Tuesday, 12 August 2014

BARUA TOKA KIVULINI



      MAJIBU TOKA KIVULINI

Kwako Mtani wangu,

Thesuperonenews.blogspot.com(Dassan)


WATU NA TABIA

Nieisoma mada yako vizuri sana. Japo nimeipenda lakini sikuridhika na maoni yako. Umejitahidi kukwepa lawama ili usilaumiwe na makabila husika. Ukweli ni kuwa maoni uliyoyasikia toka kwa watu mbalimbali juu ya tabia za makabila ndiyo ukweli ulivyo. Kwa bahati mbaya hujafanya utafiti juu ya jambo hilo. Mimi kwa kiasi nimejaribu na maoni niliyoyapata kwa bahati nzuri yalitolewa na watu wa makabila husika ambao hawakutaka kujipendelea. Ni ukweli usiopingika kuwa pamoja na tabia kuwa ya mtu binafsi, zipo tabia ambazo zinaambatana na ukabila. Na hii inatokana na mila na malezi ya makabila hayo. 

Uchoyo kwa mpare siyo jambo la siri.



 Ufundi wa mapenzi kwa mtoto wa kitanga si ajabu. 






Majivuno kwa mhaya sio siri.




 Hasira kwa mhehe si ajabu.




 Ulimbukeni kwa mgogo ni kitu cha kawaida.




 Juju kwa mrangi na mfipa ni kawaida.


  Ukarimu kwa mnyamwezi hauna ubishi. 


Michepuko kwa mngoni ni kama jadi.

 
 Ukorofi kwa mkurya hauna mjadala.


 Umbeya kwa mzaramo ni sifa.


Huruma kwa wayao haina mipaka.


  Mikato kwa wanyakyuka haina maswali ni maji mara moja:


kwamba kila kabila lina sifa zake kuu. Huwezi kuyajua haya mpaka utembee na ujichanganye  sana. Lakini katika hali ya kawaida ukiwaeleza wenyewe lazima watakunja ngumi hata mimi pamoja na kujua nitajifanya sihusiki; ila ukweli unabaki palepale kuwa makabila hayafanani na watu ni wa makabila. Huwezi kusema mzungu na mswahili ni sawasawa tunapokuja kwenye tabia. Ila wazungu wanaweza kufanana na waswahili nao kufanana.


Wakatabahu,


MWENYEKITI WA KIVULINI

DIJITALI KIVULINI

         KERO ZA SIMU

Leo Kivulini kuliletwa mada. Mada hii ilikuwa nzito na nyeti. Mada hii ilihusu masuala ya utandawazi hususani mambo ya mitandao. Mada hii zaidi ilikuwa ni malalamiko juu ya athari ya kizazi hiki cha "Digital" kwamba kama ni kuugua basi gonjwa hili la mtandao linazidi gonjwa la ukimwi; wengine wakadiriki kupendekeza kuwa litangazwe kuwa ni janga la kitaifa.

Wadau walilalamka kuwa suala la simu limekuwa ni kero badala la kuwa heri. Kutokana na wazungu kutuelewa vizuri vipaji vyetu vya kuwasiliana wametumwagia masimu kama vile mchanga wa bahari. Sasa hivi wasio na simu wamekuwa wachache kushinda wasio na macho. Bei ya simu imekuwa karibu na bure hivyo kumkuta mtu ana simu zaidi ya tatu zake mwenyewe wala sio ajabu.

Kana kwamba hiyo haitoshi; makampuni ya simu yameweka fulsa kibao. Kuna maeksitrimu, ma minikabangi, kabangi,  Burudika, Cheka zogo, shangwe, nipige tafu, mpaka kuna yatosha na mengine kemkem. Sasa kazi iko katika matumizi. Utakuta watu wamejiunga wanaongea kwa zaidi ya masaa manne. Fikiria mtu wa aina hiyo kwa kipindi chote anachoongea ni mambo mangapi yanalala. Sasa hivi mwanafunzi yuko darasani ana simu anadai anachati. Basi mwalimu atafundisha mpaka atakoma kumbe wenzake hawana habari na yeye wanawasiliana na mashoga zao wa dunuani.

Ngoma nyingine iko kwa akina mama. Mboga zinaungua, watoto wanashinda njaa; kisa mama anafanya fesibuku.

Ukienda maofisini ndiyo balaa zaidi maana tangu meneja mpaka mhuhumu wote wanagugo. Huhudumiwi wala husikilizwi mpaka wenyewe waishiwe na vifurushi kwenye simu ndipo wasituke kuwa upo na una shida.

Sasa kwa hali hiyo piga hesabu ni wangapi kwa saa na katika nchi wanafanya hivyo na uchumi ama maendeleo ya nchi yaaathirika vipi; hayo ndiyo yaliyokuwa yakijadiliwa Kivulini.

Mada hii ilikuwa ndefu na maongezi yake yalikuwa moto sana kiasi kivulini palikuwa hapakaliki. Ili wasikilizaji wangu muweze kupata picha kamili nitawatumia mjadala mzima kutumia intagramu na twita ili nanyi mtoe maoni yenu ama hata kulaiki tu itatosha.

Monday, 11 August 2014

BANGO KIVULINI

             SIRI YA KAZI

Leo asubuhi tumekuta bango kivulini kwetu. Hatujui aliyeliweka; lakini lina maandishi makuwa yasemayo:


SIRI YA KAZI

"UKIIONA KAZI, KWANZA IOGOPE NA IHESHIMU; KWA SABABU ILIANZA KUMSHINDA MWENYE KAZI NDIPO AKAAMUA KUMTAFUTA MFANYAKAZI AIFANYE TENA KWA MAKUBALIANO YA MALIPO MAALUM; ANGELIIFANYA MWENYEWE MWENYE KAZI LEO HII DUNIANI KUSINGELIKUWA NA MFANYAKAZI"

KIVULINI KUNA MENGI

            ZIARA YA MHESHIMIWA


Wiki jana tulitebelewa na Mh. Mbunge wetu. Pamoja na kuwa kivulini kwetu sio uwanja wa siasa  lakini kwa mujibu wa Katiba ya nchi hatuna mamlaka ya kuwapiga marufuku wanasiasa kuja kivulini na kufanya walitakalo ili mradi hawavunji sheria.

Baada ya Mh. Mbunge kujitambulisha kwetu tulilazimika kumsikiliza ujumbe wake. Naye kwa kujiamini kabisa akasema:

" Ndugu wapigakura wangu, waheshimiwa wananchi; nimepata malalamiko yenu ya kwamba tangu mnichague sijawahi kuja japo kuwapa shukrani kiasi kwamba mpaka uchaguzi mwingine unakuja baadhi yenu hata sura yangu  mmeisahau. Kwa hilo sikatai. Kama mjuavyo; jimbo langu lina vivuli vingi sana kiasi nimeomba katika Bunge la mwaka huu jimbo ligawanywe mara mbili ili niweze angalau kwa kutembelea kivuli kimoja kila siku nimudu kumaliza vivuli vyote katika msimu mmoja wa uongozi wangu. Vinginevyo katika Bunge hili la Katiba mpya nipendekeze kipindi kimoja cha ubunge kiwe ni kwa miaka kumi."

"Jambo jingine ambalo ningeliomba mnielewe ni kuwa na mimi ni MwanaUkawa. Kimahesabu kwa kuwa mimi ni mbunge wenu 'automatically' na nyinyi wapiga kura wangu wote ni WanaUkawa. Nadhani tunakubaliana na msemo wa  "ukipenda boga basi penda na maua yake". Kusema hivyo ina maana sisi wa jimbo hili serikali zetu ni tatu; kwa hilo sina wasiwasi na nyinyi wananchi wangu na msikubali kuyumbishwa na wanasiasa  uchwara na vijisera vyao vya majitaka."

"Kitu kingine ni kuwa nilitaka niwadokeze kidogo tu kuwa ninatarajia kuwania Urais wa nchi lakini kutokana na taratibu za chama chetu hiyo tuiache kwanza iwe ni siri yenu msimwambie mtu;  lakini kama alivyosema Kikwete akili za kuambiwa basi changanyeni na zenu mtajua pumba ni zipi na mchele ni upi"

La mwisho, nilikuwa nimewaandalia kajilunch kadogo kwenye ukumbi wetu wa Kivulini. Nendeni mkale mshibe bila ya wasiwasi kwani usafiri upo; kuna kijinauli kwa kila mtu, Mtendaji atawapa bahasha zenu."

"Kwa kuwa muda umebana sana kwa leo taarifa ya utekelezaji wa sera ya kivulini na ya maendeleo sitaitoa; tuombe mungu kura zitoshe katika uchaguzi mkuu ujao kwenye kikao kama hiki tutaelezana nini kimefanyika katika vipindi vyote sita vya ubunge wangu. Tanzanyika oyee "

Kabla hatujamhoji chochote akapeana mikono na aliokuja nao aatuacha tumeduwaa kivulini, akidai amasubiriwa na vivuli vingine.

Friday, 1 August 2014


NGANO ZA KIVULINI


     MAKUBWA KIVULINI

Siku moja majirani tulikuwa kivulini tunapunga upepo huku tukiwa na maongezi ya hapa na pale. Tulikuwa watano; wanawake wawili na wanaume watatu. Tukiwa hatuna hili wala lile akaja mzee mmoja naye jirani yetu vilevile. Akatusalimu na kasha anaanzisha mada mpya kabisa. Akasema, hebu tuwe wakweli na kila mmoja atoe mchango wake kwa moyo wote; mmoja mmoja kila mtu aseme anawaza nini hapo alipo; nini tatizo lake kubwa ambalo linamla akili. Kwanza tulitazamana, tukacheka na baadae mmoja wetu kwa jina bwana Juma Kilobaki akaanza kijieleza:

JUMA KILOBAKI:  “Ndugu zangu, kusema kweli mimi ninalowaza ni kuwa nitajikomboaje katika hii hali. Kwanza, mwanangu jana karudishwa kutoka shuleni anadaiwa ada sh.300,000/=. Pili, nimeletewa taarifa kutoka nyumbani kuwa mama mzazi kalazwa hospitali; hana damu, figo moja haifanyi kazi, na mapafu yamejaa maji; kwenda tu kumuona lazima niwe na 250,000. Tatu,nilikuwa nimekopa Benki ya Posta kwa kila mwezi kurejesha sh. 180,000/= na tarehe ya marejesho ilikuwa juzi. Nne, nimepata simu muda sio mrefu kuwa mama mkwe yuko njiani anakuja kutusalimia; yeye na wajukuu zake wawili; lakini hapa nilipo senti tano kipande sina…..!”

Tulikuwa kama tumekubaliana; wote tukasema “…du !”. Wa pili nikawa mimi……nikaanza “ Jana nililetewa taarifa kuwa kuwa watoto wa mjomba(mtu na dada yake) wamepeana mimba. Mjomba mwenyewe amekwisha pata habari juu ya suala hilo lakini yupo safari; kesho anarudi. Keshatoa maagizo kuwa asiwakute watoto hao nyumbani kwake. Mkewe kaja nyumbani analia nimsaidie. Sasa ninawaza nianzeje.”

Ikaja zamu ya Mama Sakina; yeye akaanza lake “…jamani mwenzeni nina tatizo. Mkilisikia mnaweza kudhani dogo lakini……leo ni karibu mwezi lakini amini usiamini kila siku ya mungu nikilala usiku ninamuota mume wa jirani yangu nimelala nae. Yaani ndoto hiyo imenichosha maana nikiamka nikilala tena ndoto ni hiyohiyo…sijajua nimelogwa, ama nina jinni ama vipi…..sielewi kwa kweli”

Aliyefuata alikuwa Eliza. Yeye nae alikuwa na lake. “Mwenzenu mimi tatizo langu  ni ndoa. Kila saa nawaza huu ni mwaka wa 35 lakini haijatokea hata katika utani mwanamume yoyote kunitamkia ndoa. Na si ndoa tu hata kuniambia chochote kwamba ananipenda au nini. Nikijiangalia mwenyewe sijoni kama nina kasoro sasa hii hali mpaka lini. Msinione ninacheka mkadhani vipi mwenzenu inaniuma kwelikweli sina hata raha na maisha” Kila mmoja wetu akabaki ameduwaa.

Wa mwisho alikiwa Dick Mbalanga. “ Mwenzenu mimi nasumbuliwa na mke wangu, siyo siri kwa kweli atanishinda. Huu sasa nikihama utakuwa mtaa wa tisa ndani ya mwaka mmoja. Mtaa wa kwanza alimpiga baba mwenye nyumba. Mtaa wa pili alifumaniwa na mume wa jirani yetu. Mtaa wa tatu alikutwa anafukia hirizi mlangoni kwa mwenye nyumba. Mtaa wanne nikiwa safari alikamata bata wa watu akamkaanga wakati mimi niliposafiri nilimwachia hela kibao za matumizi. Mtaa wa tano amekula hela za watu za upatu. Mtaa wa sita kamchoma kisu binti mmoja jirani, kisa, anamshuku kuwa mimi ninatembea nae. Mtaa wa saba aligombana na mama mwenye nyumba akachukua mafuta na kiberiti kutaka kuchoma nyumba. Mtaa wa nane ilibidi nihame maana alikuwa anatembea na mpemba mmoja ayelikuwa na duka lake nyumba hiyohiyo. Sasa juzi mke wangu kagombana na wapangaji wenzie akawatishia maisha na wenzake wamemwambia watamfanyizia…….mkumbuke huko kote hatukukaa tukamaliza mwaka, tulikuwa tunahama tunasamehe kodi miezi iliyobaki.”

Yule jamaa aliyetuhoji akatuangalia kingano za kivulnsha akasema “….mnaona ndugu zangu, kipindi mnaongea mliyajua haya ?; kazi kwenu mimi siyawezi labda kivuli kitawasaidia. Akaondoka na kutuacha midomo wazi kivulini.