ACHENI KUTUSINGIZIA
Kivulini kwetu jana tulikutana kujadiliana juu ya upuuzi huu ambao umekuwa kila siku ukifanywa na wanasiasa uchwara na wanaharakati njaa kuwa kila waliwazalo wao hushindwa kuliwasilisha kama mawazo yao na kusingizia kuwa ni matakwa ama mawazo ya wananchi.
Nasema tulijadili kwa pamoja tukaamua kutoa tamko kuwa tuwapashe na kuwaeleza wazi kuwa waache kabisa kama sio kukoma kudumisha harakati zao juu ya vichwa vyetu.
Kwa hali ilivyo sasa jamaa hawa ni vema wakajua kuwa kuna kila fulsa na kila nyenzo za kumwezesha kila mwananchi kuwasilisha mawazo yake popote na wakati wowote juu ya nini anawaza, nini anahitaji na kipi hakitaki. wananchi wa sasa wamesoma na wana upeo wa kufikiri na uwezo mkubwa wa kuzungumza. Wananchi wa sasa si watu wa kusemewa na si mbumbumbu kiasi cha kila siku kusingiziwa kuwa wanataka hili ama wanataka lile. Kama wazo lako ni jema au zuri kwanini usiliseme kama wewe na badala yake unatafuta uzito kwa kusingizia kuwa ni wazo la wananchi, walikutuma lini ?
Inaudhi sana kumkuta mtu mzima na masharubu yake kasimama jukwaani anatoka mapovu akijidai anawasilisha maoni ya wananchi; yeye kama nani awasemee watu na anaowasemea wako wapi. Na katika udhaifu, na uvumilivu walionao wananchi hawamkemei wala kumzomea; wanamsikiliza kwa matumaini kuwa pengine atakuwa na jipya la kuwaeleza; mpaka muda unakwisha wanabaini kuwa alichongea ni pumba tupu toka mwanzo hadi mwisho.
Mwanzoni baadhi ya majimbo tulikuwa tukiwasilishiwa mawazo yetu na wabunge bungeni; imefikia sasa mbunge wengi hakanyagi kabisa majimboni na wala hawana mawasiliano na wapiga kura wao, lakini mbunge huyohuyo akifika bungeni anaongea kama kasuku mambo na mawazo aliyoongea na mkewe kwa kuyafanya ndiyo mawazo ya wananchi; toka lini mke wako akawa ndiyo wananchi. Acheni mambo yenu.
Ukitaka jaribu kuyafuatilia anayoyasema; utakuta ni mambo tofauti ya jinsi ilivyo katika jimbo lake. Kwa wale ambao wanawasiliana na wapiga kura wao ni sahihi kuwasemea kwani walitumwa; lakini hao wengine ambao nawasema leo ambao siku hadi siku wanaongezeka idadi kwa kweli ni kero tupu na wanayatia aibu majimbo yao.
Na hao ambao kila uchao huitisha mikutano na waandishi wa habari wakidai wanatoa hoja za wananchi ama wanadai haki za wananchi, hivi ni wapi wanakaa na wananchi tunawaeleza kuwa hivyo ndivyo tunavyotaka. Utasikia wananchi hawataki hiki ama wanataka kile; cha ajabu haohao tena wanadai kuwa tutawahamasisha wananchi wasikubali ama wakubali; kama ni kweli wanachosema ni mawazo yetu iweje waje tena kutuhamasisha tukubali ama tukatae; si watuache tu tutakubali au kukataa wenyewe kwa wakati wetu; waokoe muda wautumie kulea watoto wao. Kinachoonekana sasa ni watu kutumia vyama na taasisi kuomba chochote kwa wajomba zao kwa kusingizia kuwa wanakuja kutusaidia wananchi kumbe wezi wakubwa. Tumewachoka wezi hawa na ipo siku tutawapiga mawe wakija kivulini kwetu. Harakati hizo na siasa hizo tumezichoka. Mambo ya kujenga magorofa juu ya vichwa vyetu tumeyastukia; kila siku nyinyi tu ndio mnaojua mawazo yetu nyie mawazo yenu anayajua nani; ebu oneni haya msidhani hatujui ujanja wenu na vitaasisi vyenu feki.
Monday, 13 October 2014
Tuesday, 7 October 2014
SUALA LA UCHAFU
Kivulini kwetu safari hii tunataka kuongelea suala la uchafu
katika mji wetu. Suala hili limekuwa kama tabia na inaelekea tabia hii
inaimarika sana na kuwa utamaduni wa jamii yetu.
Kama tujuavyo uchafu ni takataka; lakini pia uchafu ni hali ya
kutokuwa msafi. Uchafu pia inaweza kuwa tabia ya mtu au watu kutokuwa wasafi.
Wakati tukitathmini uchafu kuna namna nyingi ya mtu au watu
kutokuwa wasafi.
Namna ya kwanza ambayo ni rahisi kuelezeka ni tabia ya watu
kutoona kinyaa kukaa katika mazingira yenye takataka kama vile masalia ya
matunda, matambara, makaratasi na kadharika. Lakini pia kukaa mahali penye
uvundo ama panapotiririka maji machafu, kwenye mifereji michafu na kadharika.
Uchafu mwingine ni tabia ya kutotunza mazingira kwa kutupa
taka ovyo, kula ovyo, kuvaa ovyo na kadharika.
Uchafu mwingine ni kutokuwa na mpangilio mzuri wa vitu hata
kama vitu hivyo ni visafi. Mfano katika mji ni kuegesha magari ovyo, kupanga
bidhaa ovyo hadi barabarani, ujenzi holela, migongamano isiyo ya lazima,
kufanya shughuli zozote mahali pasipostahili kama kupika sehemu za wazi, kulala
kwenye mavaranda, kuosha magari barabarani, gereji kwenye makazi ya watu, vituo
vya mafuta kwenye makazi ya watu, viwanda vya jua kali mahali pasipostahili na
mengine mengi ya aina hiyo
.
Baada ya kufuatilia kwa karibu tumegundua kuwa chanzo cha
hali hii ni mamlaka husika za mji kutowajibika katika kusimamia sheria na
taratibu za mji. Aidha si kutosimamia tu bali kutokuwa na mipango au utaratibu
endelevu katika kuuweka mji namna unavyopasa kuwa.
Mamlaka zimeshindwa kutoka maelekezo fasaha na kwa wakati
juu ya kipi kifanyike, wapi kifanyike, nani afanye na afanye wakati gani. Na
juu ya hayo kueleza wazi kuwa atakayekiuka maelekezo hayoatafanywa nini na
kweli inapotokea mtu kakiuka basi hatua zichukuliwe.
Kinachojitokeza ni kusimamia machache baadhi na kusimamia
kwake ni kinyume na inavyotakiwa; kwamba upo upendeleo kwa baadhi ya watu, kwa
baadhi ya maeneo na baadhi tu na masuala yote yanayotakiwa kusimamiwa. Matokeo
ya kufanya hivi ni jamii nzima kuachwa njiapanda watu wasijue ni kipi sahihi
kufanyika na nani anapaswa kufanya kwani katika eneo moja, watu wa aina moja,
katika muda unaofanana; wapo wanaoruhusiwa kufanya na wapo wanaozuiwa kufanya
kitu kilekile, mahali palepale na katika muda uleule.
Chanzo kingine cha uchafu ni tabia ya mtu mmoja mmoja ya
uchafu. Hii inatokana aidha na malezi, ukosefu wa elimu, umaskini na mlengo wa
kushoto wa mawazo.
Kitendo cha mtu kula matunda na kutupa maganda barabarani,
kitendo cha mtu kunywa maji au soda na kutupa chupa katika mfereji, tabia ya
mtu kuuza bidhaa zake dukani na makasha, maboksi, na vifungio vingine ovyo
mbele ya duka lake, vitendo vya watu kujisaidia haja kuwa na ndogo katika
mifereji ya majitaka wakati mwingine mchana kweupe, vitendo vya kupanga bidhaa
za chakula juu ya maji yanayotiririka na kuwauzia watu na hata wao pia kununua;
lakini mbaya zaidi kitendo cha kuona haya yote yanafanyika na kuacha kuyakemea;
yate haya yanajumuika katika tabia ya uchafu. Watu wamekuwa hawaoni vibaya juu
ya masuala haya na imekuwa ni kawaida.
Hujitokeza kuacha kwa muda pindi
wanapotangaziwa na mamlaka waache kutokana pengine na milipuko ya magonjwa ama
kuwe na ugeni unakuja Kivulini kwetu. Katika harakati hizo za kuzuia uchafu
watu hulalamika sana kuwa wanaonewa na kunyanyaswa katika nchi yao kwa kuambiwa
waachane na uchafu. Baada ya milipuko na ugeni kuondoka hali ya uchafu hurejea
mahali pake. Kwa hakika inasikitisha sana.
Binafsi nilidhani ipo haja kwanza ya jamii ambamo na wenye
mamlaka wanatoka humo ibadilike na kuchukia mazingira machafu. Tuwe jamii yenye
kuona kinyaa kukaa kwenye majalala,
kutupa taka ovyo, kujisaidia ovyoovyo, kununua vitu vichafu, kuvaa mavazi
machafu, sisi wenyewe kutokuwa wachafu; kwa sababu nakumbuka kuna siku alipanda
mtu mmoja kwenye daladala(simtaji jina, siitaji jinsia yake, dini yake wala
kabila japo niliulizia na vyote nikaambiwa) kila abiria ilibidi afunge pua;
lakini hiyo haikutosha wakaomba mtu huyo ashushwe vinginevyo wao washuke;
ikabidi ashushwe kituo kinachofuata; kwani kwa jinsi alivyokuwa ananuka ni
afadhari ya kinyesi; unaweza kupata hiyo picha kuwa mtu huyu anatoka wapi na
amewakera watu kiasi gani katika maeneo yote aliyopita. Mtu kama huyu kuna
uchafu gani utakaomtisha akaogopa ?
Lakini juu ya jamii kujirekebisha, mamlaka nazo ziweke
utaratibu mzuri wa kufuatwa. Kuwe na sheria za kufuatwa ili kuweka mji katika
usafi. Taratibu zizuie baadhi ya mambo yanayosababisha uchafu kufanyika na
taratibu hizo zisimamiwe bila ya ubaguzi wala upendeleo na usimamizi huo uwe
endelevu na sio zima moto.
Ninasali ije itokee kipindi na sisi tukawa wasafi, katika
mji safi wenye kupendeza.
Subscribe to:
Posts (Atom)