Thursday, 31 July 2014



MAMBO YA KIVULINI

Kama ilivyo ada; penye wema  ubaya huwa haukai mbali. Vivyo hivyo na kivulini, daima huwa hapakosi matatizo. Kwanza kabisa unapokuwa kivulini lazima ujiandae na kuhama au kusogeasogea; kwani kivuli mara nyingi hutegemea jua. Tangu kuchomoza jua hadi kuchwa kivuli hutembea au kusogea eneo jipya.
Jambo jingine ni kuwa kama wewe mwanadamu upendavyo kivuli na viumbe wengine nao hupenda kivuli. Kivulini waweza kutembelewa na wadudu ama nyoka ambao huwa hawaji kwa ajili yako, bali hufuata kivuli waweze kujipumzisha pia. Na si hao tu wanaweza pia kuja wanyama kama simba chui, nyani na wengineo kutegemea kivuli hicho kiko wapi.
Nasikia pia kivulini waweza tenmbelewa na viumbe wa ajabu kama majini, mizimu na wengine wa aina hiyo ambao hupendelea sehemu tulivu ama hutafuta watu watulivu. Iwe iwavyo kivulini ni mahali penye faraja ili mradi uwapo kivulini kuwa na tahadhari; lolote linaweza kutokea.

Monday, 28 July 2014

FAIDA YA KIVULINI

Siku zote ukitaka kujua faida ya kivulini ni vema mwenyewe ukaenda kivulini ukajionee mwenyewe. Kwa kusimuliwa wakati mwingine unaweza kudanganywa ama ukaelezwa ukweli na ambaye ana mtazamo tofauti na wako. Kwa mfano, azengewaye na homa; kivulini hupachukia kwani hujisikia baridi. Mchovu hujisikia usingizi na mwenye vibichi kivuli humchelewesha kukausha. Iwe iwavyo kivulini ni patulivu na humliwaza mwenye kuhitaji kuliwazwa; mwenye lake jambo kivulini hupakimbia.