TUSIENDEKEZE UTAMADUNI WA MIGOMO
Kivulini kwetu kwa kipindi kirefu tulikuwa tumesimama kukutana chini ya mti wetu kutokana na hali ya hewa ya mvua na kwamba chini ya mti wetu kulikuwa na tope na unyevu hivyo tulikuwa tunasubiri hali iwe shwari.
Wakati tukiwa katika subira kuna mambo kadhaa yalitokea ambayo kwa hakika mara hali iliporejea kuwa nzuri tulianza nayo katika mijadala yetu.
Moja ya mambo ambayo tulidhani ni muhimu tukaeleweshana ni suala la migomo.
Ni kweli kuwa nchi yetu ni nchi ya demokrasia tena ya vyama vingi. Ni nchi inayoamini katika utawala bora. Ni nchi inayojali haki za binadamu. Ni nchi ambayo inajitahidi sana katika kukwepa udikteta na kuamini kila mtu kujieleza na kudai haki yake kwa kadri ya uwezo wake; wakati mwingine hata kama haki hiyo haipo; mtu ashindwe mwenyewe.
Haki ya mtu kugoma siyo mjadala mkubwa kwetu; mjadala kwetu ni matokeo ya migomo hiyo na namna migomo hiyo inavyochukuliwa.
Tuchukue mfano walipogoma wafanya biashara kufungua maduka wakilalamikia mashine za kukatia risiti. Kwa kuwa ni watu wazima wenye akili timamu tunaamini kabisa walikuwa wanajua wanachokidai. Lakini walipofunga maduka yao nchi ilikosa makusanyo ya mapato kwa siku zote walizogoma. Mapato hayo kwa hesabu zake lazima yalikuwa makubwa na yangeweza kutupa huduma nyingi sisi wananchi wa nchi hii ambamo na wao wamo. Hatukuelezwa ni hasara ya kiasi gani ilipatikana, pengine akina sisi tungelikasirika zaidi. Madai ya mgomo huo yalikuwa ni ya muda mrefu na kama yangelijadiliwa na kupatiwa ufumbuzi; ufumbuzi ambao umekuja kupatikana baada ya mgomo; hasara hiyo isingelipatikana.
Hasara nyingine ni ya usumbufu kwa wananchi ambao walikuwa wanahitaji kununua aidha vyakula au vifaa mbalimbali kwa ajili ya kazi zao. Wengine walikuwa wametoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya kufanya manunuzi. Wote hawa mbali na usumbufu wapo walioingia gharama kutokana na maduka hayo kufungwa. Gharama hizo hawana wa kumdai.
Mfano mwingine ni mgomo wa madereva. Hawa waligomea kusomeshwa tena kusomeshwa kwa gharama kubwa waliyodai iko nje ya uwezo wao. Waligomea pia kufanyishwa kazi bila ya mikataba na malipo madogo na mapungufu mengi katika ajira zao. Hili nalo lilikuwa linaweza kuzungumzwa na wahusika na kufikia makubaliano ambayo yalikuja kufikiwa baada ya mgomo. Kilichotokea wakati wa mgomo huo ni usumbufu kwa watu chungu nzima.
Sijagusia mgomo wa wenye magari ya usafirishaji, migomo bubu ya kufunga barabara ambayo sasa hivi imeshamiri; usilogwe sasa hivi kumgonga japo mbwa wa mtu; kesho utakuta mawe yamepangwa barabarani wahusika wakidai hiki ama kile.
Kivulini kwetu tunasema kuwa kila kunapotokea migomo huwa wanaoathirika zaidi ni watu ambao hawahusiki kabisa na chanzo cha migomo hiyo wala hawana maamuzi yoyoye juu ya utoaji wa hayo yanayogomewa. Na pindi wanapopata hasara iwe ya gharama yoyote huwa hawana wa kuwafidia na wakati mwingine huwa hata radhi hawaombwi. Hii kwa kweli si haki. Kama waliogonma walikuwa wakidai stahiki zao; iweje hawa nao walioathirika na migomo bila kuhusika na lolote wawe hawana haki yoyote.
Kivulini kwetu tulikuwa tunaiomba jamii yetu itafakari upya juu ya utaratibu huu wa kudai haki kwa kukiuka haki za wengine. Mwingine kumwaga damu kwa ajili ya kutetea damu ya mwingine bila makubaliano yoyote.
Kivulini kwetu pia tulikuwa tunaiomba jamii ielewe kuwa wasije wakadhani makundi mengine yameridhika na hali zao; kilichopo ni kuwa makundi mengine yanafanya ustaarabu kwa kutiojiingiza katika kero ya kuwakera wengine ili kupata haki zao.
Kivulini kwetu tulikuwa tunawaomba wote waliogoma na wenye nia ya kugoma wakumbuke kuwa endapo kila mtu atagoma kwa wakati wake ili kudai chake, ipo migomo ambayo itagharimu maisha ya wengi. Kumbukeni walipogoma madaktari hali ilikuwaje; kumbukeni walipogoma walimu hali ilikuwaje; kumbukeni walipogoma wanafunzi wavyuo vikuu hali ilikuwaje.
Kivulini kwetu tunaamini kwamba ni wajibu wetu kuelimishana na kuwekana sawa kwa sababu kila mtu anayo haki yake kama aliyonayo mwenzake. Kuwepo na utulivu haina maana ya wasiogoma kuridhika na kila kitu bali ni ustaarabu wa kuamia kutumia busara katika watu kupata mahitaji yao na kudsai haki zao bila ya kuwasababishia wengine usumbufu vinginevyo kila mtu akiingia mtaani kudai chake hatutakuwa na nchi kama ilivyo sasa bali uwanja wa mauti.