo ni kutokuwepo uangalifu wa wafanya muziki katika kuoanisha shughuli husika na muziki unaopigwa na pia kupimia unenguaji na ukatikaji kulingana na hadhara inayohusika.

Unaweza kwenda bar na kukuta nyimbo za kanisani zinapigwa. Unaweza kwenda kwenye kampeni za uchaguzi ukakuta bendi inaimba nyimbo za mapenzi, vijembe ya mitaani au maombolezo mengine ya kijamii. Unaweza kwenda harusini ukakuta wanapiga nyimbo za siasa za chama fulani. Unaweza pia kwenda kwenye mahafali fulani ukakuta hakujapigwa hata wimbo mmoja unagusia elimu. Hii ndiyo hali iliyopo kwa wanamuziki wetu na waandaaji wa shughuli hizo.

Kivulini kwetu tunajiuliza hivi mwanamuziki anayemwimba mpenzi wake katika sherehe au maadhimisho ya kitaifa wakati alipewa taarifa ya miezi kadhaa juu ya shughuli hiyo haoni kuwa ana mapungufu ? Kwanini hakuuliza afahamishwe maudhui ya sherehe ili aweze kuandaa nyimbo au wimbo wa shughuli hiyo.

Na huyu DJ anayetuwekea muziki wa kumsifu kiongozi wa chama cha siasa kwenye harusi yetu ni nani kamwambia kuwa wote walioalikwa ni wa chama hicho na hata kama yanahusiana vipi mambo hayo.

Hivi neno la bwana kuibwa mbele ya walevi wanaofakamia viloba huku wakijifanya kucheza kwa hisia sio matumizi mabaya ya nyimbo hizo. Hata kama wanadai kuwa hao ndio wanaohitajika kukombolewa lakini kweli ?

Jambo hili limekomaa na linakera kiasi chake; sisi tunashauri wanamuziki wakomae sasa na kujitahidi kuoanisha miziki yao na matukio kwani kuna kipindi hasa cha kampeni ilikuwa inafikia mpaka unaombea umeme ukatike au mitambo ikorofishe aache kuimba vituko. Mwanamuziki anajisahau kwa kuimba mambo yake mbele za viongozi na watu wenye heshima zao na hata uchezaji ulikuwa hauendani na hadhara zile; kisa kaalikwa aje kwenye kampeni.

Kivulini kwetu tunawapenmda sana wana muziki na ndiyo maana tunatumia muda wetu kuwashauri kwa sababu tunaamini kuwa aibu yenu ndiyo aibu yetu. 

Tunawashauri mnapokuwa kwenye viwanja vyenu fanyeni mnavyojua lakini muwapo nje kwenye hadhara iliyochanganyika imbeni ya hadhara, vaeni vizuri na chezeni kiungwana mkizingatia kuwa nyie ndiyo kioo cha jamii.
SINEMA ZA KISWAHILI YENYE MAJINA YA KIZUNGU


Kwa mara nyingine tena Kivulini kwetu tumeamua kueleza hisia zetu juu ya utaratibu huu ambao tunadhani una kasoro kubwa ndani yake.

Kwa kipindi kirefu sasa tumeshuhudia wasanii wetu wakifyatua sinema nyingi zenye majina ya kizungu/kiingereza ilhali lugha inayotumika katika kuigiza ni kiswahili.

Tuliwahi siku za nyuma kuhoji juu ya suala hili na majibu yaliyotoka yalikuwa ni sababu za kibiashara; kwamba sinema ikiandikwa jina kwa kiswahili inakuwa haivutii sana kama ambavyo ingeliandikwa kwa lugha aya kigeni. 

Kivulini kwetu hatujatosheka na sababu hiyo kwa sababu wateja wengi wa sinema hizo ni sisi na kama wanaona zinanunuliwa sana wajue si kwa sababu za majina ya kiingereza bali ubora wa picha na sauti na pia uzoefu ambao umekuwepo kwa waigizaji wetu. Najisikia aibu kuona tunajikana wenyewe kwa kuamini kuwa kwa kuchanganya lugha tunakitendea haki kiswahili ama kiingereza.

Pangine tungelichukua mfano wa Nigeria ambapo kuna kipindi sinema zao zilikuwa na soko sana hapa kwetu; sikumbuki kuona wakibadili majina ya sinema zao kuwa ya kiswahili; lakini sisi wapenzi bila kujali hilo tulikuwa walevi wa sinema zao.

Ushauri wetu kwa wasanii wetu kama kweli wanalitaka soko la Ulaya la sinema basi waigize sinema zao kwa lugha ya kizungu na hivyo kuleta mantiki ya kutumia majina ya kizungu na si kuchomekea maneno ambayo nayo huwa ya kama kubahatisha fulani, kuchomekea uzungu ulio nje ya maadili na kuonyesha maisha fulani ambayo hayapo katika jamii yetu.

Yapo mengi ya kusahihisha lakini hili tulidhani lina umuhimu zaidi kushinda hayo mengine ambayo si ya kutisha sana.

Hata hivyo tutakuwa wachoyo wa fadhila kutowapongeza waigizaji wetu kwa juhudi wanazofanya angalau sasa hivi kazi zao zina ubora. Ila wasikimbilie sana kutoa sinema zenye maandalizi hafifu ili kubakiza imani kwa wateja kuwa kazi zao zi la kulipua. Wasirekodi sinema kwa mapenzi yao bali warekodi kwa mapenzi yetu kwani mwisho wa siku sisi ndio tutakaozinunua na kuzitazama sinema hizo. Wasikusanye mashangazi, majirani na marafiki ili nao wauze sura; wakumbuke hiyo ni kazi na inahitaji kuheshimiwa.