Saturday, 16 January 2016


CHONDE SIASA ISITUTAWALE

Kivulini kwetu baada ya kuridhika kuwa kwa hali ilivyo tunaweza tukatupia neno japo moja tumeamua kufanya hivyo.

Tumeamua kuongea ili kuwaasa ndugu na jamaa zetu wajitahidi kutawala mambo yao badala ya mambo yao kuwatawala. Tuutawale ulevi na ulevi usitutawale. Tutawale lugha yetu na lugha isitutawale. Tutawale furaha yetu na furaha isitutawale. Tuutawale uhuru wetu na uhuru usitutawale. Yapo mengi katika maisha yetu ambayo ni busara sisi kuyatawala na kamwe tusiache yatutawale.

Moja ya mambo ambayo tulipenda kuyaongelea leo ni kushauri tuitawale siasa na tusiache siasa itutawale.

Tumeanza na siasa kwa sababu sasa hivi imekuwa kero; maisha yetu yamezingira na siasa kiasi kwamba tumekuwa walevi wa siasa. Siku hizi watu wanaamini kuwa mtu anaweza kutembea ki-UKAWA; anaweza kuongea ki- CCM; anaweza kula ki-CUF na kadharika. Tumefika mahala hatujiwezi mbele ya siasa; siasa imetutawala badala ya sisi kuitawala.

Yote tunayoyafanya sasa yalikuwa yakifanyika toka zamani; lakini sasa hivi tumenasa. Kila tendo limekuwa na tafsiri ya siasa. 

Zamani makabila yalikuwa yakitaniana; wachaga kwa wapare; wasukuma kwa wazaramo; wahehe kwa wangoni; wahaya kwa wakurya; ilikuwa ni kawaida sana. Walikuwa wenyewe wanajua mwanzo wa mipaka ya utani wao na mwisho wa mipaka hiyo na maisha yalikuwa yanakwenda murua kabisa.

Inashangaza ni shetani gani kaingia kiasi kwamba sasa hivi Mkwere akimtania Mnyamwezi anadaiwa anamdhalilisha; au Mgogo akimdhihaki Mrangi anakuwa kafanya kosa. Na bora basi hasira hizi zingekuwa za kawaida; sasa hivi zinaingizwa katika siasa na vyama.

Hapo nyuma kulikuwa na utani wa makabila, utani wa kuhusiana, na utani wa utaifa. Ilikuwa hushangai ukimkuta Mmakonde anasifu ubahili wa Mpare au mchaga anamsifia mnyamwezi kwamba anastahili kupewa mizigo mizito "mzigo mzito mpe Mnyamwezi"; ama Mchaga alipokuwa akisifiwa kwa kupenda pesa;  wao wahusika wa sifa hizo walilijua hilo na kwa kiasi walijisikia fahari na utani huo.

Sasa tunauliza huyo shetani ambaye anahusisha makabila na vyama katoka wapi. Nani anayetaka kuwaaminisha watu kuwa Wachaga wote ni UKAWA, Wapemba wote ni CUF, Waha wote ni ACT au Wafipa wote ni CCM kiasi kwamba wakitaniwa vinakuwa vyama vyao vimedhalilishwa.

Kuna watu wamekazana sana na biashara hiyo kiasi kwamba wanataka sasa siasa itutawale na itutoe katika tamaduni zetu na mahusianmo yetu ya asili na kutufanya tuanze kuogopana. Tusikubali.

Kivulini kwetu tulidhani tuanze mwaka kwa kulikemea jambo  hili kwani bila ya kufanya hivyo hawa jamaa ambao kwa kigezo cha kutetea udhalilishaji wa makabila wanapandikiza chuki na kuchonganisha makabila kwa minajili ya kukonga nyoyo zao kisiasa. Tukatae kutawaliwa na siasa.

Yapo mambo ambayo tukiyafanya yana manufaa lakini hili la upotoshaji wa mila zetu kamwe hazitatufikisha popote. Ni vizuri tukapuuza tafsiri hizi na kupambana tubaki katika mstari wetu wa mahusiano.

Wednesday, 13 January 2016



 HERI YA MWAKA MPYA

Ndugu wapendwa wa Kivulini kwetu Blog tunayo furaha kuwafahamisha kuwakaribisha tena kuendelea na maongezi yetu Kivulini baada ya kupoteana kwa muda mrefu kidogo.

Awali ya yote tungependa kuwamwagia salamu nyingi za mwaka mpya wa 2016 tukiwa na inani kuwa mtakuwa hamjambo na mnaendelea vema na shughuli zenu za kila siku.

Kwa kuwa leo tulikuwa tunawaalika tu katika Blog hii tusingependa kuwachosha na maelezo ya nini ilikuwa sababu ya kupoteana; tunadhani mnachokihitaji zaidi ni huduma.

Tutaendelea kupashana na kutaarifiana mwenendo mzima kuhusiana na Blog yetu.

Tnachukua fulsa hii kuwaahidi mema kwa mwaka huu wa 2016. Tunawakaribisha wote.

Asanteni sana.