Friday, 19 September 2014





       TAARIFA YA KUREJEA KUTOKA SAFARI




Baada ya kupotea kwa karibu viki tatu, kikosi kazi cha Kivulini kwetu kimerejea tena ulingoni kuendelea na kuwapatia taarifa mbalimbali za siku hadi siku kwa malengo yale yale ya kuwaelimisha kuwahabarisha na kuwaburudisha ili wanachama wetu na wapenzi muweze kupata kile ambacho roho zenu zinataka.

Kwa kipindi chote hicho ambacho hatukuwa hewani, tulikuwa katika ziara ndefu ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Kivulini kwetu ili kujionea jinsi maisha ya jamii yetu yanavyokwenda. Katika ziara hii tumeona mengi ambayo kwa faida ya jamii yetu tutakuwa tukiwapasha moja baada ya jingine. Tunaomba ushirikiano wenu.

Wednesday, 3 September 2014



           FACEBOOK

Leo Kivulini kwetu tulikuwa na mjadala kuhusu mitandao hususani mtandao wa Facebook. Tulikuwa tukijaribu kufanya tathmini  ili kuona ni kwa kiasi gani mitandao hii inatusaidia hasa sisi wa nchi zinazoendelea.



Kwanza tulipitia akaunti nyingi na kukuta idadi kubwa ya akaunti hizo zina walakini. Kulikuwa na akaunti nyingi sana ambazo hazikuwa na majina ya kweli. Kulikuwa na akaunti nyingi ambazo hazikuwa na picha za kweli za wahusika. Kulikuwa na akaunti nyingi ambazo badala ya picha za watu kulikuwa na picha za maboksi, miti, bendera, wanyama, maua n.k. Kulikuwa na baadhi ya akaunti zilikuwa na jina moja lakini picha ni ya kikundi na hivyo kuwa vigumu kumjua mwenye jina  husika ni nani. Lakini zipo akaunti ambazo zilikuwa ni za halali kwa kila hali.



Utafiti huo kwanza ulituthihirishia kuwa pindi akaunti hizo zilikuwa ni za mizengwe, hata mawazo na uchangiaji wake katika facebook wa hao waongo pia ulikuwa ni wa bandia.  Mengi yaliyokuwa yakielezwa hayakuwa mawazo halisi au mitizamo thabiti. Uchangiaji mwingi ni wa kufuata mkumbo, kijipendekeza, ushabiki njaa, na kejeli.



Kivulini kwetu hatukuwa na nia ya kuingilia uhuru wa mtu wala kukinzana na maboresho ya utandawazi bali tulikuwa tukitaka kujithibitishia kuwa fulsa hii ya mitandao ya jamii imetusaidiaje kwa mtu mmoja mmoja. Ili kupata picha ya nini kipo katika facebook na faida zake nitatoa mifano midogo mitatu.

1. Kuna siku mtu aliweka picha ya jeneza kwenye ukurasa wake. Watu zaidi ya mia tano wali like. Sijaelewa wali like kwa sababu ya urafiki na aliyeliweka ama wali like kwa kulipenda sana jeneza ama vipi. Lakini iwe iwavyo bila ya hata mmoja wapo kutoa maoni yoyote inatia shaka.

2. Inatokea dada anaweka picha yake. Baada ya sekunde kunamiminika like, sifa, na kashfa kibao mpaka wakati mwingine anaamua kuiondoa.

3. Anatokea mtu anaandika neno moja tu NAOMBA; zaidi ya watu elfu watachangia kwa sentesi mojamoja au neno mojamoja. Baada ya mjadala kwisha ndiyo hadithi imekwisha.

Sasa unaweza kukuta mtu kashinda ana facebook lakini hajapata rafiki, hajapata mchumba, hajafanya biashara, hajaongeza japo elimu kidogo ya chochote, hajatoa mawazo wala kuelimisha chochote lakini bando limekwenda, muda umekwenda, macho yameingia giza na vidole vimewasha. Sasa huu mtandao unakuwa umekuweka wapi katika ulimwengu wa sasa.



Hii ni mada inayotugusa wengi sana, na lazima tukasirike kidogo; lakini ukweli unabaki palepale kuwa hatuitumii vizuri hii mitandao. Wenzetu wanauza, wananunua, wanaelimika, wanaelimisha, wanatafuta na wanapata watakavyo kupitia mitandao. Ndugu zangu tusikubali siku ipite hujajifunza au kupata chochote cha nyongeza kutoka katika mtandao.




Saturday, 30 August 2014

WAHAMIAJI HARAMU

  HAPA KWETU FULL KIYOYOZI


Kivulini kwetu tunataka daima mambo yawe mazuri kama ilivyo hapo juu na si vinginevyo kama inavyoonekana hapa chini.


Kwa taarifa tu, hii ninaitoa kama tahadhari kuwa nyie mawakala wa wahamiaji; mchezo wenu ndiyo mauti kwetu.

Habari tulizonazo ni kuwa Kivulini kwetu wahamiaji haramu wamekuwa wengi kupita kiasi . Hatuna uhakika kama watu wa Uhamiaji wanalijua hili kwa mapana yake ama la, lakini iwe iwavyo, mambo yakiharibika wote tutaingia katika matatizo.


Sasa hivi wahamiaji kutoka nchi jirani na za mbali wamekuwa wakipishana mitaani mpaka wenyewe kwa wenyewe wanaanza kukimbiana; lakini sisi wenyeji wala hatuna wasiwasi; tupo tu tunawagawia huduma zote watakazo. Wapo wengi tu wanaouza matunda kwa baiskeli; wapo wanaouza maua na mapazia; wapowanaojifanya makandarasi; wapo wanaojifanya madaktari; wauza vikombe; wasuka nywele; wasanii; wajasiliamali; na wa aina kadha wa kadha. Sasa hivi kila mgeni anatusifia hapa kwetu kwamba KIVULINI KWETU NI FULL KIYOYOZI. Kwamba hapa shida ni kuingia, lakini ukifika ni kama umeingia peponi; hakuna bugudha.

Kitendawili ninachokiona ni kuwa wageni hawa huja mikono mitupu tena kupitia njia za panya, lakini baada ya kipindi kifupi hustawi kushinda hata wenyeji; na ustawi wao huupata kwa kutumia fulsa hizihizi ambazo wakati mwingine wageni tumeshindwa kuzipata. Ni vipi wanafanikisha mambo yao, hilo nalo neno. Anakuja mhamiaji haramu baada ya miezi miwili anapanda cheo anakuwa mwekezaji.



Kwa sasa sio tatizo sana, lakini baada ya muda watazaliana, watanunua ardhi kwa maekali, wataoa shangazi zetu, na wakiwa wengi wanaanzisha kashkash za kwao hapa Kivulini kwetu, kipindi hicho tumejisahau hata madaraka mengine tumewakabidhi. Mbona sisi kwao hatufanyi hivyo na wala hawatuachii tukajimwaga kama sisi tunavyowaachia. Huu wema kuzidi uwezo tumeutoa wapi.

Nimelazimika kusema msije mkasema sikuwaambia.


UBINAADAMU KAZI

KWANI SALAMU KILO BEI GANI ?




 Kwenu msiopenda kusalimia na kusalimiwa,

Kuvulini kwetu wamenituma niwaambie ama niwapashe mpashike kuwa tabia hii mliyonayo ni chafu na inatia kichefuchefu. Tabia yenyewe ni ya kuwa wazito katika salamu. Kwanza hamna utaratibu wa kusalimia watu na mbaya zaidi hata mkisalimiwa hampokei salamu na kama mnapokea basi ni kama mnalazimishwa. Kwani hamjui kuwa salamu ndiyo kipimo cha awali cha ustaarabu wa mtu ? Basi habari ndiyo hiyo.

Watu wa kivulini kwetu wamewachokeni kwa tabia hiyo ya ovyo. Ikiwa hata mbwa, kuku, nyani na wengineo wakikutana wanasalimiana sembuse wewe mwanadamu usiyekuwa na mkia. Kumbe ubinaadamu wako umekalia wapi; miguuni kiunoni ama kichwani ? Kwa kweli mnaudhi.

Nalisema hil ili liwatue vizuri vichwani mwenu. Ebu tuelezeni, tabia hiyo ni kwa vile mna pesa sana, ama ni kwa vile mmesoma sana ama ni kwa ajili gani. Na mseme pia kama mkiwasalimia watu ama mkiitikia salamu za watu mtapungukiwa nini. Na kama mnajua bei ya salamu huko mnunuako tuelezeni salamu kwa kilo mnauziwa bei gani ? Mbona sisi tunajua salamu hazina gharama.

Utawakuta watu hawana cha pesa, hawana cha elimu, hawana sura nzuri; kwanza miguu yao yote ni ya kushoto lakini mabahili kwa salamu kushinda hata nyoka. Nini hasa kinawasumbua ? Mmelogwa ?

Wenyewe ukiwabana utasikia wanasema kwani salamu ni lazima; kwa taarifa yetu ili mradi nyinyi ni binadamu na tuko nanyi katika jamii hii, salamu ni lazima. Ni lazima kwa sababu hatima yako wewe ni kifo na siku ukifa hatutakuacha barabarani utuozee utunukie; tutalazimika sisi kubana pua zetu kukuzoazoa na kwenda japo kukutupa jalalani; sasa sisi utatulipa nini na kipindi hicho kujitambui. Maiti hazikwi na pesa, hazikwi na vyeti, wala hazikwi madaraka, anazikwa mtupu kama alivyozaliwa; sasa mnalinga nini nyie.

 Jambo jingine ni kuwa wewe ni binadamu eti siyo tumbili; na binadamu kama walivyo viumbe wengine tuna taratibu zetu ambazo ni lazima zifuatwe ili tukukubali katika jamii; vinginevyo hamia msituni ukaishi na mafisi wenzio utuache sisi tusalimiane; kwanza hutulishi, hutuvishi na wala wewe sio barabara kusema tutapita wapi.

Ninaongea hivi kwa hasira kutokana na kukerwa. Mtu anakuja msibani anawakuta watu wamejaa, hana salamu hana cha nini anakaa kwenye kiti na kuendelea kubonyezabonyesa kasimu kake ka mchina; hata kuwashika mikono wafiwa anaona tabu; kumbe kilichomleta pale kitu gani. Ama mtu anaingia katika ofisi ya watu hasalimii wala haulizi getini; ili mradi alikwishaongea na mwenyeji wake kuwa atakuja basi. Ama jirani yenu kila siku akiingia au akitoka hasalimii majirani. Hawa ndio wanaosababisha majirani wanafungulia muziki mpaka sauti ya mwisho siku wanaumwa ama wamefiwa katika vyumba vyao.

Hii ni mara yangu ya mwisho kuwakumbusha nyinyi takataka msiojua maana na umuhimu wa salamu; kwamba kuwakumbusha huku si kutaka chochote kutoka kwenu bali ni kuwafahamisha kuwa ubinaadamu kazi hivyo lazima muwajibike kama binaadamu hata kama mlilelewa ndivyo sivyo; salimieni na pokeeni salamu; vinginevyo nendeni mkaishi na majongoo vichakani; mtuondolee kiwingu.

Thursday, 28 August 2014

MTAANI KWETU



        VALANGATI KIVULINI

Ndugu zangu leo Kivulini kwetu kumetokea valangati la kufa mtu.



Majira kama ya saa tano asubuhi maeneo ya mtaa wa madukani niliukuta umati wa watu wakishuhudia patashika nguo kuchanika baina ya akinamama wawili. Vurugu iliyokuwapo pale ilikuwa si ya kuzimwa na wapita njia. Mungu ashukuliwe baada ya msukosuko mkubwa kwa bahati wakapita askari wa Tigo na pikipiki lao ndio waliofanikiwa kumaliza kasheshe ile tena baada ya kulipua kabomu kadogo ka kutoa machozi.



Utulivu uliporejea nikapata fulsa ya kuongea na mmoja wa mashuhuda waliokuwepo kutoka mwanzo ili nijue chanzo cha kadhia hiyo; ndipo nilipopewa mkanda mzima.



Chanzo chetu cha habari kinasema kisa cha ugomvi huo ni mwekezaji wa ndani ambaye ana hotelibaa pale mtaani palipotokea ugomvi. Inasemekana mwekezaji huyo alikuwa amemwajiri dada mmoja kutoa huduma katika mradi huo ambaye kutokana na umahiri wake na bidii yake ya kazi akaamua kumuongeza jukumu la kumhudumia pia yeye mwekezaji binafsi.



Chanzo chetu cha habari kinaendelea kumwaga cheche kwa kusema kuwa baada ya kipindi kifupi tokea mwekezaji huyo amtunukie shahada mhudumu wake akatokea mteja mmoja wa kike ambaye naye kutokana na umaarufu wake katika ile hotelibaa ikapelekea mwekezaji kumtunukia medali ya uteja wa kutukuka na hivyo mbali ya kuwa mteja katika mradi akawa pia mteja wake binafsi.



Changanya kanganya hii iliendelea kwa kipindi cha kama mwezi mmoja hivi bila mteja bora na mhudumu mahiri kutambuana kuwa wapo katika kujenga nyumba moja. Wenyewe wakawa wanacheka na kuchangamkiana sana kiasi cha kuwa mashosti. Lakini wapo baadhi ya wateja na wahudumu katika kiwekezwa hicho ambao walikuwa wanajua kuwa urafiki huo ulikuwa ni wa mashaka; kwamba walikuwa wakila sahani  moja bila wenyewe kugusana mikono.



Kikichotokea leo ni kama ajali. Ilikuwa ni kawaida kwa mwekezaji kumpa kinoti kama kibali mteja bora kumpelekea mhudumu mahiri  ili apewe huduma aliyokuwa anaitaka na pesa atalipa atakapojisikia. Kwa bahati mbaya leo aliandika vinoti viwili; kimoja cha huduma kwa mteja na kingine cha huduma kwa mwekezaji; vikiwa katika karatasi zinazofanana. Kwa uzembe wa mteja bora alipofika kwa shosti wake akajichanganya na kutoa kinoti cha huduma binafsi ya mwekezaji ambamo ndani ya kinoti hicho kulikuwa na jina la mteja bora lililoanza na haneei,  likifuatiwa na saa ya kukutana, mahali pa kukutana, nini cha kufanya na mambo mengine ambayo hayaandikiki na chini ya kinoti hicho kulitiwa saini kwa mbwembwe na mwekezaji mwenyewe.

Mhudumu mahiri baada ya kupokea kinoti hicho kwa makosa na yeye akakosea kumhoji kwa kumuuliza mteja bora ana maana gani kumpatia ujumbe ambao si wake ama ndiyo kantangaze anaianzia kwake. Mteja bila kengere kogonga kichwani kwake akahoji kuwa kama ujumbe haumuhusu maneno yote hayo yanakujaje; kwani inahuu..



Majibizano yakiwa katika hatua za awali, mara akaingia mwekezaji pale hotelibaa; kuingia kwake ikawa kama unazima moto kwa kupulizia gesi asilia. Yakaanza kurushwa maneno, jembe, matusi, vitisho, kutoka pembe hadi pembe; aliyekuwa na masikio ya chuma alisikiliza na mwenye masikio ya mbao alisalimisha masikio yake maana  matusi na kashfa zilizokuwa zikimwagwa pale zilikuwa ni mpya kutoka  dukani ambazo zilikuwa hazijawahi kutumika. Kana kwamba hiyo haitoshi vitendea kazi na bidhaa zikaanza kutumika kama silaha za mapambano na ukumbi wote wa biashara ukawa mbengelembengele; vurumai hadi barabarani. Ilibidi ili kujenga heshima mwekezaji aingie mitini na kuacha gari liende bila dereva maana mambo sasa yalikuwa si mambo.



Baada ya kupata taarifa hiyo nikabaki ninajiuliza kufanya vurugu kiasi hiki wale akina dada mashosti wakati wote ni madoezi maana yake nini na yule mwenye mali aliyeko nyumbani afanyeje ? Na huyu mwekezaji naye huu ndio kweli utaratibu wa kuwekeza; kwa kuwa na mhudumu mpaka binafsi na mteja mpaka binafsi. Kwa staili hii uchumi kivulini kwetu utaimarika kweli ?

Wednesday, 27 August 2014

BARUA PEPE KWENDA USTAWI WA JAMII

WATOTO WA MITAANI NA WALALA MATANGA

Kwenu Waheshimiwa sana Wana Ustawi wa jamii,

Jamii ya Kivulini kwetu imelazimika kutuma barua hii pepe ipeperuke hadi ije kuwapepea enyi waheshimiwa sana ambao kwa hakika tunawategemea.

Madhumuni ya waraka huu ni kuwazindua mkumbuke shuka kabla usingizi haujawakolea na pia kabla ya usiku wa manane ili msijekumbuka shuka wakati kumekucha.



Mara tu baada ya kupokea waraka huu ebu kwa mchana pitieni kwenye makutano yote ya barabara muone jinsi ustawi unavyomomonyoka na kuzorota. Mtajionea jinsi ambavyo wananchi wa kila rika walivyogeuza makutano ya barabara na bustani za miji kuwa makazi rasmi na ya kudumu. Wameweka majiko ya kupikia, fenicha za kukalia na kulalia. Wanafua, wanapika, wanapiga soga na mengine mengi ya kinyumbani yanaendelea.



Baada ya hapo ebu nyakati za usiku piteni mitaa ya masoko muone jinsi ambavyo watu wamelala kuanzia mwanzo wa mitaa hadi inakoishia utadhani kuna misiba iliyounganika mtaa mmoja hadi mwingine.

Yawezekana waheshimiwa mmebanwa na kazi za kuingiza data maofisini; lakini ebu fanyeni mtoke ofisini muende kwenye kwenye viwanja ili mpate kuona jinsi jamii inavyopoteza mwelekeo. Kitendo cha watu milioni kulala nje lazima kuna namna mahali hapajakaa vizuri. Nina uhakika Waziri wa Makazi na Nyumba hajachacha kiasi hicho na wala hajui kuna watu wengi kiasi hicho wanalala nje.


Vinginevyo tuvunje Wizara ya Ustawi tuunde kitu kingine kitakachosaidia kustawisha jamii maana hali kwa kweli ni mbaya na inatisha. Watu wanakutwa wanakoroma barabarani mpaka saa mbili....kwao wapi ?


Monday, 25 August 2014

NGANO ZA KALE

            HEKAYA ZA SUNGURA


Ipo hadithi moja ambayo wengi wetu hatuijui yote bali tunaijua kipande tu; hadithi hii ni ya Sungura mjanja na ndizi mbichi.

Inasemekana kuwa hapo zamani za kale SUNGURA mjanja alikwenda kondeni ambako kulikuwa na migomba ambayo mingi kati yake ilikuwa imebeba mikungu ya ndizi.

Siku hiyo ambayo Sungura aliingia katika shamba hilo alikuwa na njaa sana lakini kwa bahati mbaya mikungu karibu yote ilisheheni ndizi zilizokuwa mbichi japo zilikuwa zimekomaa.

Kutokana na njaa aliyokuwa nayo akaona ni heri ajaribu kufanya maarifa apate japo ndizi kadhaa chache aweze kutuliza njaa yake na ikiwezekana kiasi apelekee wanae. Kwa kutumia nguvu zilizokuwa zimebaki mwilini mwake akatikisa kila mgomba ili aweze kupata chochote; lakini bahati haikuwa yake; hakuna hata ndizi moja iliyoanguka; alichoambulia ni uchovu zaidi.

Baada ya Sungura kuona mambo yameshindikana akaamua kutoka kwa hasira huku akisema SIZITAKI.....MBICHI HIZI. Wakati akiyasema hayo Sungura hakujua kuwa hakuwa peke yake katika lile shamba; alikuwepo SHORE pia. Shore alimwonea huruma sana sungura kwa namna alivyochoka  na  kunyong'onyea kwa njaa kiasi cha kutembea kwa shida kuelekea kwao. Hakumsemesha hata neno moja akamwacha aende zake.

Baada ya siku mbili karibu shamba zima la migomba  ndizi zote ziliiva. Kwa kuwa Shore alikuwa habanduki shambani hata kama ndizi ni mbichi; kwa kuona zimeiva  akamkumbuka Sungura. Akaamua akamwite aje shamba ale kwa kadri atakavyoweza.

Kwa bahati Shore akamkuta Sungura maskani kwake akamwomba wafuatane kwenda shamba. Sungura mwanzoni alikataa katakata kuwa yeye hana haja ya ndizi kwanza ndizi zenyewe mbichi. Lakini baada ya kubembelezwa sana akaamua aongozane na Shore kwenda shambani.

Walipofika shambani Sungura hakuamini macho yake kwani ndizi zote zilikuwa zimebadilika rangi. Shore akamwambia Sungura aanze kutikisa migomba. Katika kutikisa mgomba wa kwanza tu zilidondoka ndizi ambazo kwa siku ile Sungura na familia yake hawangeweza kuzimaliza.

Akiwa mwenye furaha Sungura akamwuliza Shore kuwa amejuaje kuwa ndizi zile zilikuwa zimeiva. Shore akamwambia kuwa yeye huwa habanduki shambani hata kama ndizi mbivu zimeisha bali hukaa humo humo shambani akila matunda mengine hadi ndizi mbichi zinaiva. Hapo ndipo Sungura alipomwangalia Shore kwa mshangao na kutikisa kichwa huku akisema " ama kweli MVUMILIVU HULA MBIVU".